Kansela wa Ujerumani Merkel apambana na maswali ya waandishi
20 Julai 2013Amesisitiza hata hivyo kuwa bado anasubiri majibu kutoka Marekani kuhusiana na suala hilo.
Merkel anaendelea kuwa mgombea mwenye nafasi ya juu katika uchaguzi utakaofanyika hapo Septemba 22, na uchunguzi mpya wa maoni ya wapiga kura unaonesha kuwa kadhia hiyo ya upelelezi wa mawasiliano ya simu na internet sio suala kuu hadi sasa katika uchaguzi.
Matumaini ya wapinzani
Lakini upinzani una matumaini kuwa hali hiyo huenda ikabadilika kwa kuwa vyombo vya habari vinaelekea kulichukulia suala hilo kwa nguvu.
Akishinikizwa na maswali kuhusu mpango wa usalama wa taifa nchini Marekani wa PRISM kwa muda wote wa dakika 100 za mkutano wake wa kila mwaka na waandishi habari wakati wa majira ya joto, Merkel ameendelea kusema kuwa amefahamu kuhusu suala hilo kupitia vyombo vya habari, na hana taarifa za kina na ameomba kuwepo uvumilivu.
Merkel amesisitiza kuwa nchi yake , "sio taifa la kufanyiwa uchunguzi" na kwamba "sheria za Ujerumani zinatakiwa kutumika katika ardhi ya Ujerumani" lakini pia amekiri kuwa hali hiyo ina mipaka yake katika enzi hizi za mfumo wa mawasiliano ya dunia.
Mbinyo umeongezeka kwa wiki kadha dhidi ya Merkel kuhusiana na madai ya upelelezi yaliyotolewa na mfanyakazi wa shirika la ujasusi la Marekani anayetafutwa Edward Snowden, ambaye pia amesema shirika la ujasusi la Ujerumani BND lilishiriki pamoja na shirika hilo la usalama wa taifa nchini Marekani kufanya uchunguzi huo.
Merkel kavunja kiapo
Upinzani wenye nadharia za wastani za mrengo wa shoto umedai kuwa Merkel amevunja kiapo chake cha kuongoza nchi kwamba atalinda haki za raia za mawasiliano ya binafsi , suala ambalo ni nyeti kutokana na historia ya shughuli za askari kanzu chini ya utawala wa Wanazi pamoja na ule wa Ujerumani ya mashariki ya kikomunisti.
Uchunguzi uliofanywa na kituo cha televisheni ya taifa cha ARD umegundua kuwa zaidi ya theluthi mbili ya wapiga kura wa Ujerumani hawaridhishwi na juhudi za serikali kuufahamisha umma juu ya suala hilo.
Hata hivyo , uchunguzi huo huo pia umesema kuwa, takriban kwa sasa, hali hiyo haijabadilisha nafasi ya uongozi aliyonayo kansela Merkel wakati nchi hiyo inaelekea katika likizo za majira ya joto, na kwamba theluthi mbili ya Wajerumani wanasema suala hilo halitaathiri kwa kiasi kikubwa matokeo ya uchaguzi.
Mafanikio ya Merkel
Kansela amesisitiza mafanikio yake katika kuushughulikia uchumi pamoja na jinsi alivyoshughulikia mafuriko ya hivi karibuni , na amesema kuwa serikali yake inayoundwa na vyama vya nadharia za wastani za mrengo wa kulia , kuwa ni ya mafanikio makubwa tangu Ujerumani mbili kuungana mwaka 1990.
Kuhusiana na suala la uchunguzi wa shirika la usalama wa taifa la Marekani NSA, Merkel amezungumzia kitisho cha ugaidi wa kimataifa pamoja na maafa ya kutisha ya Septemba 11 na kusema ni kitu cha kawaida kwa mashirika ya ujasusi kushirikiana, akitaja msaada wa ujasusi wa Marekani hapo zamani kusaidia kujua wahanga raia wa Ujerumani waliotekwa nyara waliko nje ya nchi. Pia amesisitiza kuwa ni muhimu kuwa na mipaka kuhusiana na uchunguzi wa siri wa mataifa, na kwamba katika baadhi ya nyakati , "matokeo hayahalalishi njia ya kupatikana kwake".
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe
Mhariri : Amina Abubakar