1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kamanda wa zamani wa IRA Martin McGuinness afariki

Caro Robi
21 Machi 2017

Aliyekuwa naibu wa waziri wa Ireland Kaskazini Martin McGuinness amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 66 kutokana na matatizo ya moyo. Hayo ni kulingana na chama chake cha kizalendo cha Sinn Fein.

https://p.dw.com/p/2ZcS3
Nordirland Martin McGuinness Politiker
Picha: Reuters/C. Kilcoyne

Taarifa kutoka kwa Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May imesema licha ya kuwa haungi mkono njia aliyoichukua McGuinness hapo awali katika maisha yake, anatambua kuwa alikuwa na wajibu muhimu katika kuliongoza Jeshi la Ukombozi wa Ireland IRA kuachana na ghasia, na kwa kufanya hivyo alichangia pakubwa katika safari ya kipekee ya Ireland Kaskazini kutoka machafuko hadi amani.

Mc Guinness ambaye ni kamanda wa zamani wa Jeshi la Ukombozi wa Ireland, IRA, alikuwa amejiuzulu kutoka siasa mwezi Janauri mwaka huu kutokana na matatizo ya moyo na kuvurugika kwa mahusiano na chama hasimu cha Democratic Unionist, DUP.

Chama cha Sinn Fein kilikataa kumteua kiongozi atakayechukua wadhifa wa McGuinness chamani kutokana na mzozo kati yake na DUP na kupelekea chaguzi za serikali za mitaa mwezi huu ambapo kilijinyaukulia viti vingi.

Kufuatia vuta nikuvute hiyo kati ya Sinn Fein na DUP inamaanisha serikali ya Uingereza huenda ikachagua uongozi wa moja kwa moja kuhusu Ireland Kaskazini kutoka London katika kipindi cha wiki chache zijazo.

Großbritannien Nordirland 2007 Martin McGuinness Ian Paisley Tony Blair Bertie Ahern
Martin McGuinness, Ian Paisley, Tony Blair na Bertie AhernPicha: picture-alliance/dpa/C. Mc Arthur

Miaka kumi iliyopita McGuinness aliweka historia kwa kujiunga na serikali ya mseto na hasimu wake mkubwa Ian Paisley wa chama cha DUP iliyokuwa sehemu muhimu ya mchakato wa kupatikana amani wa Ireland Kaskazini.

Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair mmoja wa waasisi wa makubaliano hayo ya amani ya 1998 amesema hangeweza kufikia makubaliano hayo bila ya uongozi, ujasiri na imani thabiti ya Mc Guinness kuwa yaliyopita hayapaswi kuamua mustakabali wa maisha ya siku za usoni.

Kiongozi wa Sinn Fein Gerry Adams amemtaja McGuinness kuwa Mrepublican aliyejitolea kufanya kazi bila kuchoka kwa ajili ya amani na maridhiano na kuungana kwa taifa lake. Naye kiongozi wa DUP Arlene Foster ametoa taarifa fupi akisema ameshtushwa na kifo chake na kutoa risala zake za rambi rambi kwa familia ya marehemu.

McGuinness alizaliwa mwaka 1950, katika mji wa Derry, kaskazini mwa Ireland Kaskazini. Alijihusisha na makundi ya asasi za kiraia akiwa kijana na kuimarika haraka katika kada za Jeshi la Ukombozi wa Ireland IRA.

Alikuwa anashikilia wadhifa wa pili wa kamanda wa IRA mwaka 1972 wakati Wanajeshi wa Uingereza walipowapiga risasi waandamanaji 26 wa Republican mjini Derry na kuwaua 13 kati yao. Alifungwa jela kwa kuhusishwa na vitendo vya IRA na baadaye alikuwa naibu wa waziri wa Ireland Kaskazini mwaka 2007 akishirikiana na Paisley.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman