Kalou akosolewa kwa video ya mzaha kuhusu corona | Michezo | DW | 04.05.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Kalou akosolewa kwa video ya mzaha kuhusu corona

Mchezaji wa  timu ya Hertha Berlin Salomon Kalou amekosolewa vikali Jumatatu (04.05.2020) kwa kuonyesha mubashara video kuhusu sheria ya kuwataka watu wasikaribiane ikivunjwa.

Mshambuliaji huyo wa Ivory Coast alichukua simu yake Jumatatu (04.05.2020) wakati alipowasalimia wachezji wenzake kupitia ngumi, kupiga makofi na mchambuliaji mwenzake, Vedad Ibisevic, kulalamika kuhusu makato ya mshahara na kumfumania mwenzake ambaye alionekana akipimwa kubaini kama ana virusi vya corona.

Video hiyo, ambayo imeshafutwa mtandaoni, ilioneshwa siku ambayo kitengo cha ligi kinachopanga ratiba za mechi, DFL, kiliporipoti visa 10 vya maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 miongoni mwa timu 36 za ligi kuu na ligi ya daraja la pili, na inakinzana msisitizo uliotolewa na bodi hiyo ya ligi kwamba kila kitu kinafanywa kuzuia kuenea kwa kirusi cha corona.

Video ya Kalou ilimuonesha mchezaji wa Hertha, Jordan Torunarigha, akipimwa na daktari aliyekuwa amevalia barakoa ya kawaida tu kama kinga. Daktari huyo, David de Mel, alirudia mara kwa mara kumuomba Kalou aifute video hiyo, kabla mchezaji huyo kuondoka na kwenda zake akicheka, akisema alikuwa "akifanya mzaha tu."

DFL imeikosoa vikali video hiyo katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa tiwtter. "Picha kutoka kwa Salomon Kalou katika chumba cha kubadilisha nguo cha timu ya Hertha BSC hazikubaliki kabisa. Hakuwezi kuwa na uvumilivu wowote kuhusu picha hizo - pia kutoka kwa wachezaji na vilabu vinavyofuata maagizo, kwa sababu wameelewa ugumu wa hali ilivyo," ilisema DFL.

Jarida la michezo la Kicker la Ujerumani limesema video hiyo itavuruga jitihada za kuianzisha tena ligi ya Bundesliga kwa kuwa ni kama "kichocheo kwa wakosoaji wanaotaka soka la kulipwa liendelee kusimama."

Kansela wa Ujerumani, Angele Merkel, na mawaziri wakuu wa majimbo yote 16 wataamua siku ya Jumatano kama ligi iendelee bila mashabiki uwanjani.

(ap)