1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juventus, AC Milan wafuzu Ligi ya Mabingwa

24 Mei 2021

Mabingwa mara saba wa Ligi ya Serie A, AC Milan wamerudi katika Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya baada ya kukosa kushiriki kinyang'anyiro hicho kwa kipindi cha miaka 8. Wengine waliofuzu kwa mashindano hayo ni Juventus.

https://p.dw.com/p/3tsVn
Fussball I Krzysztof Piatek
Picha: Francesco Scaccianoce/LPS/ZUMA/picture alliance

Mikwaju miwili ya penalti iliyopachikwa wavuni na kiungo wa Ivory Coast Frank Kessie iliwapa ushindi Milan walipokuwa wakicheza na Atalanta ambao tayari walikuwa washafuzu pamoja na mabingwa Intermilan. Stefano Pioli ni kocha mkuu wa AC Milan.

"Nimeridhika kwa sababu nafikiri tumeonyesha kwamba tulistahili kumaliza wa pili kwenye msimamo. Tulionyesha uwezo wetu msimu mzima ila haikuwa rahisi kufika siku ya mwisho ya msimu bila kufuzu. Haikuwa rahisi kwetu ila wachezaji wameonyesha ari yao ya kutaka kuimaliza ligi katika nafasi bora," alisema Stefano Pioli.

Juventus wao walipata ushindi wa 4-1 walipokuwa wakikwaana na Bologna licha ya nyota wao Cristiano Ronaldo kuwa nje ya kikosi cha kwanza katika mpambano huo na kocha wao Andrea Pirlo alikuwa na haya ya kusema baada ya mpambano huo.

Champions League | Juventus v FC Porto
Wachezaji wa Juventus wakisherehekea kufunga bao Picha: Massimo Pinca/REUTERS

"Tuliamua kwamba Ronaldo alicheza mechi kubwa Jumatano katika fainali ya Kombe la Italia, alitumia nguvu nyingi sana kwa hiyo tuliamua kumpumzisha na aingie baadaye iwapo atahitajika. Tuna Alvaro Morata pia kwa hiyo sikuwa na shaka kwamba angecheza vizuri," alisema Pirlo.

Licha ya ushindi huo Juventus walihitaji Napoli wapoteze pointi na hilo lilifanyika baada ya kutoka sare ya bao moja na Hellas Verona na kuishia kumaliza msimu katika nafasi ya tano.