Jose Mourinho anajisikia kama mtoto mdogo | Michezo | DW | 02.03.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Jose Mourinho anajisikia kama mtoto mdogo

Baada ya kushinda kombe la kwanza kuu msimu huu, Chelsea itajaribu kuimarisha udhibiti wake wa kinyang'anyiro cha taji la ligi kuu ya kandanda ya England.

Chelsea watapambana na West Ham Jumatano wiki hii. Vijana hao wa kocha Jose Mourinho waliwabwaga Tottenham Hotspur kwa kuwafunga magoli mawili kwa sifuri jana Jumapili na kunyakua Kombe la Capital One. Lakini pia huenda walipewa sababu nyingine ya kusheherekea baada ya Manchester City kulazwa na Liverpool mabao mawili kwa moja kaatika mchuano wa ligi mapema jana.

Na baada ya kumaliza miaka miwili na nusu bila kunyakua taji lolote kuu, Mourinho alisema ushindi wa Kombe la Capital One umemfanya kujihisi kama mtoto tena. "Ni muhimu kwangu kujiskia kama mtoto mdogo nikiwa na umri wa miaka 52, na kwangu hilo ni muhimu. Nafahamu ninastahili kuijenga timu yangu na hilo tunalifanya lakini mimi hujilisha na mataji. Ni vigumu kwangu kuishi bila kushinda mataji, hata nikifahamu kuwa tunafanya kazi na kujiimarisha kwa ajili ya miaka mingi ijayo. Ni muhimu kwangu pamoja na vijana wangu".

Chelsea sasa inaongoza ligi mbele ya Man City kwa pengo la pointi tano, wakiwa na mchuano wa ziada, hali inayomweka Jose Mourinho katika nafasi nzuri ya kurudia mafanikio ya msimu wake wa kwanza katika klabu hiyo miaka kumi iliyopita.

Katika michuano mingine ya Jumatano, Leicester watakuwa wageni wa Man City. Arsenal ambao waliwacharaza Everton magoli mawili kwa bila jana Jumapili, sasa wako nyuma ya City katika nafasi ya tatu na pengo la pointi nne, wakati Manchester United ikiwa nyuma yao katika nafasi ya nne na pengo la pointi moja tu. Liverpool inafunga nafasi tano bora na tofauti ya pointi mbili nyuma ya Arsenal. Arsenal watachuana na Queens Park Rangers, wakati United wakichuana na Newcastle nao Liverpool watawaalika Burnley.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/reuters
Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com