Je,Ugiriki iachiliwe kufilisika?
26 Februari 2010Wachambuzi katika benki ya Goldman Sachs mjini New York, Marekani, wanaonya kuwa Ugiriki inakabiliwa na changamoto kali kujipatia mikopo na huenda ikashindwa kupata fedha za kugharimia matumizi yake. Kwa maoni ya wataalamu hao, itakuwa vigumu sana kwa serikali ya Ugiriki peke yake kujipatia fedha zinazohitajiwa. Hatimae itahitaji kusaidiwa kutoka nje, iwapo kwa msaada wa fedha au kwa mikopo inayodhaminiwa na mwanachama mmoja mmoja katika Umoja wa Ulaya.
Kwa upande mwingine, gazeti la Financial Times nchini Ujerumani limeripoti kuwa benki kubwa nyingi za Kijerumani zimeamua kutonunua hati za serikali ya Ugiriki kwa sababu ya kuhofia hali ya kifedha inayokutikana Ugiriki. Uamuzi wa benki hizo za Kijerumani unatazamwa kama ishara kuwa ni hatari kuwekeza katika hati za serikali ya Ugiriki. Wasiwasi huo uliongezeka baada ya serikali ya Ugiriki kuarifu kuwa tathmini ya nakisi ya bajeti yake ya mwaka 2009 ni asilimia 12.7 ya pato lake la ndani na sio asilimia 3.7 iliyokadiriwa hapo awali. Tarakimu hizo zimedhihirisha hali mbaya sana ya kifedha na uwekaji hesabu mbovu.
Serikali ya Ugiriki inashinikizwa na Umoja wa Ulaya kuchukua hatua kali zaidi kupunguza matumizi yake katika sekta ya huduma za umma kwa hadi asilimia nne katika mwaka huu. Mapema juma hili, nchini Ugiriki watu waliaandamana kwa maelfu kupinga hatua kali zilizopangwa kuchukuliwa na serikali katika jitahada ya kupunguza nakisi ya bajeti yake.
Nchi zinazotumia sarafu ya Euro katika Umoja wa Ulaya zinafuatilizia kwa makini hali ya uchumi nchini Ugiriki kwani mzozo huo wa fedha umeathiri thamani ya Euro. Waziri wa Fedha wa Luxembourg, Luc Frieden, katika mahojiano yaliyochapishwa leo katika gazeti la kibiashara la Ujerumani, Handelsblatt, amesema, ikihitajika nchi za kanda ya Euro hazina budi kuinusuru Ugiriki kwa maslahi ya mshikamano wa Ulaya.
Mwandishi:P.Martin/AFPE
Mhariri:Othman,Miraji