Jeshi lamuidhinisha Sisi kuwania urais | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.01.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Jeshi lamuidhinisha Sisi kuwania urais

Baraza Kuu la Kijeshi nchini Misri Jumatatu (27.01.2014) limemuidhinisha Jemedari Mkuu Abdel Fattah al- Sisi kuwania urais wa nchi hiyo.

Wananchi wanaomuunga mkono Jemedari Mkuu Abdel Fattah al-Sisi mjini Cairo.

Wananchi wanaomuunga mkono Jemedari Mkuu Abdel Fattah al-Sisi mjini Cairo.

Sisi,ambaye alimpinduwa rais wa itikadi kali za Kiislamu Mohamed Mursi hapo mwezi wa Julai amepata umashuhuri mkubwa akiwa kama kiongozi ambaye anaweza kuitowa Misri kwenye hali ya kuyumba kisiasa na kukomesha umwagaji damu mambo ambayo yamekuwa yakiisibu nchi hiyo tokea mwaka 2011.

Kuchaguliwa kwake katika wadhifa wa urais kutaadhimisha kurudi tena kwa mwanajeshi kama mkuu wa nchi ikiwa ni miaka mitatu baada ya Wamisri kuasi dhidi ya rais Hosni Mubarak mkuu wa zamani wa jeshi la anga.

Shirika la habari la taifa MENA limeripoti kwamba Baraza Kuu la Kijeshi lilikutana kujadili matukio juu ya suala la usalama na madai ya wananchi kutaka Sisi ambaye ni waziri wa ulinzi agombee urais.Sisi anatarajiwa kutangaza kuwa mgombea hivi karibuni.

Atuzwa kwa kazi nzuri

Jemedari Mkuu wa Misri Abdel Fattah al-Sisi.

Jemedari Mkuu wa Misri Abdel Fattah al-Sisi.

Mapema leo hii Rais wa mpito Adly Mansour ametowa agizo la kumpandisha cheo Sisi kuwa Jemedari Mkuu ambaye atabidi ajiuzulu kutoka jeshini iwapo atawania urais.

Afisa mmoja wa serikali akizungumzia kupandishwa cheo huko amesema anafikiri ni kuaga kwa sisi kama mkuu wa majeshi.

Ni nadra sana kwa jeshi la Misri kuwapandisha vyeo maafisa wake waandamizi kufikia ngazi ya Jemedari Mkuu.

Afisa huyo mwandamizi wa serikali amesema "kupandishwa cheo huko kunamaanisha kutunukiwa kwa Sisi" kabla ya kujiuzulu kutoka jeshini.

Jubel auf dem Tahrir-Platz nach Absetzung Mursis

Wananchi wanaomuunga mkono Jemedari Mkuu Abdel Fattah al-Sisi wakiwa katika uwanja wa Tahrir mjini Cairo.

Karim Bitar mchambuzi katika Taasisi ya Ushirikiano wa Kimataifa na Mikakati amesema cheo kama hicho kwa kawaida hutolewa baada ya kupatikana ushindi muhumi vitani jambo ambalo linamaanisha kwamba ukandamizaji unaoendelea hivi sasa na vita dhidi ya ugaidi unahesabiwa kuwa ni ushindi sawa na ule unaopatikana katika medani ya vita.

Bitar anaona kupandishwa cheo huko kama ni hatua mpya katika kujenga hekaya ya muokozi,shujaa na mtu wa vitendo.

Kupandishwa kwa al - Sisi kunamuweka katika cheo sawa na kile alichokuwa akishikilia mtangulizi wake Mohammed Hussein Tantawi, ambaye alikuwa mkuu wa majeshi na waziri wa ulinzi kwa miaka kadhaa chini ya utawala wa Mubarak na ambaye baadae aliingilia kati akiwa kama mtawala wa kijeshi kwa miezi 17 kufuatia kupinduliwa kwa Mubarak katika uasi wa mwaka 2011.Baada ya Mursi kuchaguliwa katika uchaguzi wa kwanza huru wa kidemokrasia hapo mwaka 2012 alimuondowa Tantawi na kumuweka el-Sisi.

Kwa mujibu wa sheria mwanajeshi anaetumikia jeshini hawezi kugombania wadhifa wa urais.

Kiongozi madhubuti

Shabiki wa Jemedari Mkuu Abdel Fattah al-Sisi akibeba picha yake.

Shabiki wa Jemedari Mkuu Abdel Fattah al-Sisi akibeba picha yake.

"Nigelipendelea uchaguzi wa urais uwe na wagombea wa kiraia ili kuweza kuleta demokrasia ya kiraia" anasema hayo Alfred Raouf mwanachama wa chama cha kiliberali cha Al-Dostour.Lakini ameongeza kusema anafahamu kwamba watu wanataka Sisi awe mgombea kutokana na mashaka ya usalama wao ambapo wanataka mtu madhubuti kuongoza nchi.

Hapo Jumapili Rais Mansour alitangaza kwamba uchaguzi wa rais utafanyika mwezi wa Aprili baada ya kufanyia marekebisho utaratibu wa serikali ya mpito uliotayarishwa na serikali iliowekwa na jeshi baada ya kuangushwa kwa Mursi hatua ambayo inaelezwa kuwa imekusudia kumuwezesha mkuu huyo wa majeshi kuwania wadhifa huo wa urais.

Iwapo Sisi atashinda kama inavyotarajiwa na wengi atashawishi matokeo ya uchaguzi wa bunge kwa kuunda chama ambacho kitawavutia wagombea mashuhuri.

Wafuasi wa Mursi wakiaandamana Cairo.

Wafuasi wa Mursi wakiaandamana Cairo.

Lakini Amiri Jeshi huyo ambaye anashutumiwa na wafuasi wa Mursi kwa kufanya mapinduzi dhidi ya rais wa itikadi kali za Kiislam anakabilia na upinzani mkubwa ulijiotolea na aina fulani ya uasi.

Wakati huo huo Naibu Waziri Mkuu wa Misri Ziad Bahaa Eddin ametangaza kujiuzulu katika serikali inayoungwa mkono na jeshi ili kurudi tena katika harakati za kisiasa na kisheria pamoja na kukishughulikia chama chake.Eddin ambaye pia anashikilia wadhifa wa waziri wa ushirikiano wa kimataifa amesema katika taarifa kwamba uamuzi wake huo umekuja baada ya kupitishwa kwa katiba mpya na kuashiria kumalizika kwa awamu muhimu ya mpango ambapo kwayo suala la kutunza umoja na kuondokana na pingamizi zote lilikuwa muhimu.

Baruwa ya kujiuzulu kwake ilikuwa na tarehe 24 Januari.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP

mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com