Jenerali Fonseka apandishwa kizimbani. | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.03.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Jenerali Fonseka apandishwa kizimbani.

Aliyekuwa mkuu wa jeshi la Sri Lanka Sarath Fonseka amefikishwa katika mahakama ya kijeshi kwa makosa ya kujihusisha na siasa wakati bado akiitumikia kazi yake ya jeshi. Kesi hiyo imesababisha wasiwasi mkubwa kisiasa.

default

Aliyekuwa mkuu wa jeshi la Sri Lanka Jenerali Sarath Fonseka.

Kesi hiyo imeanza kusikilizwa leo kwenye makao makuu ya jeshi la majini katika mji mkuu wa nchi hiyo Colombo.

Duru za polisi zinasem akuwa ulinzi umeimarisha mjini humo wakati kesi hiyo ikisikilizwa huku wafuasi kadhaa wa Jenerali huyo wakitawanywa kwa gesi ya kutoa machozi wakati walipojaribu kuandamana.

Jenerali Sarath Fonseka, ambaye alishindwa katika uchaguzi wa Rais uliofanyika nchini humo mapema mwaka huu na Rais wa nchi hiyo ambaye alikuwa akitetea kiti hicho Mahinda Rajapaska, anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo yatasikilizwa tofauti, yanayohusiana na siasa, madai kwamba alikuwa akipanga kufanya mapinduzi dhidi ya serikali.

Anashtakiwa pia kwa kukiuka taratibu za kijeshi na kwamba iwapo atatiwa hatiani anaweza akahukumiwa kifungo cha hadi miaka mitano gerezani.

Takriban watu 35 wanatarajia kutoa ushahidi wao katika kesi hiyo ambayo inaweza kuchukua wiki chache kama sio miezi.

Kamanda huyo wa zamani wa jeshi la Sri Lanka ambaye alikamatwa Februari nane, mwaka huu, amekanusha mashtaka hayo na kusema kuwa yamechochewa kisiasa na pia yana lengo la kumnyima nafasi ya kushiriki katika uchaguzi wa bunge utakaofanyika nchini humo mwezi ujao.

Washirika wa kamanda huyo wa zamani wa jeshi la Sri Lanka wamehoji mantiki ya kumshtaki Jenerali Fonseka katika mahakama ya kijeshi wakati hayupo tena jeshini.

Kiongozi wa chama Janatha Vimukthi Peremuna JVP Somawansa Amarasinghe amesema kukamatwa kwa kiongozi huyo na kuwekwa kizuizini ni kinyume na sheria, kutokana na kwamba Jeneral Fonseka hahusishwi tena na sheria za kijeshi.

Hata hivyo msemaji wa Jeshi la nchi hiyo amekataa kutoa taarifa yoyote kuhusiana na kesi hiyo itakayosikilizwa katika mahakama hiyo ya kijeshi.

Mkuu huyo wa zamani wa Jeshi la Sri- Lanka Jenerali Fonseka na Rais wa nchin hiyo Mahinda Rajapaksa mwaka uliopita walifanyakazi kwa pamoja na kumaliza vita vilivyodumu miaka 25 dhidi ya waasi wa Tamil Tiger waliokuwa wakitaka kujitenga.

Katika kinyang'anyiro cha uchaguzi mkuu wa Rais uliofanyika Januari mwaka huu Jenerali Fonseka alishindwa kwa asilimia 18 na mpinzani wake Rais Rajapaska, na kumtuhumu Rais Rajapaska kwa kufanya udanganyifu wakati wa zoezi hilo.

Kukamatwa kwa Jenerali Fonseka mapema mwezi uliopita kulisababisha maandamano makubwa nchini humo.

Mwandishi: Halima Nyanza(Reuters)

Mhariri Saumu Mwasimba

 • Tarehe 16.03.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/MU1t
 • Tarehe 16.03.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/MU1t
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com