Jamhuri ya Kongo yafanya kura ya maoni | Matukio ya Afrika | DW | 25.10.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Jamhuri ya Kongo yafanya kura ya maoni

Shughuli za upigaji kura ya maoni zimeanza polepole katika Jamhuri ya Congo kuamua ikiwa Rais Dennis Sassou Nguesso mwenye umri wa miaka 71 anaweza kuwania muhula wa tatu kwenye uchaguzi wa mwaka ujao.

Rais Sassou Nguesso wa Jamhuri ya Kongo ambaye anataka kuendelea kukaa madarakani

Rais Sassou Nguesso wa Jamhuri ya Kongo ambaye anataka kuendelea kukaa madarakani

Nguesso ni kiongozi wa hivi punde barani Afrika ambaye ametawala kwa muda mrefu kutafuta njia ya kisheria kuongeza kipindi chake uongozini. Juhudi kadhaa kama hizi zimeibua ghasia,watu wanne waliaga dunia nchini Congo wiki ilyopita wakati maafisa wa usalama walipowapiga risasi waandamanaji.

Siku ya Jumanne serikali ilisema watu wanne waliaga dunia kwenye mapigano kati ya waandamanaji wa upinzani na maafisa wa usalama huko Brazaville na pia mjini Pointe-Noire.

Mwito wa upinzani kususia kupiga kura na ukosefu wa vifaa kumechangia kuwepo kwa idadi ndogo ya wapiga kura katika vituo vingi vya kupigia kura kulingana na mashuhuda.Wamesema katika vituo vingine wapiga kura pekee walioonekana ni wanachama wa vikosi vya usalama.

Vifo katika maandamano

Wapinzani wamewataka watu waisusie kura hiyo ya maoni

Wapinzani wamewataka watu waisusie kura hiyo ya maoni

Lakini kiongozi wa upinzani Paul-Marie Mpouele alidai siku ya Ijumaa kuwa zaidi ya watu 20 waliaga dunia kwenye mzozo huo na akataka wafuasi wa upinzani kukataa kushiriki kwenye kura hiyo ya maoni na pia matendo yoyote ya uvunjaji sheria.

Kamishna wa tume ya uchaguzi nchini humo amesema "wakati vifaa vya kupiga kura viliwasili katika kituo cha kupiga kura usiku hakukua na mtu wa kuvipokea, hivyo walilazimika kuviacha katika kituo cha polisi"

Amesema asubuhi hii mkuu wa kituo cha kupiga kura alilazimika kuchukua vifaa hivyo kutoka kwenye kituo hicho cha polisi na hii ndiyo sababu kuchelewa huko.

Wachambuzi wameonya kutokea kwa mapigano zaidi nchini humo yenye utajiri wa mafuta.Wakazi kadhaa wamehama kutoka kusini mwa maeneo yaliyo jirani ya Brazaville hadi maeneo mengine siku ya Jumamosi ili kuepuka mapigano,ingawa wengine wamesema wanahofia hawataweza kupiga kura kutokana na hali hiyo.Wengine wamelalamika kuwa hawajapokea kadi zao za kupigia kura.

Nguesso ameongoza kwa miaka 31 kati ya miaka 36 iliyopita.Alishinda uchaguzi wenye utata wa mwaka 2002 na 2009 na kulingana na katiba pia umri wake haruhusiwi kuwania tena uongozi.

Wimbi la kubadilisha katiba Afrika

Kiongozi wa Burkina Faso ambaye aliongoza nchi yake kwa miaka 27 alifukuzwa madarakani Oktoba iliyopita kufuatia maandamano. Kuna michakato inayoendelea pia Rwanda na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo kutaka kuzibadilisha katiba.

Mabadiliko hayo ya kisheria ni changamoto kwa serikali za magharibi -wanaweza kuunga mkono viongozi ambao wametawala kwa muda mrefu au wasisitize uzingatiaji wa muhula wa kuhudumu.

Congo ilitawaliwa zamani na Ufaransa na Rais Francois Hollande alisema wiki iliyopita kuwa Sassou Nguesso ana haki ya kupata ushauri kutoka kwa raia wake.

Askofu wa Brazzaville Anatole Nilandou ametoa mwito kwa vyama mbalimbali vya kisiasa kufanya mazungumzo kuhusu mzozo huo ulioibuka kuhusu kuwania tena kwa Sassou Nguesso kwa awamu nyingine 2016.

Misafara yoyote ya magari ilipigwa marufuku katika barabara za Brazzaville siku ya Jumapili ila tu ya maafisa wa polisi na walio na vibali rasmi vya polisi.

Mji huo mkuu ulikuwa kimya wakati wa kuanza kwa shughuli za kupiga kura.

Mwandishi:Bernard Maranga/Reuters/AFP
Mhariri: Daniel Gakuba

DW inapendekeza