Jamhuri ya Afrika ya Kati yahitaji walinda amani kwa dharura | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.03.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Jamhuri ya Afrika ya Kati yahitaji walinda amani kwa dharura

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wamesema kuna haja ya dharura ya kutuma kikosi cha kulinda amani Afrika ya Kati lakini hakutakuwa na ufumbuzi wa haraka kwa mzozo wa nchi hiyo ambapo gharama zake zinatajwa kuwa ni kubwa mno.

Wanajeshi wakiwa katika doria mji mkuu wa Afrika ya Kati Bangui.

Wanajeshi wakiwa katika doria mji mkuu wa Afrika ya Kati Bangui.

Toussaint Kongo-Doudou waziri wa mambo ya nje wa Jamhuri ya Afrika ya Kati akitowa ombi kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Alhamisi (06.03.2014) amekaririwa akisema "Tafadhali tunahitaji msaada wenu iwapo utakawia kupatikana utakuwa hauna maana.Huenda hata tukaipoteza nchi."

Waziri huyo amesema hakuna mbadala katika suala la kunusurika na kwamba nchi yake iko katika hatari ya kugawika.Ameomba kutumwa kwa haraka kwa kikosi cha kulinda amani cha kimataifa nchini humo kuimarisha vikosi vya Ufaransa na Umoja wa Afrika ambavyo tayari viko nchini humo vikijitahidi kudhibiti mauaji ya kidini kati ya Wakristo na Waislamu.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekutana kujadili pendekezo la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon la kutuma kikosi cha wanajeshi wa kulinda amani 12, 000 nchini humo.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika mojawapo ya vikao vyake mjini New York,Marekani.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika mojawapo ya vikao vyake mjini New York,Marekani.

Balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa Gerard Araud amesema atasambaza azimio wiki zinazokuja na ametabiri kutafikiwa muafaka juu ya azimio hilo lakini amesema kutakuwa na mazungumzo magumu juu ya namna ya kupunguza gharama za shughuli hiyo.Marekani imeelezea kuunga mkono kwake operesheni hiyo ya kulinda amani ambapo balozi wake katika Umoja wa Mataifa Samantha Power amekaririwa akisema wako tayari kushirikiana kwa karibu na washirika kuanzia sasa. Hata hivyo utawala wa Rais Barack Obama wa Marekani itabidi ulishawishi bunge la Marekani kugharamia operesheni hiyo.

Gharama ni kubwa mno

Mkuu wa shughuli za kulinda amani za Umoja wa Mataifa Herve Ladsous ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba kikosi hicho kinachohitajika kitafanya shughuli zake kwenye mazingira yatakayokuwa na changamoto kubwa. Amesema "Hakutakuwa na ufumbuzi wa haraka Jamhuri ya Afrika ya Kati.Kukabiliana na mzozo huo kutahitaji wakati na kutahitaji rasilmali. Kiwango cha mahitaji Afrika ya Kati ni kikubwa mno."

Herve Ladsous Mkuu wa Shughuli za Kulinda Amani za Umoja wa Mataifa.

Herve Ladsous Mkuu wa Shughuli za Kulinda Amani za Umoja wa Mataifa.

Ladsous anakiri kwamba gharama za shughuli hizo za kulinda amani zitakuwa kubwa lakini kusubiri kuchukuwa hatua anasema kutakuwa na gharama kubwa zaidi kwani mzozo huo unaweza kuwa na taathira mbaya kwa utulivu wa kanda nzima ikiwa ni pamoja na kugawika kwa nchi hiyo na kuanzishwa kwa makundi ya watu wenye itikadi kali.

Umoja wa Mataifa unakadiria gharama za shughuli hizo ambapo wanajeshi watawekwa kwa awamu ili kupunguza gharama,zinaweza kufikia mamilioni ya dola kwa mwaka.

Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema Waislamu wengi wamelazimika kukimbia kutoka eneo la magharibi mwa nchi hiyo ambapo raia wako katika hatari ya kuuwawa.Amesema mzozo huo umewalazimisha watu 290,000 kukimbilia nchi jirani na raia wengine wa kigeni 80,000 wameikimbia nchi hiyo.

Maelfu ya watu wameuwawa Jamhuri ya Afrika Kati tokea nchi hiyo itumbukie kwenye machafuko na mauaji kwa misingi ya kidini mwaka mmoja uliopita.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/AP

Mhariri:Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com