1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

India yatangaza sheria ya kutotoka nje

Saumu Mwasimba
25 Machi 2020

Wananchi wa India wameanza kubakia majumbani kufuatia tangazo la serikali la sheria ya kuwazuia watu kutoka nje kuzuia maambukizi ya virusi vya Corona. Lakini pia maelfu wakimbilia madukani kununua mahitaji

https://p.dw.com/p/3a0WP
Indien Kalkutta Coronavirus
mji wa KolkattaPicha: DW/P. Tiwari

Bado ulimwengu unahangaika kuzuia kusambaa kwa virusi vya Corona na India ndiyo inayozungumziwa zaidi hii leo(25.03.2020) baada ya kutangaza kufunga shughuli zote nchini humo kuanzia usiku wa kuamkia leo Jumatano.

Waziri mkuu Narendra Modi alitangaza sheria hiyo kiasi masaa manne kabla ya kuanza kutekelezwa. Na umma wa watu ulianza kumiminika kwenye maduka ya vyakula na dawa kufanya manunuzi kukabiliana na hali hiyo.

Leo Jumatano nchi hiyo yenye idadi ya watu bilioni 1.3 imeingia kwenye hali ya taharuki kubwa ambapo bado watu walikimbilia madukani kufanya manunuzi ya kujikimu katika kipindi cha wiki tatu za kukaa majumbani.

Waziri mkuu Modi pia aliweka wazi kwamba huduma muhimu zitaendelea kutolewa ikiwemo kuachwa wazi maduka ya dawa na watu wataruhusiwa kwenda kufanya manunuzi ya chakula na dawa.Hata hivyo hakuna usafiri wowote ulioonekana barabarani katika maeeneo mengi ya India nchi ambayo inajukana kwa msongamano wa watu na magari.

Indien Coronavirus
Picha: DW/S. Ghosh

Baadhi ya wananchi wamesikika wakilalamika kwamba wanashindwa kwenda kununua dawa kwasababu hakuna usafiri. Baadhi ya wenye maduka ya chakula mjini New Delhi pia wamelalamika kwamba polisi chungunzima wamewazunguka kwasababu ya kufungua maduka.Wanasema hakuna utaratibu uliowekwa wazi bali ni kizaazaa kinachoendelea, polisi wanawapa amri ya kufunga maduka wakati serikali imeyataka maduka ya chakula kufanya kazi.

Lakini pia chama cha madaktari nchini humo kimeripoti kwamba baadhi ya madaktari wanaotibu walioambukizwa wanatimulia majumbani mwao kwa nguvu kutokana na majirani kuwa na hofu kwamba huenda na wao wameambukizwa na wanaweza kuvisambaza virusi kwa majirani. Mpaka sasa India ina wagonjwa 536 na vifo 9 kutokana na virusi vya Corona.

Narendra Modi na wataalamu wa afya walionya kwamba india ambayo ni nchi ya pili yenye idadi kubwa ya watu duniani inakabiliwa na hatari kubwa ya kuwa na wimbi la maambukizi ikiwa hatua kali hazitochukuliwa.Kwengineko Sri Lanka imewakamata mamia ya watu wanaotuhumiwa kukiuka amri ya kuwataka watu wakae majumbani kuzuia maambukizi ya Corona.

Bundestag Abgeordnete applaudieren medizinischen Helfern
Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Na  bunge la Ujerumani linakutana kupitisha mpango wa kiuchumi kukabiliana na hali nchini. Korea Kusini nayo inajiandaa kuipelekea Marekani vifaa vya kupima virusi vya Corona baada ya rais Trump kuomba msaada huo. Na barani Afrika nchi mbali mbali zimeshachukua uamuzi wa kufunga shughuli zote na kuwataka watu kutotoka majumbani kukabiliana na maambukizi ya virusi hivyo vinavyosambaa kwa kasi huku pia wasiwasi ukiongezeka katika bara hilo juu ya hali ya kiuchumi ya watu wenye kipato kidogo. Afrika Kusini ndiyo inayoongoza barani humo kwa idadi ya walioambukizwa ambapo kuna visa 554 za wagonjwa. Idadi jumla duniani ya walioambukizwa virusi hivyo ni watu laki mbili.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Josephat Charo