1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ILO: Idadi ya wanaofanya kazi za kulazimishwa imeongezeka

19 Machi 2024

Ripoti ya Shirika la Kazi la Kimataifa(ILO) imeonya kuhusu ongezeko la idadi ya watu wanaofanya kazi za kulazimishwa pamoja na faida kubwa itakonayo na vitendo hivyo vya unyonyaji.

https://p.dw.com/p/4duIs
Malawi, Lilongwe
kijana akinyanyua matofali na kuyapeleka kwenye tanuru ambapo yatachomwa wakati wa kazi ili kupata pesa katika Kijiji cha Jumpha.Picha: Amos Gumulira/AFP/Getty Images

Jumla ya faida haramu kutokana na kazi ya kulazimishwa imeongezeka na kufikia dola bilioni 64 ambayo ni asilimia 37 tangu 2014. Hii ikiwa ongezeko kubwa ambalo limechochewa na ukuaji wa idadi ya watu wanaolazimishwa kufanya kazi, pamoja na faida kubwa inayotokana na unyonyaji wa waathirika.

Soma pia: Shirika la ILO laonya kuhusu ongezeko la idadi ya watu wanaofanya kazi za kulazimishwa

Ripoti ya ILO, inakadiria kuwa wafanyabiashara na wahalifu wanakusanya karibu dola 10,000 kwa kila mwathirika, ambapo awali walikusanya dola 8,269 muongo mmoja uliopita.

Jumla ya faida haramu ya kila mwaka kutokana na kazi za kulazimishwa ni kubwa zaidi barani Ulaya na Asia ya Kati ambako wanakusanya takriban dola bilioni 84, ikifuatiwa na Asia na Pasifiki dola bilioni 62, Amerika dola bilioni 52, Afrika dola bilioni 20, na mataifa ya ghuba yakikusanya dola bilioni 18.

Kulingana na Manuela Tomei, Mkurugenzi katika Idara ya Masharti ya Kazi na Usawa katika shirika la ILO amesema takriban watu milioni 27.6 wamehusishwa na kazi za kulazimishwa kwa mwaka wa 2021.

"Hakuna eneo ambalo lina kinga dhidi ya kufanya kazi za kulazimishwa. Hakuna sekta ya uchumi ambayo haiepukiki na kazi ya kulazimishwa. Na kwa kweli, makadirio yetu yanatoa takwimu, kuanzia kwenye viwanda vya uzalishaji hadi kilimo, kazi za ndani, biashara unyonyaji wa kingono."

Aidha ripoti hiyo inadokeza kwamba ukahaba wa kulazimishwa ulichangia faida hizo kwa asilimia 73.

Hatua za kukomesha

Utumikishwaji wa watoto
Mvulana wa Bangladesh Aslam (umri wa miaka 9) anafanya kazi katika kiwanda cha puto huko Kamrangir Char.Picha: dpa

Katika mapendekezo yake ripo hiyo inasisitiza haja ya haraka ya uwekezaji katika hatua za utekelezaji ili kukomesha mtiririko wa faida haramu na kuwawajibisha wahusika.

Inapendekeza pia kuimarisha mifumo ya kisheria, kutoa mafunzo kwa maafisa wa utekelezaji, kuimarisha ukaguzi hasa katika sekta zilizo hatarini zaidi, na kuweka uratibu bora kati ya utekelezaji wa sheria za kazi na uhalifu.

Soma pia: ILO: Mizozo yachangia kudorora kwa soko la ajira duniani

Hata hivyo kazi za kulazimishwa haziwezi kukomeshwa kupitia hatua za utekelezaji wa sheria pekee, bali hatua za utekelezaji lazima ziwe sehemu ya mbinu ya kina ambayo inatoa kipaumbele kushughulikia sababu kuu na kuwalinda waathiriwa.

 

APE//dpa