IDHAA YA KISWAHILI | DW
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo
Matangazo
Matangazo

Habari

Habari za Ulimwengu | 24.05.2020 | 15:00

Waandamanaji Hong Kong wapinga mswada wa sheria kali juu ya usalama wa taifa uliopendekezwa na China

Polisi wa jiji la Hong Kong wametumia gesi ya kutoa machozi na maji ya kuwasha ili kuwakabili maelfu ya waandamaji waliojitokeza kupinga mswada wa sheria kali juu ya usalama wa taifa uliopendekwa na China. China inakusudia kuiweka sheria hiyo katika jiji la Hong Kong ili kuzuia uhujumu, usaliti na nyendo za kujitenga. Wapinzani wa sheria hiyo wanasema inaenda kinyume cha kanuni ya nchi moja mifumo miwili, inayohakikisha uhuru wa jimbo la Hong Kong. Makundi ya waandamanaji waliokusanyika kuupinga mswada huo wa sheria walitoa kauli mbiu za kusisitiza msimamo wa pamoja na ukombozi wa Hong Kong. Watu wapatao 120 walikamatwa na polisi kwa kujiunga na mikusanyiko isiyoruhusiwa. Polisi wamesema waandamanaji waliwarushia mawe na kuwapulizia unyevunyevu usiojulikana. Kwa mujibu wa taarifa ya polisi maafisa wanne wamejeruhiwa.

Waislamu washerehekea Idd ul fitri chini ya vizuizi vya kukabiliana na corona

Waislamu kote duniani wanasherehekea sikukuu ya Eid al-Fitr huku wengi wakiwa chini ya vizuizi vilivyowekwa na mataifa kukabiliana na kuenea kwa virusi vya corona. Sherehe hizo zimeandamwa na kiwingu cha janga la corona huku nchi nyingi duniani zikitangaza kurejesha vizuizi ambavyo kwa sehemu vililegezwa wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan. Katika hali ya kupunguza msisimko wa sherehe hizo mataifa kadhaa ikiwemo Saudi Arabia, Uturuki, Misri na Syria yamepiga marufuku ibada za umma, moja ya tukio muhimu katika sikukuu ya Eid, kwa lengo la kuzuia kusambaa virusi vya corona. Sikukuu ya Eid huashiria kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramdhan na huadhimishwa kwa ibada ya swala, dhifa za chakula na manunuzi ya zawadi pamoja na mavazi.

Wafilipino waonya dhidi ya matumizi ya sindano za dawa ya Fabunan inayodaiwa kutibu corona

Wizara ya afya nchini Ufilipino imewaonya umma ambao ni watumiaji wa mitandao ya kijamii dhidi ya kuweka jumbe kuwa dawa ya kufubaza virusi vya corona iliyotengenezwa na daktari wa nchi hiyo inaweza kukinga na kutibu virusi vya corona. Mamlaka ya chakula na dawa nchini humo (FDA) imetahadharisha dhidi ya matumizi ya sindano iliyo na dawa hiyo ya Fabunan kufuatia ripoti kwamba watu wengi wanainunua hii ikiwa ni kwa mujibu wa naibu Waziri wa ufilipino Maria Rosario. Maria amesema mamlaka ya FDA itaendelea kutoa taarifa kwa umma nchini humo juu ya maendeleo yoyote ya kitabibu ya kukabiliana na COVID 19. Ruben Fabunan, daktari ambaye kwa sasa anaishi Marekani alitengezea dawa hiyo pamoja na kaka zake watatu ambao pia ni madaktari.

China inakaribisha juhudi za kutambua chanzo cha virusi vya corona lakini kwa masharti

Waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi amesema taifa hilo liko wazi kushirikiana na jamii ya Kimataifa ili kutambua chanzo cha mripuko wa virusi vya corona lakini ametahadharisha kuwa uchunguzi ufanyike bila kuingiliwa kati kisiasa. Wangi Yi ameifokea Marekani kwa kile alichokiita juhudi za wanasiasa wa taifa hilo kueneza uvumi kuhusu chanzo cha mripuko huo na kutaka kuinyanyapaa China. Yi amesema hali hiyo inaweza kusababisha nchi hizo kurejea tena katika enzi za vita baridi. Marekani na Australia katika wiki za hivi karibuni zimetaka kufanyika uchunguzi kamili juu ya chimbuko hasa la virusi hivyo. Rais wa Marekani Donald Trump pamoja na Waziri wake wa mambo ya kigeni Mike Pompeo wameishutumu China kwa kutokuwa wazi kuhusu virusi hivyo, na mara kadhaa wamerejelea semi zao kwamba virusi vya corona vimetoka katika maabara ya China.

Benjamin Netanyahu afika mahakamani kusikiliza kesi yake ya rushwa.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netayahu amefika mahakamani leo kusikiliza kesi ya rushwa inayomkabili. Waziri Mkuu huyo aliye na miaka 70 aliwasili katika mahakama hiyo mjini Jerusalaem akiandamana na walinzi wake. Netanyahu anatuhumiwa kwa makosa ya udanganyifu, kupoteza uaminifu na rushwa. Benjamin Netanyahu aliyeweka historia ya kuwa Waziri Mkuu aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi nchini Israel amesema keshi dhidi yake ni njama ya kutaka kuipindua serikali na akaapa kuendelea kuiongoza serikali licha ya kukabiliwa na kesi hiyo. Amesema kwa ushirikiano wa kila mmoja ataendelea kuiongoza Israel na kushughulikia masuala muhimu ikiwemo kufufua uchumi, ajira pamoja na kuuimarisha usalama wa taifa hilo Mashariki ya kati.

Papa Francis awataka waumini wa kikatoliki kufikiria njia za kulinda na kuimarisha mazingira

Watu Jumapili ya leo walirejea katika uwanja wa kanisa la mtakatifu Petro kupata baraka za kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis kutoka kidirisha cha kanisa hilo kwa mara ya kwanza ndani ya takriban miezi mitatu wakati akitoa wito kwa dunia kutafakari kuhusu masuala ya mazingira. Ni watu wachache tu waliofika katika uwanja huo uliofunguliwa tena siku ya Jumatatu wiki iliyopita baada ya kufungwa ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona. Papa Francis amewahimiza waumini wa kikatoliki kutafakari juu ya mazingira kwa miezi 12 ijayo namna ya kuimarisha na kulinda mazingira na namna ya kuwasaidia wale wanaoathirika na mabadiliko ya tabia nchi.

Miito zaidi ya kumtaka Dominic Cummings ajiuzulku yatolewa Uingereza

Wabunge kadhaa kutoka chama tawala cha kihafidhina wamejiunga na wenzao wa chama cha upinzani kumtaka mshauri wa Waziri Mkuu Boris Johnson, Dominic Cummings kujiuzulu kwa madai ya kukiuka vizuizi vya kitaifa vilivyowekwa kupambana na virusi vya corona. Cummings ametetea uamuzi wake aliouchukua mwishoni mwa mwezi machi, wa kusafiri maili 250 kutoka jiji la London hadi mjini Durham kwa wazazi wake kaskazini Mashariki mwa Uingereza baada ya mkewe kuonesha dalili za ugonjwa wa COVID 19. Vizuizi hivyo vilivyoanza kutekelezwa Machi 23 vilitaka watu wabakie nyumbani na kutoka nje kwa mahitaji muhimu pekee na kufanya mazoezi. Mtu yeyote aliyekuwa na dalili za corona alitakiwa kujiweka karantini.

Matukio ya kisiasa

Matukio ya Afrika

Masuala ya jamii

Michezo

Habari kwa lugha ya Kiingereza

Matangazo
Tazama vidio 02:38