IDHAA YA KISWAHILI | DW
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo
Matangazo
Matangazo

Habari

Habari za Ulimwengu | 02.07.2020 | 15:00

Muungano wa kijeshi wa Saudia waanzisha operesheni dhidi ya waasi wa Yemen

Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia umethibitisha kuwa umeanzisha operesheni mpya dhidi ya Wahouthi nchini Yemen na kuonya kuwa utaulenga uongozi wa waasi hao kufuatia mashambulizi ya makombora na ndege zisizoruka na rubani katika taifa hilo la kifalme. Wakaazi wa mji mkuu unaodhibitiwa na waasi, Sanaa wamesema kumekuwa na milipuko mikubwa kuona moshi mkubwa jana baada ya mashambulizi ya angani kuulenga uwanja wa ndege wa kimataifa, ambao uko karibu na kituo cha jeshi la angani. Waasi wa Houthi wanaungwa mkono na Iran wamesema kwenye televisheni yao ya Al-Masirah kuwa muungano huo umefanya mashambulizi 57 ya angani mjini Sanaa na katika ngome yao ya kaskazini ya Saada. Msemaji wa muungano huo wa kijeshi Turki al-Maliki amewaambia waanahabari mjini Riyadh, kuwa operesheni hiyo imefanywa kama jibu la kitisho cha wapiganaji wa Houthi baada ya kuanzisha mashambulizi ya makombora na ndege zisizoruka na rubani kutokea mji mkuu wa Sanaa pamoja na Saada.

Makundi hasimu ya Palestina yaonyesha umoja wa nadra dhidi ya unyakuzi

Makundi hasimu ya Kipalestina ya Hamas na Fatah leo yamechukua hatua ya nadra ya kuonyesha umoja kupitia mkutano wa njia ya video, yakinuwia kushirikiana dhidi ya mipango ya Israel ya kutaka kunyakua maeneo yanayokaliwa ya Ukingo wa Magharibi. Jibril Rajoub, katibu mkuu wa kamati kuu ya kundi la Fatah, alizungumza akiwa Ramallah na Salah al-Arouri, mkuu wa tawi la kisiasa la Hamas akiwa mjini Beirut, na kusema kwamba wakati umefika kwa makundi hayo mawili kutenda kile kinachotarajiwa kutoka kwao, na kuonyesha umoja huku wakipinga mipango ya Israel na mshirika wake Marekani. Wapalestina wamepinga vikali mpango wa amani wenye utata uliopendekezwa na Rais wa Marekani, Donald Trump kuhusu Mashariki ya Kati. Mpango wa Israel unategemewa kuongozwa na mpango huo wa Marekani, ambao unairuhusu Israel kunyakuwa asilimia 30 ya ardhi ya Ukingo wa Magharibi, ambayo ilichukuliwa kwa nguvu na Israel tangu mwaka 1967

Mjumbe wa zamani wa Libya alituhumu Baraza la Usalama kwa unafiki

Aliyekuwa mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya amelituhumu Baraza la Usalama kwa unafiki na kwa kuhujumu juhudi zake za kuleta amani katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini iliyoharibiwa kwa vita. Katika mahojiano yaliyorushwa leo, Ghassan Salame amesema wengi wa wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wanaunga mkono operesheni ya kijeshi iliyoanzishwa mwaka jana na kamanda wa Libya Khalifa Haftar kuukamata mji mkuu Tripoli, kutoka mikononi mwa serikali inayotambulika na jumuia ya kimataifa. Yalikuwa mahojiano yake ya kwanza tangu alipojiuzulu kutoka wadhifa huo mnamo Machi mwaka huu. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amemwambia Kamanda wa vikosi vya mashariki mwa Libya, Khalifa Haftar kuwa hapatakuwa na suluhisho la kijeshi kwa mzozo aliouanzisha Aprili 2019 dhidi ya serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa yenye makao yake mjini Tripoli.

Zaidi ya watu 160 wauawa nchini Myanmar katika mgodi wa madini

Miili ya karibu wachimba migodi 160 wa madini ya jade wameopolewa kutoka kwenye tope baada ya maporomoko ya ardhi kutokea kaskazini ya Myanmar hii leo, katika mojawapo ya ajali mbaya kabisa kuwahi kuikumba sekta hiyo yenye hatari kubwa. Mkasa huo umetokea baada ya mvua kubwa kunyesha karibu na mpaka wa China katika jimbo la Kachin. Idara ya Zima Moto ya Myanmar imesema wachimba migodi hao walifunikwa na wimbi la tope na mpaka sasa miili ya watu 162 imepatikana. Polisi ya eneo hilo imesema waathiriwa walikaidi onyo la kutofanya kazi katika migodi hiyo wakati wa mvua. Shughuli ya utafutaji na uokozi imesitishwa kwa muda kwa sababu ya mvua kubwa. Watu hufariki kila mwaka wakati wakifanya kazi katika sekta hiyo yenye faida kubwa, lakini isiyodhibitiwa ipasavyo ya madini ya jade, ambayo inawatumia wafanyakazi wahamiaji wanaopewa malipo duni kuchimba madini hayo yanayothaminiwa sana nchini China.

Putin awashukuru Warusi kwa kumuunga mkono na imani baada ya kura

Rais wa Urusi Vladmir Putin, amewashukuru Warusi baada ya kuidhinisha kwa kishindo marekebisho ya katiba ambayo yatamruhusu kurefusha utawala wake hadi 2036. Putin amelihutubia taifa kupitia televisheni baada ya tangazo kutoka tume ya uchaguzi ya Urusi kuwa karibu asilimia 78 ya wapiga kura waliunga mkono marekebisho ya katiba. Rais huyo amesisitiza kuwa mabadiliko hayo yalihitajika kwa sababu yanaimarisha mfumo wa kisiasa na kuboresha huduma za kijamii pamoja na kuongeza nguvu uhuru wa nchi hiyo. Hakutaja chochote kuhusu ukweli kwamba mabadiliko hayo pia yatauweka upya ukomo wa muhula wake kikatiba, yakimruhusu kubakia madarakani kwa miaka mingine 12 baada ya kumalizika kwa muhula wake wa sasa mwaka wa 2024.

Mjumbe wa amani Marekani kuanzisha mazungumzo ya kumaliza vita Afghanistan

Mjumbe wa Amani wa Marekani amewaambia maafisa wa Pakistan kuwa kundi la Taliban la Afghanistan na viongozi wa kisiasa wa serikali wanakaribia kuanza mazungumzo ya kuamua mustakabali wa Afghanistan baada ya vita, ikiwa ni hatua muhimu inayofuata katika mpango wa uliosainiwa na Marekani na Taliban Februari mwaka huu. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ubalozi wa Marekani mjini Islamabad, ni kuwa Zalmay Khalilzad alikuwa katika jimbo hilo kusafisha njia ya mazungumzo ya Waafghanistan yanayotarajiwa kuanza baadaye mwezi huu. Hakuna terehe iliyotangazwa, lakini Rais wa Afghanistan, Ashraf Ghani amesema kuwa duru ya kwanza itaandaliwa mjini Doha ambako Taliban wana ofisi yao ya kisiasa.

Moto waharibu jengo la kinu cha nyuklia Iran

Moto umezuka mapema leo katika jengo lililoko juu ya kinu cha nyuklia cha chini ya ardhi nchini Iran, ijapokuwa maafisa wamesema haukuathiri operesheni zake au kusababisha kuvuja kwa mionzi. Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran limeupuuza moto huo likiuita tu "tukio" ambalo liliathiri tu ujenzi unaoendelea wa jengo la kiwanda. Msemaji wa shirika hilo, Behrouz Kamalvandi na mkuu wa nishati ya nyuklia wa Iran, Ali Akbar Salehi walifika haraka katika kinu hicho cha jimbo la Natanz, ambacho kimewahi kulengwa huko nyuma katika matukio ya hujuma. Kamalvandi hakusema kilicholiharibu jengo hilo, ijapokuwa gavana wa Natanz, Ramazanali Ferdowsi amesema moto ulizuka katika eneo hilo.

Matukio ya kisiasa

Matukio ya Afrika

Masuala ya jamii

Michezo

Habari kwa lugha ya Kiingereza

Matangazo
Tazama vidio 01:07