1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo
Matangazo
Matangazo
default

Taarifa ya Habari za Ulimwengu kutoka Idhaa ya Kiswahili ya DW

Habari | 28.02.2021 | 10:00

Watu watano wameuwawa katika makabiliano ya polisi Myanmar

Duru kutoka kwa mwanasiasa na daktari mmoja nchini Myanmar zinasema polisi wamewafyatulia risasi waandamanaji wanaopinga utawala wa kijeshi na kuwauwa watu wanne huku wengine wakijeruhiwa katika siku ya pili ya kamata kamata dhidi ya waandamanaji. Mwanamke mmoja pia ameripotiwa kuuwawa wakati polisi walipojaribu kuvunja maandamano ya walimu kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi mjini Yangon. Sababu hasa ya kifo chake bado haijajulikana. Mnyamnar imekuwa katika machafuko tangu jeshi lilipochukua madaraka na kumkamata kiongozi wa taifa hilo Aung San Suu Kyi na wanachama wengine wa chama chake cha NLD mnamo Februari mosi, kwa madai ya udanganyifu katika uchaguzi wa Novemba uliokipa ushindi chama hicho. Hatua ya jeshi kuchukua madaraka imezua maandamano makubwa Myanmar ya kudai utawala wa kiraia huku mataifa ya Magharibi yakikosoa hatua hiyo.

Wanaharakati 47 wakamatwa kwa makosa ya kufanya uasi Hong Kong

Polisi mjini Hong Kong imewakamata wanaharakati 47 wa kutetea demokrasia kwa makosa ya njama ya kufanya uasi ikitumia sheria iliyo na utata ya usalama wa kitaifa iliyopitishwa mwaka uliopita. Wanaharakati hao wakiwemo wabunge wa zamani waliwahi kukamatwa mwezi Januari lakini baadae wakaachiliwa huru. Kulingana na taarifa ya polisi watu hao walikamatwa tena hivi karibuni na watafikishwa mahakamani Jumatatu. Wanadaiwa kukiuka sheria mpya ya usalama wa kitaifa iliyowekwa na China kwa kuhudhuria uchaguzi wa bunge ambao haukuwa rasmi katika eneo hilo lililo na utawala wa ndani. Kwa mujibu wa polisi mjini Hong Kong, washtakiwa hao wanajumuisha wanaume 39 na wanawake wanane walio kati ya umri wa miaka 23 na 64

Biden kutoa tamko kuhusu Saudi Arabia siku ya Jumatatu

Rais wa Marekani Joe Biden amesema serikali yake itatoa tamko juu ya Saudi Arabia kesho Jumatatu kufuatia ripoti ya kijasusi ya Marekani kusema kuwa mrithi wa kiti cha ufalme wa taifa hilo Mohammed Bin Salman aliamuru mauaji ya muandishi habari Jamal Khashoggi. Utawala wa Biden umekosolewa hasa katika ripoti ya gazeti la Washington Post iliyosema Biden angeonesha nguvu zake kwa Mohammed Bin Salman ambaye hakuwekewa vikwazo vya aina yoyote licha ya kutajwa kuhusika na mauaji ya Khashoggi. Biden amesema atatangaza Jumatatu hatua watakayochukua kwa Saudi Arabia. Jamal Khashoggi aliyekuwa uhamishoni Marekani akiandika ripoti zinazomkosoa Mohammed Salman na serikali ya Saudi Arabia, aliuwawa tarehe 2 mwezi Oktoba mwaka 2018, katika ubalozi wa Saudi Arabia mjini Istanbul, Uturuki.

Kundi la Taliban lataka vikosi vya kimataifa kuondoka Afghanistan

Kundi la Taliban leo Jumapili, limetoa wito wa kuondolewa vikosi vyote vya kimataifa nchini Afghanistan ndani ya muda uliokubalika katika makubaliano ya Doha. Kundi hilo limetoa taarifa hiyo wakati wa kuadhimisha mwaka mmoja tangu liliposaini makubaliano ya amani na Marekani nchini Qatar mnamo Februari 29 mwaka jana. Kundi la Taliban pia limetaka wafungwa zaidi waachiliwe huru na majina yao kuondolewa katika orodha ya watu hatari. Kufuatia Makubaliano ya Doha, Kundi hilo liliacha kufanya mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa Marekani wanaoongozwa na Jumuiya ya NATO nchini Afghanistan lakini likaendeleza mashambulizi yake dhidi ya serikali ya Afghan inayotambuliwa kimataifa. Mazungumzo kati ya kundi la Taliban na serikali ya Afghanistan hadi sasa hayajafanikiwa huku pande zote mbili zikishutumiana kukiuka makubaliano ya Doha. Hata hivyo washirika

Watu watano akiwemo mtoto wameuwawa katika mashambulizi ya mabomu Yemen

Afisa mmoja wa kijeshi nchini Yemen ameliambia shirika la habari la AFP kwamba watu watano akiwemo mtoto mdogo wameuwawa leo Jumapili wakati nyumba yao iliporipuliwa karibu na bandari ya Bahari ya Sham mjini Hodeida, katika mapigano ya hivi karibuni ya wenyewe kwa wenyewe nchini humo. Hata hivyo serikali ya nchi hiyo inayoungwa mkono na Saudi Arabia na waasi wa Houthi ndio wanaolaumiwa kwa shambulio hilo. Lakini waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran wamesema mripuko huo ulisababishwa na mashambulio mawili ya angani kutoka kwa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia. Hodeida, eneo lililo Kusini Magharibi mwa mji uliotekwa na waasi wa Sanaa ni njia muhimu ya kupitisha chakula, mafuta na misaada ya kibinaadamu. Mwezi Uliopita Umoja wa Mataifa ulionya maelfu ya raia wa Yemen wako katika hatari baada ya mapigano kuongezeka mjini Hodeida.

Marekani yaidhinisha chanjo ya Johnson & Johnson kupambana na COVID 19

Marekani imeidhinisha chanjo ya kampuni ya Jonhson & Johnson kwa matumizi ya dharura, hii ikiwa ni chanjo ya tatu kutolewa kukabiliana na janga la virusi vya corona. Mpaka sasa zaidi ya wamarekani laki tatu wamekufa kutokana na ugonjwa wa COVID 19. Idara ya chakula na madawa nchini Marekani FDA, imesema chanjo hiyo inayotolewa kwa dozi moja ina ufanisi mkubwa kuzuia Covid-19 pamoja na aina mpya ya kirusi cha corona. Rais wa Marekani Joe Biden ameipongeza chanjo hiyo na kuitaja kuwa maendeleo makubwa katika juhudi za taifa hilo kuvidhibiti virusi vya corona. Chanjo hiyo ni ya tatu kuidhinishwa kutumika nchini Marekani baada ya chanjo za Pfizer na Moderna zilizoidhinishwa mwezi Desemba.

Maambukizi mengine mapya zaidi ya elfu 11 yaripotiwa Urusi

Urusi imeripoti maambukizi mapya zaidi ya elfu 11,000 ya virusi vya corona huku idadi jumla ya maambukizi ikipanda na kufikia zaidi ya milioni 4. Taasisi ya udhibiti wa virusi hivyo nchini humo imesema vifo zaidi ya 379 vimethibitishwa ndani ya saa 24 zilizopita na kusababisha idadi jumla ya waliofariki kutokana na ugonjwa wa COVID 19 kufikia zaidi ya watu elfu 86. Kwa upande mwengine Israel kupitia wizara yake ya afya imesema nusu ya idadi ya watu nchini humo wameshapata dozi ya kwanza ya Pfizer-BioNTech kupambana na virusi vya corona.

Sikiliza sauti 09:48