Homa ya nguruwe yaenea Ulaya | Masuala ya Jamii | DW | 24.07.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Homa ya nguruwe yaenea Ulaya

Uingereza, Ujerumani na Uhispania zaathirika zaidi

default

Madaktari wakiwa wamejihami dhidi ya virusi vya H1N1

Takwimu za Idara ya kupambana na magonjwa ya mripuko barani Ulaya zinaonyesha kuwa jumla ya watu 11,159 nchini Uingereza tayari wameambukizwa virusi vinavyosababisha homa ya nguruwe, wengine 2455 wameambukizwa Ujerumani, na 1526 wameambukizwa Uhispania. Mamlaka hiyo ina wajibu wa kukusanya takwimu za wagonjwa walioambukizwa ugonjwa huo katika mataifa ya Ulaya.

Idadi ya maambukizi mapya inaripotiwa kuongezeka tangu mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu. Kwa sasa kiasi cha visa 3500 hadi 4 vya maambukizi mapya kimeripotiwa katika mataifa ya Norway,Uswisi na Iceland. Jumla ya watu 17,733 wameambukizwa virusi hivyo barani Ulaya. Mpaka sasa watu 35 wamefariki baada ya kuambukizwa ugonjwa huo, 30 kati yao raia wa Uingereza, na waliosalia wa Uhispania.

Idara ya kupambana na usambaaji wa magonjwa iliyonakili kisa cha kwanza ina azma ya kupunguza idadi ya watu wanaoambukizwa.Wiki iliyopita mtu mmoja alifariki mjini Budapest, Hungary, baada ya kupata maambukizi kwenye mapafu.Tathmini ya upasuaji ilibaini kuwa mtu huyo alikuwa ameambukizwa virusi vya H1N1.

Hata hivyo, kamisheni ya Umoja wa Ulaya ilikuwa imeonya kuhusu uwezekano wa kusambaa kwa homa ya nguruwe barani Ulaya.Akiwa mjini Brussels, Ubelgiji, kamishna anayehusika na masuala ya Afya katika Umoja wa Ulaya, Androulla Vassiliou, alisema kuwa idadi ya vifo barani Ulaya bado iko chini, ila baada ya muda wataalam wa afya walitangaza takwimu mpya baada ya ongezeko la vifo vya watu nchini Ujerumani.

Kulingana na Kamishna Vassiliou virusi vinavyosababisha homa ya nguruwe huenda vikaongezeka katika kipindi hiki cha mapumziko wakati ambapo safari nyingi hutokea. Hali hiyo inalazimu kuwa na usimamizi mwafaka wa mfumo maalum wa chanjo katika mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya kama njia moja ya kujikinga. Umoja Ulaya unaweza tu kusimamia suala lenyewe ila utekezaji utahitaji mchango wa nchi wanachama.

Kwa sasa Uingereza ndiyo iliyoathirika zaidi na maambukizi ya homa ya nguruwe. Cherie Blair, mkewe waziri mkuu wa zamani wa Uingereza, naye anaaminika kuwa ameambukizwa ugonjwa huo. Hata hivyo, mengi ya mataifa yameathirika kwa kiasi kidogo tu. Kulingana na mtaalam wa masuala ya kiuchumi katika Chuo cha Imperial kilichoko mjini London, Uingereza, idadi ya waliofariki baada ya kuambukizwa homa hiyo haitofautiani sana na ile ya wanaoambukizwa mafua kila katika msimu wa baridi kali.

Nchini Ufaransa, kundi la wanafunzi 47 raia wa Uhispania na Uingereza ambao wanaripotiwa kuwa watoto wa matajiri, wamezuliwa na kuwekwa katika karantini.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Henri Welschinger aliyefanikiwa kukutana na wagonjwa hao katika Chuo kikuu, hakuna haja ya kuingiwa na wasiwasi. Kwa upande wake, Shirika la habari la AFP lilitangaza kuwa wanafunzi hao hawakuwa wameambukizwa virusi hivyo ila walikuwa na homa tu ya kawaida. Kufuatia hilo, hospitali moja iliyoko Lübeck walikozaliwa vijana hao ilifungwa kama njia moja ya kuzuia maambukizi.

Hapa Ujerumani, ambako idadi ya walioambukizwa virusi vya homa hiyo inaripotiwa kuongezeka kwa kiasi kikubwa, kunatakiwa kuwa na mpango madhubuti wa kuwaandaa madaktari,wauguzi,maafisa wa polisi pamoja na wataalam wengine wanaohusika kwa karibu na tatizo hilo.Baraza la Mawaziri, kwa upande wake, linapaswa kuafikiana kuhusu njia mwafaka za kupambana na janga hilo.

Italia, kwa upande wake, inajiandaa kwa kuagiza dosi milioni 48 za chanjo dhidi ya virusi hivyo.Waziri wa Afya wa Italia, Maurizio Sacconi, alisema kuwa wafanyakazi katika sekta ya afya pamoja na maafisa wa polisi, idara ya wazima moto na raia walio na umri wa zaidi ya miaka 65 watachanjwa wakati awamu ya kwanza ya chanjo hiyo itakapoanza ifikapo mwezi Novemba.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com