1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hisa za Bayer zaporomoka

13 Agosti 2018

Hisa za kampuni kubwa ya kilimo na madawa ya Bayer ya Ujerumani imeshuka kwa zaidi ya asilimia 10 baada ya mahakama ya California kuiagiza kampuni mpya ya Marekani inayozalisha mbegu ya Monsanto kulipa dola milioni 289.

https://p.dw.com/p/335XL
Bayer AG Logo
Picha: picture-alliance/Geisler/C. Hardt

Hisa za kampuni kubwa ya kilimo na madawa ya Bayer nchini Ujerumani imeshuka kwa zaidi ya asilimia 10 leo baada ya mahakama ya California nchini Marekani kuiagiza kampuni mpya ya Marekani inayozalisha mbegu ya Monsanto ambayo sasa ni tawi la Bayer  kulipa dola milioni 289  kutokana na kushindwa kutoa onyo kuhusu hatari ya maradhi ya saratani yanayoweza kusababishwa na dawa ya kuua magugu inayotengenezwa na kampuni hiyo. 

Mahakama iliamuru mfanyakazi wa shughuli za usafi katika shule ya Benicia, California Dewayne Johnson kulipwa karibu dola milioni 290, ikisema Monsanto ilitakiwa kuwaonya wanunuzi kwamba dawa ya Roundup inayoua magugu inaweza kusababisha saratani. Mfanyakazi huyo Johnson alikutikana na maradhi hayo ya saratani mnamo mwaka 2014. 

Kesi dhidi ya Monsanto iliyonunuliwa na kampuni ya Bayer mwaka huu kwa dola bilioni 63, ni ya kwanza miongoni mwa kesi zaidi ya 5,000 kama hizo dhidi ya dawa za kuua magugu zinazozalishwa na kiwanda hicho, ambazo ni pamoja na chapa ya Roundup, kote nchini Marekani. 

Wakati waangalizi wakitabiri kwamba maelfu ya kesi kama hizo yanaweza kufuatia, Bayer imesema matokeo ya hukumu hiyo yanakinzana na vithibitisho vya kisayansi na kwa maana hiyo mahakama nyingine huenda zikatoa hukumu tofauti.

USA, , San Francisco: Dewayne Johnson
Dewayne Johnson aliyeathirika na dawa hiyyo ya Roundup na kutakiwa kulipwa takriban dola milioni 290.Picha: picture-alliance/dpa/J. Edelson

Kesi ya Johnson iliwasilishwa tangu mwaka 2016.

Monsanto ilisema siku ya Ijumaa kwamba itakata rufaa dhidi ya hukumu hiyo ambayo ni tukio la mwishoni kabisa baada ya mjadala wa muda mrefu dhidi ya madai kwamba athari za Roundup zinaweza kusababisha saratani.

Kampuni ya Bayer imesema kupitia taarifa yake iliyoangazia aina ya saratani aliyonayo mlalamikaji kwamba hukumu hiyo inatofautiana na vithibitisho vya kisayansi, uzoefu wa muda mrefu na hitimisho kutoka kwa wadhibiti wa kimataifa wa dawa unaothibitisha kwamba kemikali ya glyphosate ni salama na haisababishi saratani hiyo ya lymphoma.

Kesi ya mfanyakazi wa usafi Dewayne Johnson iliyowasilishwa mwaka 2016, ilieendeshwa kwa haraka kutokana na ukali wa saratani ya mlalamikaji ambayo huathiri mfumo wa lymph unaosafirisha majimaji mwilini inayodaiwa kusabishwa na dawa za Roundup na Ranger Pro, ambayo ni aina nyingine ya dawa ya kuua magugu inayozalishwa na Monsanto yenye kemikali ya glyphosate.

Frankreich Protest gegen Monsanto
Kampuni ya Monsanto imenunuliwa na Bayer, na imepita miezi miwili tu tangu kukamilisha manunuzi yake.Picha: picture-alliance/AP Photo/F. Mori

Hisa za Bayer zilishuka kwa asilimia 11, ambacho ni kiwango cha chini zaidi kwenye soko la hisa, na kulingana na wachambuzi mvutano huo pia unaweza kuathiri mapato ya huko mbeleni.  

Bayer bado inakabiliwa na mlolongo wa kesi zitokanazo na athari za dawa inazozalisha.

kesi Wawekezaji wa Ujerumani wameondoa hisa zao kwenye kampuni ya Bayer, wakihofia hukumu hiyo inayoweza kusababisha athari kubwa dhidi ya kampuni ya Monsanto.

Hukumu hiyo imekuja ikiwa ni miezi miwili baada ya ya Bayer kuhitimisha makubaliano ya kununua kampuni ya Monsanto, na Bayer inapanga kuachana na jina hilo la Monsanto mara baada ya ununuzi kukamilika.

Kesi yake iliyotokana na uchunguzi wa mwaka 2015, uliofanywa na shirika la kimataifa la utafiti wa saratani, ambalo ni sehemu ya shirika la Umoja wa Mataifa la afya, WHO, lililokitaja kiungo muhimu kwenye dawa hiyo ya Roundup cha glyphosate kuwa kinaweza kusababisha saratani.

Aidha, kampuni ya Bayer hivi sasa inakabiliwa na maelfu ya kesi kutoka kwa wagonjwa wanaodai kuathirika baada ya kutumia vifaa inavyotengeneza kwa ajili ya uzazi wa mpango vya Essure na Mirena.

Lakini pia, wazalishaji wa asali nchini Canada wameibua madai wakitaka kulipwa fidia dhidi ya dawa ya kuua wadudu inayozalishwa na kiwanda hicho ya neonicotinoid, ambayo wanaharakati wanadai kwamba imesababisha nyuki wengi kufa.

Bayer imesema, katika ripoti yake ya robo ya kwanza ya mwaka kwamba imetenga dola takribani bilioni 277 kwa ajili ya madai ambayo bado yanasubiri kushughulikiwa.

Mwandishi: Lilian Mtono/RTRE/AFPE

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman