1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hayati Magufuli aagwa nyumbani kwake Chato

Dotto Bulendu25 Machi 2021

Mwili wa Marehemu John Magufuli umeagwa nyumbani kwake katika uwanja uliopewa jina lake, ikiwa ni siku ya mwisho kwa Watanzania kutoa heshima zao za mwisho kabla ya hapo kesho kulazwa rasmi katika nyumba yake ya milele.

https://p.dw.com/p/3r6lT
Tansania Abschiedszeremonie Präsidenten John Magufuli im Bezirk Chato
Picha: Eric Boniface/DW

Mwili wa aliyekuwa rais wa taifa hilo la Afrika Mashariki, Marehemu John Magufuli, unaagwa nyumbani kwake katika Uwanja uliopewa jina lake, ikiwa ni siku ya mwisho kwa Watanzania kutoa heshima zao za mwisho kwake kabla ya hapo kesho Ijumaa kulazwa rasmi katika nyumba yake ya milele. 

Asubuhi ilianza kwa ukimya hapa Chato ulipolala mwili wa Marehemu John Magufuli huku wakazi wa wilaya hii na maeneo ya jirani baadhi wakilala katika uwanja wa Magufuli kusuburi kutoa hehima zao za mwisho.

Viongozi mbalimbali serikali watoa heshima zao za mwisho

Tansania Abschiedszeremonie Präsidenten John Magufuli im Bezirk Chato
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa hayati John Magufuli wakati wa hafla ya kuuaga inayofanyika wilayani Chato mkoani Geita nchini TanzaniaPicha: Eric Boniface/DW

Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Hemed Suleiman Abdallah ndiye anayeowaongoza waombolezaji hii leo huku akiwa na ujumbe maalum kwa Watanzania.

"Tuendelee kushikamana sana katika kulijenga taifa letu. Tayari mpendwa wetu dokta John Pombe Magufuli ametuonyesha njia. Ameliwacha taifa hili likiwa salama na heshima kubwa sana. Tuliona alitutoa kwenye uchumi wa chini na kutuweka kwenye uchumi wa kati kabla ya muda ambao umetabiriwa na wataalamu."

Mwili wa Marehemu John Magufuli ulioingia katika viwanja hivi vya Magufuli mishale ya saa nne asubuhi na kupokewa na ukimya mkubwa wa waombolezaji, ulisomewa dua na viongozi wa dini huku wananchi wakitoa hisia zao juu ya msiba huu mkubwa uliolipata taifa la Tanzania.

Katika kuhakikisha wana Chato wanapata muda wa kumuaga kiongozi wao aliyewahudumia kwa miaka 26 kwanza kwa nafasi ya ubunge na kisha urais, Serikali imewahakikishia waombolezaji wote kupata nafasi ya kumuaga Rais Magufuli.

Leo ndiyo siku maalum kwa waombolezaji kumuaga Marehemu John Magufuli Rais wa awamu ya tano wa Tanzania kabla ya kuagwa kupumzishwa katika nyumba yake ya milele hiyo mnamo siku ya Ijumaa Chato yalipo makazi yake na wazazi wake.