Hatimaye dos Santos ang′oka rasmi siasa za Angola | Matukio ya Afrika | DW | 09.09.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

ANGOLA

Hatimaye dos Santos ang'oka rasmi siasa za Angola

Rais Joao Lourenco wa Angola amechaguliwa rasmi kuwa kiongozi wa chama tawala, MPLA, akichukuwa mikoba ya rais wa zamani, Jose Eduardo dos Santos aliyekuwa akizitawala siasa za nchi hiyo kwa takribani miongo minne.

Akiwa amehudumu kwenye nafasi ya urais tangu Agosti 2017, Lourenco alipata asilimia 98.59 ya kura za wajumbe 2,951 wa chama hicho tawala siku ya Jumamosi (Septemba 8), na hivyo kukamilishiwa hatua za kumilikishwa mamlaka ya juu kabisa kwenye taasisi zote muhimu za nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.

"Kwa nguvu za jana na za leo tunajenga kesho yetu, tunaweza kusahihisha kilichokosewa," Lourenco aliwaambia wajumbe wa mkutano mkuu wa sita usiokuwa wa kawaida wa MPLA.

Tangu aingie madarakani, Lourenco amekuwa akionesha kutafautiana kisera na kimkakati na mtangulizi wake, dos Santos, huku akielezea bayana kuwa anataka kuzizika kabisa siasa za zamani.

"Ndugu zangu, sote tunajuwa kuwa tutaweza tu kuujenga mustakabali mwema kama tunao uthubutu wa kweli wa kurekebisha kisicho sahihi - ufisadi na udugunaizesheni, uzembe na kukiuka sheria - mambo ambayo yamekuwa yakitokea katika miaka ya hivi karibuni," alisema Lourenco.

Hatimaye dos Santos ang'atuka rasmi

Angola Luanda Parteitag MPLA (DW/António Cascais)

Wajumbe wa chama tawala cha Angola, MPLA, kwenye mkutano mkuu wa tarehe 8 Septemba 2018 mjini Luanda.

Hata hivyo, dos Santos aliwaaga wajumbe wa mkutano huo mkuu wa MPLA kwa kuwaambia kuwa hajutii alichokifanya kwenye utawala wake. "Leo naondoka nikiwa kifua mbele na nakabidhisha kijiti kwa Komredi Joao Lourenco," alisema dos Santos kwenye makao makuu ya chama tawala mjini Luanda. 

Mpiganaji huo wa ukombozi mwenye umri wa miaka 76 hakuwania tena urais kwenye uchaguzi wa Agosti 2017 na alimkabidhi madaraka waziri wake wa ulinzi, Lourenco, mwenye umri wa miaka 64. Hata hivyo, aliendelea kushikilia nafasi ya juu kabisa kwenye chama, ambako ndiko hasa nguvu za utawala wa nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta ziliko.

Lakini siku ya Jumamosi, "Komredi Nambari Moja" - kama alivyokuwa akiitwa - hatimaye aliwachia udhibiti wa MPLA kwa Lourenco, huku akikiri baadhi ya makosa wakati wa utawala wake. "Hakuna binaadamu asiye makosa, nami nakisia kuwa nilifanya makosa pia," alisema dos Santos.

Mzozo wa dos Santos na Lourenco

Berlin Joao Lourenco Präsident Angola (DW/Cristiane Vieira Teixeira)

Rais wa Angola na mwenyekiti mpya wa chama tawala cha MPLA, Joao Lourenco

Wachambuzi wanasema kuondoka kwa mkongwe huyo wa siasa za Angola kwenye ulingo rasmi wa siasa ni dalili nzuri baada ya vita vikubwa vya maneno kati yake na Lourenco, ambaye alikuwa akimdhania kuwa angelimlinda baada ya kuondoka madarakani.

Kabla ya kuachia madaraka mwaka jana, dos Santos alihakikisha kuwa anavigawa vyombo vyote vyenye nguvu kwa uchumi na siasa za nchi yake kwa watu wake wa karibu, kama vile alivyomkabidhisha shirika la mafuta bintiye, Isabel, anayetajwa kuwa mmoja wa wanawake matajiri kabisa barani Afrika. Aliwateuwa pia maafisa watiifu kwake kuongoza vyombo vya usalama.

Hata hivyo, mara tu baada ya kushika madaraka, Lourenco alitumia mamlaka yake kuipanguwa safu ya mtangulizi wake serikalini, ikiwemo kumuondoa Isabel kutoka ukuu wa shirika la mafuta la Sonangol, na pia kaka yake, Jose "Zenu" Filomeno, kutoka uongozi wa mfuko wa fedha wa Angola.

Filomeno anakabiliwa sasa na mashitaka ya kutumia vibaya fedha za umma, huku Isabel akichunguzwa kwa tuhuma kadhaa za ufisadi. Wengi wa wandani wa dos Santos wamejikuta wakiondoshwa kwenye nafasi zao, wakiwemo wakuu wa jeshi, polisi na wa mashirika ya umma.

Rais huyo mpya anakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa ajira, ukuwaji mdogo wa uchumi na nakisi kubwa ya bajeti licha ya Angola kuwa taifa la pili kwa uzalishaji mafuta ghafi barani Afrika.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Isaac Gamba