Hatimae uchaguzi wafanyika Guinea-Bissau | Matukio ya Afrika | DW | 13.04.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Hatimae uchaguzi wafanyika Guinea-Bissau

Hakuna uchaguzi barani Afrika uliokuwa ukisitishwa na kuahirishwa mara kwa mara katika miaka ya hivi karibuni kama ule wa Guinea-Bissau.Hatimae unafanyika Jumapili (13.04.2014) kumchaguwa rais na bunge.

Picha za wagombea wa uchaguzi nchini Guinea-Bissau.

Picha za wagombea wa uchaguzi nchini Guinea-Bissau.

Tokea mapinduzi ya mwaka 2012 nchi hiyo imekuwa ikisubiri kupata serikali itakayochaguliwa kihalali. Katika uchaguzi huo mkuu wananchi wa Guinea-Bissau wanatarajiwa kupiga kura ya kumchaguwa rais na bunge kwa matarajio ya kurudisha demokrasia nchini humo.

Jose Mario Vaz,Paulo Gomes, Nuno Nabian na Abel Incada hawa ni wagombea wanne wanaowekewa matumaini makubwa katika uchaguzi huo wa Guinea -Bissau nchi ilioko Afrika Magharibi.Majina manne ambayo yumkini yakawa yamejulikana hivi karibuni tu na watu walioelimika nchini humo. Rais wa mpito wa hivi sasa Manuel Serifo Nhamadjo hatogombania urais kwenye uchaguzi huo.Kwa mara ya kwanza tokea kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi hapo mwaka 1991 hakuna kigogo kimoja tu kikuu cha kisiasa katika uchaguzi huo wa rais kwenye nchi hiyo yenye idadi ya watu milioni 1.7.

Waziri Mkuu wa zamani wa Guinea -Bissau Carlos Gomes Junior akiwa uhamishoni Lisbon Ureno.

Waziri Mkuu wa zamani wa Guinea -Bissau Carlos Gomes Junior akiwa uhamishoni Lisbon Ureno.

Kukosekana kwa Carlos Gomes Junior waziri mkuu wa zamani katika uchaguzi huo kunajitokeza wazi ambapo serikali yake ilipinduliwa na jeshi hapo mwaka 2012 wakati huo alikuwa ndio kwanza alikuwa ameshinda duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais na alikuwa akiwekewa matumaini ya kushinda duru ya pili ambayo haikuandaliwa tena kutokana na mapinduzi hayo.

Tokea wakati huo serikali ya mpito ndio iliokuwa madarakani nchini Guinea- Bissau.Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya Mataifa ya Magharibi ECOWAS iliweka hali ya utulivu nchini humo.Lakini Mkuu wa Majeshi Antonio Indaji aliendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika serikali ya mpito ya nchi hiyo. Kwa hiyo Carlos Gomes Junior waziri mkuu wa zamani hakuthubutu kurudi nchini humo na amekuwa akifuatilia uchaguzi huo kutoka uhamishoni anakoishi nchini Ureno na Cape Verde.

Wagombea wakuu

Kukosekana kwa majina mashuhuri kumepelekea kugawika kwa chama kilichopigania uhuru hapo zamani ambacho ni chama kikubwa kabisa nchini humo PAIGC katika kambi kuu mbili za kisiasa ambapo kuna wagombea wawili wanaowania urais katika chama hicho kikongwe. Mgombea rasmi wa chama hicho ni Jose Mario Vaz ambaye alikuwa waziri wa fedha hadi hapo mwaka 2012 wakati serikali ilipopinduliwa.

Mgombea urais wa chama cha PAIGC Jose Mario Vaz.

Mgombea urais wa chama cha PAIGC Jose Mario Vaz.

Vaz anasema watashinda uchaguzi wa bunge na rais na kwamba kwa faida ya wananchi kipau mbele kikubwa ni kuimarisha uchumi,kujenga nafasi za ajira na kuinuwa uchumi ili kuufanya uendelee kukua.

Vaz anategemea karata zake kutokana na uwiano mzuri uliokuweko wakati wa serikali iliyopinduliwa hapo mwaka 2012 ambapo uchumi wake ulipanda juu na mishahara ya serikali ilikuwa ikilipwa kwa kawaida. Hata hivyo tokea kutokea kwa mapinduzi hayo uchumi wa nchi hiyo umekuwa ukishuka.

Jose Mario Vaz aliwahi kushutumiwa kwa ubadhirifu wa msaada wa fedha lakini amesema shutuma hizo zimechochewa kisiasa lakini hakuwahi kufikishwa mahakamani.

Paulo Gomes mgombea huru katika uchaguzi wa rais Guinea-Bissau.

Paulo Gomes mgombea huru katika uchaguzi wa rais Guinea-Bissau.

Pia katika fani hiyo ya kiuchumi kuna mgombea Paulo Gomes ambaye ni mwanachama wa chama cha PAIGC ambaye anagombea kama mgombea huru.Anasema yeye ni mtaalamu na sio mwanasiasa kwa vitendo lakini ana fursa kubwa ya kuutambuwa uchumi wa nchi yake kutokana na tajiriba yake kubwa ya kimataifa.Amepata elimu yake katika Chuo Kikuu chenye hadhi cha Havard nchini Marekani na amewahi kufanya kazi na Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika.

Kambi nyengine za kisiasa

Rais wa zamani wa Guinea-Bissau marehemu Kumba Iala (kushoto) na Nuno Gomes Nabiam wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais.

Rais wa zamani wa Guinea-Bissau marehemu Kumba Iala (kushoto) na Nuno Gomes Nabiam wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais.

Kwa upande wa kambi nyengine za kisiasa za jadi nchini humo chama cha Social Renewal (PRS) kina wagombea wanne lakini mgombea rasmi ni Abel Incada lakini wengi wanamuwekea matumaini Nuno Nabiam mgombea huru aliyesaidiwa wakati wa kampeni na rais wa zamani marehemu Kumba Iala na ziada ya hilo anatajwa kuwa ni mgombea anayehusiana na Mkuu wa Majeshi ya nchi hiyo Antonio Indajai.Karibu sehemu kubwa ya wanajeshi wa nchi hiyo wanatoka kwenye kabila la Balanta ambao hufanya theluthi moja ya wananchi wa nchi hiyo na hapo kijadi ndio ulipo msingi wa uchaguzi wa chama cha

(PRS).Alipoulizwa na DW juu ya haja ya kufanywa kwa mageuzi ya kijeshi nchini humo Nabiam amesema anaamini kwamba mageuzi kwenye fani ya usalama yanahitajika hasa lakini inapaswa yazingatiwe kwa uangalifu wakati mageuzi hayo yanapopaswa kutekelezwa na suala hilo linahitaji kujadiliwa.

Hadi sasa kampeni za uchaguzi wa rais nchini humo zimefanyika kwa utulivu na amani. Waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Afrika,Timor ya Mashariki na New Zealend wanatazamiwa kuyakinisha uchaguzi huo unafanyika kwa njia ya haki.Kutokana na uwakilishi wa uwiano iwapo hakuna mgombea kati ya wagombea 13 atakayepata ushindi mkubwa wa kura itabidi wagombea wawili waliojizolea kura nyingi waingie duru ya pili ya uchaguzi.

Guinea-Bissau kisanduku cha baruti

Mkuu wa majeshi nchini Guinea -Bissau Antonio Indjai.

Mkuu wa majeshi nchini Guinea -Bissau Antonio Indjai.

Lakini licha ya kwamba hivi sasa hali ni shwari nchini humo Guinea-Bissau ni sanduku la baruti ambalo linaweza kuripuka wakati wowote ule kama ilivyojionyesha hivi karibuni kutokana na mapinduzi kadhaa na mauaji ya kisiasa nchini humo Jeshi la nchi hiyo limekuwa halitaki kujiweka chini ya udhibiti wa serikali na hadi sasa limekuwa likikaidi jaribio lolote lile la kulifanyia mageuzi.Mwezi wa Aprili mwaka 2012 lilifanya mapinduzi dhidi ya waziri mkuu wa zamani Paulo Gomes Junior ambaye kwa msaada wa Angola alikuwa amepanga kulifanyia mageuzi jeshi hilo.

Mtalamu wa taaluma ya siasa wa Ureno Elisabete Azevedo - Harman anasema nchi hiyo inahitaji mageuzi kadhaa miongoni mwao ni yale ya kijeshi Lakini pia inahitaji kuunda nafasi za ajira kutokana na kwamba uchumi wa nchi hiyo umezorota kabisa jambo ambalo linaifanya kuwa rahisi kuathirika na makundi ya kihalifu yenye kufanya biashara ya madawa ya kulevya.Guinea- Bissau kinahesabiwa kuwa kituo cha kupitishia madawa ya kulevya yanayosafirishwa kutoka Amerika Kusini kwenda Ulaya na watu wanaojishughulisha na biashara hiyo haramu.

Kazi pevu inamkabili rais mpya wa nchi hiyo na changamoto kuu ni : kuhakikisha kukamilika kwa muhula wa rais kuwa madarakani katika kipindi cha miaka minne.Tokea nchi hiyo ijipatie uhuru wake kutoka Ureno hapo mwaka 1974 hakuna rais yoyote kati ya marais kumi aliyeweza kukamilisha kipindi chote cha miaka minne madarakani nchini Guinea-Bissau.Marais watatu walipinduliwa katika mapinduzi na mmoja Joao Bernado Vieira aliuwawa hapo mwaka 2009.

Mwandishi : Johannes Beck/Mohamed Dahman

Mhariri: Bruce Amani