Hamsini nimetimia | Miaka 50 ya DW Kiswahili | DW | 30.01.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Miaka 50 ya DW Kiswahili

Hamsini nimetimia

Deutsche Welle Kiswahili, khamsini ‘shatimia Tangu nilipokubali, habari kuwaletea Kwa lugha hii asali, Kiswahili kiso dowa Na leo nasherehekea.

Karte mit Korrespondenten für 50 Jahre special page Kisuaheli Redaktion

Deutsche Welle Kisuaheli Redaktion Karte von Korrespondenten

Nilianza myaka mingi, dunia kutangazia
Nikaelimisha wengi, Ulaya hadi Asia
Afrika ‘kawa kambi, Arabuni hahamia
Kote nikahishimiwa

Siku zote nihewani, habari kusimulia
Zimo za utamaduni, siasa uchumi pia
Na michezo viwanjani, zote nazifatilia
Kwa kina nazizamia

Vipindi vino tajika, adhimu kuvisikia
’Pambazuko Afrika, Muangaza wa Ulaya
Noa bongo elimika, tamaduni na sanaa
Kwa wiki vyajirudia

Mitazamo mbalimbali, kwa kina yachambuliwa
Ya serikali katili, na za kidemokrasia
Ya kwondowa ubatili, na haki kusimamia
Bila ya kupendelea

Na suala la mazingira, nimo nalichanjagia
Afrika kudorora, siwezi kuiachia
Nawatafuta vinara, wakaja kulichambua
Debe tukalipigia

Habari zilo muhimu, nazeneza zikanea
Uenezi wa elimu, washamiri na kumea
Idhaa hii adhimu, wengi waitegemea
Idhaa ilo muruwa

Chemchemu ya habari, wengi nawasambazia
Si kwamba najifakhari, nasema bila ya ria
Watangazaji mahiri, ninao walobobea
Fani ilowakolea

Napokea wanafunzi, Bonn kuja jisomea
Nawita wenye ujuzi, na wanaochipukia
Wakaja kustaladhi, raha ya kutangazia
Shahada nawapatia

Sikiza uelimike, redio ya manufaa
Shikilia usichoke, dira yako ya dunia
Soma na kurasa zake, Facebook tembelea
Deutsche Welle aminia

Wataka Kijerumani, njoo 'takupatia
Sogea mtandaoni, usome bila fidia
Na kama una maoni, lete nitayapokea
Ujumbe niandikia

Maoni yako muhimu, kwa mimi kuendelea
Siitakidi ni sumu, ya kuweza kuniua
Bali ni nguvu ya hamu, ya mbele kukimbilia
Usichoke n'andikia

Mkono wangu mrefu, kwa zawadi kuzitoa
Pale panaposadifu, shindano kuandaliwa
Na hiyo huwa sharafu, ya mimi kupendezewa
Zawadi nyingi natoa

Mafanikio siwezi, peke yangu kufikia
Lau si nyi’ wasikizi, munaofuatilia
Po nisingemaizi, haya niliyowambia
Ahsante kwa pamoya

Sherehe hii ya sasa, khamsini kutimia
Moyo yanituturusha, mbele nikifikiria
Mungu atupe maisha, ya kuishi miaka mia
Karne kusherehekea

Tanbihi: Ushairi huu umeandikwa na Hamad Hamad wa Copenhagen, Denmark ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Idhaa ya Kiswahili ya DW.

Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com