Hali ni tete kufuatia kura ya maoni Ukraine | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.05.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Hali ni tete kufuatia kura ya maoni Ukraine

Vikosi vya usalama vya Ukraine vimepambana na wanaharakati wanaotaka kujitenga baada ya kura ya maoni iliofanyika kinyume na sheria mashariki mwa nchi hiyo kuonyesha kuunga mkono kwa kauli moja kujipatia uhuru wake.

Mpiganaji wa waasi akijibanza nyuma ya mabehewa ya treni katika mstari wa mbele wa mapambano kwenye mji wa Slavyansk. (12.05.2014)

Mpiganaji wa waasi akijibanza nyuma ya mabehewa ya treni katika mstari wa mbele wa mapambano kwenye mji wa Slavyansk. (12.05.2014)

Miripuko kadhaa na sauti za risasi zilisikika karibu na eneo lenye vurugu katika mji wa Slavyansk Jumatatu (12.05.2014) wakati serikali ya Ukraine ikiwa katika harakati za kuwatimuwa waasi wanaoiunga mkono Urusi waliojichimbia katika eneo hilo.

Mapigano yalizuka katika kijiji cha karibu kwenye mstari wa mbele wa mpambano katika mji huo uliozingirwa wenye wakaazi takriban 110,000 wa kile serikali ya Ukraine inachokiita operesheni dhidi ya ugaidi.

Waasi wamekuwa wakiushambulia takriban kila siku mnara huo wa televisheni na vikosi vya serikali vimekuwa vikijibu mapigo kwa mashambulizi ya risasi.

Waziri wa mambo ya ndani wa Ukraine Arsen Avakov amesema katika mtandao wake wa Facebook kwamba wanaharakati wanaotaka kujitenga waliwashambulia askari na mnara huo wa televisheni kwa maguruneti.

Ameripoti kwamba wanaharakati hao ambao imethibitika kuwa wana silaha nzito na waliofunzwa vyema waliushambulia kwa mizinga mnara huo mara kumi na tano na kwamba kulikuwa hakuna maafa kwa upande wa jeshi na pia kulikuwa hakuna taarifa juu ya maafa yaliyotokea kwa upande wa waasi.

Urusi inaheshimu matokeo

Waziri wa Mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov.

Waziri wa Mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov.

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema leo serikali yake inaheshimu matokeo ya kura hiyo ya maoni juu ya kuwa na mamlaka ya kujitawala katika majimbo hayo mawili ya Ukraine.

Amesema matokeo rasmi yatatangazwa hivi karibuni lakini wanaheshimu maamuzi ya wapiga kura wa Donetsk na Luhansk na kwamba wanaamini utekelezaji wa vitendo wa matokeo hayo utapelekea kufanyika kwa mazungumzo kati ya serikali ya Ukraine na wawakilishi wa eneo la mashariki.

Urusi imesema inataraji utekelezaji wa vitendo wa matokeo ya kura hiyo ya maoni utafanyika kwa njia ya ustaarabu.

Imeongeza kusema kwamba Shirika la Usalama na Ushirikiano la Ulaya (OSCE) linaweza kusaidia kuandaa mazungumzo kati ya serikali ya Ukraine na wawakilishi wa eneo la mashariki baada ya takriban asilimia 90 ya wapiga kura kusema katika kura ya maoni iliopigwa hapo jana Jumapili kwamba wanaunga mkono kwa majimbo yao ya Donetsk na Lugansk kuwa na mamlaka za dola.

Hatima ya majimbo

Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi wakianza kuhesabu kura Lugansk. (11.05.2014 )

Wajumbe wa Tume ya Uchaguzi wakianza kuhesabu kura Lugansk. (11.05.2014 )

Waasi wanaoiunga mkono Urusi wamesema hatima ya majimbo hayo itajadiliwa baadae leo hii na inaweza kujumuisha uwezekano wa kujitenga,kunyakuliwa na Urusi au kuendelea kubakia kuwa sehemu ya Ukraine.

Kaimu rais wa Ukraine Oleksandr Turchynov amesema katika taarifa leo hii kwamba upuuzi huo ambao magaidi wanauita kuwa kura ya maoni hautokuwa na taathira ya kisheria isipokuwa kuwajibika kihalifu kwa waandaaji wa kura hiyo.

Serikali ya Ukraine na mataifa ya magharibi zimelaani kura hiyo ya maoni kuwa ulaghai na ukiukaji wa sheria ya kimataifa na imeishutumu Urusi kwa kuchochea machafuko katika jaribio la kunyakuwa ardhi zaidi kutoka Ukraine baada ya kulitwaa jimbo la Crimea.

Mwandishi : Mohamed Dahman /AP/AFP/dpa

Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com