1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guardiola: Muamuzi aliwapendelea Liverpool

17 Oktoba 2022

Huenda msimu wa Liverpool katika ligi hiyo ndio ukawa umeanza sasa hasa baada ya kutoa ushindi wa moja bila dhidi ya Manchester City uwanjani Anfield Mo Salah akiwa mfungaji wa bao la pekee.

https://p.dw.com/p/4IIG9
Champions League | Manchester City v Borussia Dortmund
Picha: Carl Recine/Reuters

Kocha wa Liverpool Jurgen Klopp alionyeshwa kadi nyekundu baada ya kumkaripia muamuzi wa pili wa mechi kwa kile alichosema ni Mo Salah kuchezewa rafu na Bernado Silva.

Lakini baadae Klopp mwenyewe alikiri kwamba alichokifanya ni makosa.

"Bila shaka kadi nyekundu ni makosa yangu. nilipitiliwa na hisia wakati huo ila sidhani kama nilimkosea heshima mtu yeyote yule. Ila nataka niulize, ni vipi muamuzi hakupuliza kipenga kwa jinsi Salah alivyochezewa na Silva? Ingezewezekana vipi asipulize kipenga, ningependa kupata maelezo," alisema Klopp.

Naye kocha wa Manchester City Pep Guardiola naye amemlalamikia muamuzi kwa kufutilia mbali bao la Phil Foden kunako kipindi cha kwanza.

"Kabla mechi muamuzi alizungumza na msaidizi wangu Rodolfo na Jurgen na akasema, sawa sitofanya makosa, kila kitu kitakuwa wazi. Na sehemu kubwa ya mechi ilikuwa hakuna kupuliza firimbi, hata mchezaji akichezewa vibaya anasema endelea endelea tu, hadi pale tulipofunga sisi ndio firimbi ikapulizwa. Kwa hiyo hicho ndicho kilichotokea," alisema Guardiola.

Mwanya kati ya Manchester City na Arsenal ambao wanaongoza ligi kwa sasa umefikia pointi nne baada ya hao the gunners kupata ushindi mwembamba wa moja bila walipokuwa wakicheza na Leeds United.