Gebrselassie :rekodi mpya marathon Berli n | Michezo | DW | 29.09.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Gebrselassie :rekodi mpya marathon Berli n

Bingwa mara 2 wa Olimpik avunja mara ya pili rekodi ya dunia ya mbio za marathon huko Berlin.

default

Haile Gebrselassie

RIADHA:

Haile Gebrselassie wa Ethiopia,ameweka rekodi mpya ya dunia katika mbio za marathon mjini Berlin,Ujerumani jana ikiwa kwa mwaka wapili mfululizo.

Jurgen Klinsmann kocha wa Bayern Munich atiwa shindo kwa msukosuko mwengine katika Bundesliga.

Haile Gebrselassie wa Ethiopia, alitamba tena jana mjini Berlin,Ujerumani: Mwaka mmoja tangu kuivunja ile rekodi ya dunia ya mkenya Paul Tergat,Gebrselassie, alirudi Berlin kuivunja rekodi alioiweka mwaka jana kwa muda wake wa masaa 2 dakika 3 na sek.59 na hivyo kuipunguza ile ya mwaka uliopita, kwa sek.27.

Kwavile Haile Gebrselassie alishinda pia mbio hizi za Berlin marathon 2006, amekuwa mwanariadha wa kwanza kushinda Berlin marathon mara 3 mfululizo.Mwishoe Gebre alisema,

"Nimefurahi sana ,kwani kila kitu kimekwenda vyema,watiaji kasi na mashabiki."

Akaongeza kusema, "Mji wa Berlin ni mji wangu wa bahati".

Gebrselassie alimtangulia mkenya James Kwambai aliemaliza wapili na mkenya mwengine Charles Kamathi aliebidi kuridhika na nafasi ya 3.

Gebreselassie alikimbia mbio za mita 10.000 tu katika michezo ya Olimpik ya Beijing mwezi uliopita na kumaliza nafasi ya 6.Alikwepa kushiriki mbio za Olimpic marathon kutokana na hali ya hewa ya jiji la Beijing ambayo alihisi ingeathiri afya yake.

Gebrselassie ni bingwa mara mbili wa Olimpik wa masafa ya mita 10.000 na sasa ameinyanyua rekodi ya dunia kutoka pale ilipoachwa na Paul Tergat kwa muda wa sek. 57 katika mbio 2 zilizopita za Berlin marathon.Muda wa Paul Tergat ulikuwa masaa 2 dakika 4 na sek.55. hapo 2003.

Upande wa wanawake, Irina Mikitenko wa Ujerumani ndie mshindi na amekuwa mkimbiaji wa 4 bora kabisa katika historia ya mbio za marathon.Muda wake ulikuwa masaa 2:19:19. Irina alishinda mbio za London marathon mapema mwaka huu.Mikitenko anapanga sasa kutamba katika mbio za ubingwa wa dunia wa riadha hapo August,mwakani-siku yake ya kuzaliwa.

Mbio za Berlin marathon hapo jana zilijumuisha wanariadha 40.000 na ni sehemu ya mbio maarufu za marathon ulimwenguni.

Tukigeukia sasa Ligi mashuhuri za Ulaya kabla duru ya kati ya wiki hii ya champions League-kombe la klabu bingwa barani Ulaya,mabingwa wa Ujerumani-Bayern Munich wameangukia nafasi ya 9 ya ngazi ya Ligi baada ya kuchapwa bao 1:0 na Hannover.

Lawama zimetolewa kwa kocha wao Jurgen klinsmann aliechezesha timu bila ya mastadi 4 wenye hekima za kurekebisha mchezo-mbrazil Ze Roberto,waerumani Bastian Schweinsteiger na Lukas Podolski na mfaransa Franck Ribery.Wote hawa walikuwa wamekaa ubaoni pale hannover ilipoichezesha Munich kindumbwendumbwe.

Hii inafuatia pigo kali la wiki moja kabla ilipozabwa mabao 5-2 na Werder Bremen.

Huu ulikuwa mpambano wa 6 msimu huu tangu Bayern Munich kuongozwa na Klinsmann aliepata umaarufu alipoingoza Ujerumani katika kombe la dunia 2006 hapa Ujerumani na kumaliza 3 nyuma ya mabingwa wa dunia-Itali na makamo Ufaransa.

Hadi sasa,Munich imeshinda mara 2,imetoka sare 2 na imeshindwa mara 2 chini ya Jurgen Klinsmann.

swali ni je, kwa muda gani meneja wa Bayern Munich Uli Hoeness atamvumilia Klinsmann ?

Hoeness amenukuliwa kusema "Ninakasirika nikiangalia orodha ya Ligi."

Kwahivyo, nafasi ya Klinsmann kama kocha itakua na uhakika tu iwapo Munich itashinda na changamoto ijayo ni hapo kesho itakapoteremka katika champions league kupambana na Olympique Lyon ya Ufaransa.

Klinsmann binafsi asema:

"Inakera sana ,kwani haikustahiki kabisa kutokea hivyo.Lakini,ndio imeshatokea na haiwezekani kubadilisha.jumaane tuna kibarua kingine na Olympique Lyon."

Bayern munich imeshinda mpambano wake wa kwanza katika champions League na Steua Bucharest ya Rumania kwa bao 1:0.Ikiwa Munich itateleza tena kesho,basi shoka la kumfyeka klinsmann litaanza kumeta-meta.

Hamburg ndio inayoongoza Bundesliga wakati huu na mwishoni mwa wiki ilitamba kwa bao 1:0 mbele ya Borussia Dortmund.Bremen ilitokwa na jasho kabla kuzima vishindo vya Hoffenheim kwa mabao 5-4.

Katika Premier League-ligi ya Uingereza,Chelsea na liverpool ziko kileleni baada ya Chelsea kuitimua Stoke Coty kwa mabao 2:0 na Liverpool kuizaba Everton 2:0.

Aston Villa ikiwa nafasi ya tatu ya ngazi ya Ligi imeichapa Sunderland mabao 2-1.

Katika La Liga-ligi ya Spain Valencia ingali kileleni kwa pointi zake 13 ikifuatwa na Villareal huku Real Madrid ikinyatia nafasi ya 3.

Valencia ilitandika Huelva mabao 4-2 wakati Villa iliichapa Sporting Gijon bao 1:0.

Huko nchini Itali, AC Milan wamewalaza mabingwa Inter Milan bao 1:0 katika mechi ya patashika kubwa kati ya watani 2 wa mjini-hii iliongoza kwa Lazio Roma kuipiku Inter na kushika usukani wa ligi.Ronaldinho ndie alilifumania lango la Inter Milan kwa bao lake maridadi la kichwa mnamo dakika ya 36 ya mchezo kufuatia mkwaju kutoka kwa Kaka.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com