Gbagbo ashtakiwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.08.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Gbagbo ashtakiwa

Aliyekuwa rais wa Cote d'Ivoire Laurent Gbagbo na mke wake Simone, ameshtakiwa kwa mara ya kwanza kwa makosa mbalimbali ikiwemo "uhalifu wa kiuchumi".

default

Laurent Gbagbo

Mwendesha mashtaka nchini Cote d'Ivoire Simplice Kouadio Koffi amesema rais huyo wa zamani, Laurent Gbagbo mwenye umri wa miaka 66 pia ameshtakiwa kwa makosa ya unyang'anyi wa kutumia silaha, uporaji na uharibufu wa mali ya umma.

Kulingana na mwendesha mashtaka huyo Simone Gbagbo mwenye umri wa miaka 62, alishtakiwa pia kwa makosa sawa, hususan  dhidi ya uendeshaji wa shughuli za sekta ya benki.

Amefahamisha kwamba Gbagbo alishtakiwa jana jioni, na kwamba mke wake alishtakiwa Jumanne ya wiki hii na kuondolewa katika kifungo cha nyumbani alipokuwa na kupelekwa gerezani. Hata hivyo rais huyo wa zamani atabakia katika makaazi ambayo anashikiliwa sasa.

Serikali ya Rais Alassane Ouattara imekamilisha sasa utoaji hukumu wa viongozi katika utawala wa zamani, ambao walituhumiwa kutumia machafuko yaliyokuwepo dhidi ya raia walioonekana kuwa ni wafuasi wa Ouattara, wakati na baada ya uchaguzi nchini humo uliofanyika Novemba mwaka jana, pamoja na kuiibia hazina ya serikali kwa wale waliobaki madarakani licha ya vikwazo vilivyowekwa na nchi za magharibi.

Alhamisi iliyopita, serikali ya Cote d'Ivoire iliwakamata wanajeshi 57 waliokuwa katika utawala wa Gbagbo na kuwashtaki kwa makosa ya uhalifu kuanzia ya mauaji na utekaji nyara, kuhatarisha usalama wa taifa pamoja na kununua silaha haramu.

Katika wiki hiyo pia, aliyekuwa kiongozi wa chama cha siasa cha bwana Gbagbo Pascal Affi N'Guessan na watu wengine 11 walishtakiwa kwa makosa ya kuhujumu usalama wa taifa kutokana na kukataa kwake kukiri kushindwa katika uchaguzi, ambao ulipelekea nchi hiyo kukaribia kuingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Gbagbo pia alilaumiwa na mataifa ya magharibi pamoja na viongozi wa nchi za Kiafrika kwa kuyakataa matokeo yaliyothibitishwa na Umoja wa Mataifa kwamba alishindwa na Rais Ouattara katika uchaguzi huo, uliofanyika Novemba mwaka jana.

Kiongozi huyo wa zamani aligoma kujiuzulu na kuyatumia majeshi kupambana na waandamanaji waliokuwa wakimpinga. Watu 300 waliuawa katika machafuko hayo yaliyoikumba nchi hiyo huku wengine milioni kuyakimbia makaazi yao.

Kufuatia kufunguliwa mashtaka kwa Gbagbo na wafuasi wake, kumekuwa na malalamiko kwamba hakuna hata mtu mmoja kutoka katika upande wa Rais Ouattara aliyekamatwa, licha ya ushahidi kuonesha kuwa nao pia walitenda uhalifu.

Alhamisi iliyopita, ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo lililituhumu jeshi la Rais Ouattara kwa mauaji katika kipindi cha mwezi uliopita.

Mwezi June mwaka huu, Mwendesha mashtaka mkuu katika mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa kivita Luis Moreno-Ocampo alitaka ruhusa ya majaji kuchunguza madai ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu kufuatia machafuko yaliyotokea baada ya uchaguzi nchini humo.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp, reuters)

Mhariri:Josephat Charo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com