Gazetini | Magazetini | DW | 02.07.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Gazetini

Uchambuzi wa wahariri umetuwama juu ya ukosefu wa kazi Ujerumani na Mkataba wa Lisbon wa UU.

Uchambuzi wa wahariri wa magazeti ya leo ya Ujerumani, umetuwama mno juu ya taarifa ya hivi punde iliotolewa na Idara ya Leba juu ya ukosefu wa kazi nchini Ujerumani na mjadala motomoto kuhusu hatima ya Mkataba wa Lisbon wa Umoja wa Ulaya baada ya kukataliwa na wapigakura wa Jamhuri ya Ireland na kubisha kwa rais wa Poland kuidhinisha.

"Rais Kaczynski wa Poland, hatautia saini mkataba huo ingawa Bunge la nchi yake limeuidhinisha.Rais wa Ujerumani Horst Köhler, ameamua kutotia saini kwa kuwa tu angefanya hivyo, mahakimu wa Mahkama Kuu ya Katiba ya Ujerumani wangemzuwia.Mahakimu hao wamo kuukagua mkataba huo kujua iwapo hauendi kinyume na katiba ya Ujerumani.Wakati rais Kazcynski hasa anamlipizia kisasi waziri-mkuu aliechukua nafasi ya nduguye ,Rais Köhler wa Ujerumani ametumia busara.

Wanasiasa wamepoteza nafasi ya muda mrefu waliokuwa nayo -laendelea kusema gazeti, kuwaeleza wapigakura wao maana hasa ya mkataba huo na kwanini muungano wa Ulaya hauwezikani kwa aina nyengine.

Gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG linadhani:

Rais wa Poland hatautia saini mkataba huo kwa kadiri itavyowezekana.Mbali na hayo, mkataba huo pia umezimwa mjini Prague kwa kadiri Mahkama Kuu ya huko nayo haikutoa hukumu yake na hata Ujerumani rais Köhler anangoja hukumu kutoka Karlsruhe.

Utaratibu unaotumiwa kwa mafanikio tangu miaka ya 1950 na Umoja wa ulaya kuimarisha muungano haufai tena.

Wapigakura wengi wana shaka-shaka nao na si wachache wanaopinga jinsi Umoja wa Ulaya unavyopanuka na kuendelea.

Huenda hii ikawa hali ya muda mfupi, lakini kura za maoni zilizopigwa Ufaransa,Holland na hivi punde Jamhuri ya Ireland juu ya katiba na mkataba, zimedhihirisha wazi ukweli huu wa kisiasa.Iwapo mkataba wa Lisbon utashindwa au utakuja kuokolewa,kunahitajika mjadala motomoto na ulio wazi juu ya maana na shabaha inaolenga UU.

Ama gazeti la Landeszeitung linalochapishwa Lüneburg laandika:

Uhuru na sheria ni miongoni mwa mafanikio makubwa ya Umoja wa Ulaya.Umoja lakini ni miongoni mwa udhaifu wake mkubwa.Yule alietarajia kukataa kwa wapigakura wa Ireland ni kilele cha msukosuko kimefikiwa,huyo hakumtia maanani kile atakachozusha rais wa Poland.

Lech Kaczynski anaucheza tena mpira wake anaoupenda-yeye hupenda kutia breki safari ya Umoja wa Ulaya inakoelekea.

Kukataa kwake hivi sasa kuutia saini mkataba ni kumfanyia kero waziri mkuu wa sasa wa Poland ,Bw. Tusk anaeungamkono mkondo wa Ulaya.Isitoshe, kunabainisha msimamo wake...."

Mwishoe, tumalizie kwa ripoti ya mwezi uliopita ya ukosefu wa kazi nchini Ujerumani iliotoka jana:

Gazeti la WESTFALEN-BLATT:

"...Tangu Februari ,2005, idadi ya wasio na kazi imepungua kwa kima cha milioni 2.1 kutoka milioni 5,3.

Hata mwezi uliopita wa Juni,maalfu ya wajerumani waliokuwa hawana kazi, walijipatia kazi.Mambo yafaa kuendelea hivyo.Lakini, tangu miezi sasa ishara zimeibuka zenye kubainisha kuzorota upya kwa uchumi.....Kuanzia 2009 ukuaji wa uchumi kwa maoni ya Taasisi ya IFO utakua 1%.Hii haitatosha kabisa kujipatia nafasi mpya za kazi."