Gavana wa Nairobi Mike Sonko aachiliwa kwa dhamana | Matukio ya Afrika | DW | 11.12.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Gavana wa Nairobi Mike Sonko aachiliwa kwa dhamana

Huko nchini Kenya, mahakama katika mji mkuu, Nairobi, imemuachilia kwa dhamana Gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko, kwa masharti ya kuweka bondi ya dola elfu 15 sawa na shilingi milioni 15 za Kenya.

Mike Mbuvi Sonko, alifikishwa katika mahakama ya Milimani kwa gari la wagonjwa akitokea Hospitali ya Rufaa ya Kenyatta, alikokuwa akitibiwa, huku akiwa amevalia mavazi mekundu kuanzia kichwani. Hata hivyo hakimu Mkuu Dauglas Ogoti alipofika mahakamani, Sonko alivua kofia hiyo nyekundu na huku akisubiri hatma yake iliyokuwa mikononi mwa hakimu huyo.

Sonko pamoja na maafisa wakuu katika kaunti ya Nairobi, wanatuhimiwa kwa makosa 18 yakiwemo ya ufisadi, uhalifu wa kiuchumi, kupokea rushwa na matumizi mabaya ya afisi. Waliyakana makosa hayo walipofikishwa mahakamani siku ya Jumatatu. Sasa ana kila sababu ya kutabasamu lakini kwa kipindi kipi?

Katika kipindi chote ambacho atakuwa nje, gavana huyo hataruhusiwa kuingia ofisini kutekeleza majukumu yake kama gavana. Hatua hiyo ni nafuu kwa Sonko ambaye hana naibu baada ya kuwapiga kalamu manaibu wake. 

Kenia Gouverneur Mike Mbuvi Sonko (DW/S. Wasilwa)

Mike Sonko(kulia) akiwa mahakamani

Sonko anakabiliwa na makosa mengine ya kumdhulumu afisa wa polisi na kukataa kukamatwa katika mahakama ya Voi. Haijulikani iwapo akiondoka mahakamani atatiwa nguvuni tena na kufikishwa kujibu makosa hayo. Akisoma uamuzi wake, Ogoti aliibua masuala ya kimsingi.

Katiba inaeleza kuwa kwa mmoja kugombea kiti chochote cha kisiasa anastahili kupata cheti cha uadilifu kutoka kwa idara ya Polisi, pamoja na Tume ya Kukabilina na Ufisadi, hivyo suala la Sonko kupasi na kugombea ubunge na kisha baadaye ugavana linaacha masuala mengi zaidi ya majibu. Hivyo Ogoti alitoa masharti ya Sonko kuwasilisha vyeti vya konesha uadilifu wake mahakamani kabla ya kupewa dhamana hiyo.

Sonko aliwakilishwa na mawakili 12 wakiwemo masenta wawili, kiongozi wa maseneta wengi katika bunge la Seneti Kipchumba Murkomen na Mutula Kilonzo. Rais Uhuru Kenyatta mara kwa mara akisema kuwa mafisadi wanastahili kubeba mizigo yao.

Gavana huyo mwenye umri wa 44 anayependa mbwembwe na dhahabu amevutia mahasimu na mashabiki kwa kiwango sawa, huku wengi wakihisi kuwa hajatosha katika utendaji kazi wake katika kaunti ya Nairobi.