Frelimo na Renamo zaeleza nia ya kuepusha vita Msumbiji | Matukio ya Afrika | DW | 23.10.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Frelimo na Renamo zaeleza nia ya kuepusha vita Msumbiji

Rais wa Msumbiji Armando Guebuza na upinzani Renamo wameelezea nia ya kuiepusha nchi hiyo kurudi tena katika vita, baada ya waasi wa zamani kutangaza kuuvunja mkataba wa amani wa mwaka 1992

Siku mbili za machafuko ya kulipiza kisasi zimeongeza hofu kuwa Msumbiji huenda likatumbukia tena katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, ikiwa ni miongo miwili baada ya kumalizika mojawapo ya migogoro mikubwa zaidi ya umwagaji damu barani Afrika ambapo karibu watu milioni moja waliuawa.

Wafuasi wa Renamo, ambacho sasa ni chama cha upinzani, walikishambulia kituo kimoja cha polisi hapo jana, saa chache baada ya kundi hilo kutangaza kuwa shambulizi la serikali katika kambi yao liliuvunja mkataba wa amani ambao ulimaliza mapigano yaliyodumu miaka 16. Lakini kupitia mazungumzo na mpatanishi huru Lourenco do Rosario, Renamo imesisitiza kuwa haitaki kurudi tena vitani. Badala yake, imewataka wanajeshi wa serikali kuondoka kutoka kambi waliyoiteka siku ya Jumatatu, katikati ya milima ya Gorongosa, na kuahidi kutoanzisha mapigano.

Kiongozi wa kundi la upinzani la Renamo Afonso Dhlakama akiwa katika kambi yake

Kiongozi wa kundi la upinzani la Renamo Afonso Dhlakama akiwa katika kambi yake

Rais Armando Guebuza pia alitangaza upya nia yake ya kuwa “mazungumzo ndiyo njia pekee ya kusonga mbele licha ya vurugu hizo”. Polisi walitoroka kambi yao katika mji wa katikati wa Maringue wakati wapiganaji wa Renamo walipoanza kufyatua risasi mapema jana huku mvutano baina ya waasi hao wa zamani na chama tawala cha Frelimo ukiongezeka.

Lakini mtafiti wa Taasisi ya Masuala ya Kimataifa ya Afrika Kusini Aditi Lalbahadur anasema haiwezekani kuwa nchi hiyo itatumbukia tena vitani. Lalbahadur anasema Renamo haina uwezo wa kuanzisha vita na kwamba vita siyo sehemu ya matakwa ya serikali ijapokuwa ina jeshi dhabiti. Renamo inadai kuwa na uwakilishi zaidi katika tume ya uchaguzi na jeshini.

Shule zimefungwa katika eneo karibu na kambi ya kijeshi ya Renamo katika milima ya Gorongoso ambayo ilitekwa na jeshi la serikali hatua ambayo waasi wanasema ililenga kumuuwa kiongozi wao Afonso Dhlakama. Rais Guebuza alisema jeshi lilichukua hatua ya kujikinga baada ya wapiganaji wa Renamo kuwafyatulia risasi. Dhlakama alitoroka kabla ya shambulizi hilo lakini yuko tayari kurudi katika meza ya mazungumzo wiki hii.

Huku ikielekea katika uchaguzi wa mitaa mwezi ujao na uchaguzi mkuu mwaka wa 2014, Msumbiji ina historia ya machafuko yanayohusiana na uchaguzi. Marekani imesema katika taarifa imezitaka pande zote mbili kuchukua hatua mwafaka za kutuliza mivutano baina yao.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP

Mhariri: Josephat Charo