Francois Hollande kukutana na Obama Washington | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.11.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Francois Hollande kukutana na Obama Washington

Rais Barack Obama wa Marekani ataonesha mshikamano na rais wa Ufaransa Hollande katika ikulu ya Marekani leo(24.11.2015), siku 11 baada ya kundi la Dola la Kiislamu kufanya mashambulizi kadhaa ya mauaji mjini Paris.

NSA Abhöraffäre Obama mit Hollande Symbolbild

Rais Hollande (kushoto) na rais Obama (kulia)

Lakini Hollande huenda akaondoka Washington bila ya uungwaji mkono imara kwa wito wake wa kuiingiza Urusi katika muungano mpya utakaopambana na makundi yenye itikadi kali.

Ziara ya Hollande mjini Washington ni sehemu ya msukumo wa kidiplomasia kuwezesha jumuiya ya kimataifa kuimarisha kampeni dhidi ya wanamgambo wa kundi la Dola la Kiislamu.

Putin bei Hollande in Paris

Rais Hollande (kushoto) na rais Putin wa Urusi(kulia)

Kundi hilo linaaminika kuhusika na mashambulio ya Novemba 13 ambayo yamesababisha vifo vya watu 130 mjini Paris, pamoja na mashambulizi mengine tofauti nchini Lebanon, na Uturuki na kuiangusha ndege ya abiria ya Urusi nchini Misri.

Wakati kundi la itikadi kali la Dola la Kiislamu likipanua uwezo wake nje ya eneo lake inalolidhibiti nchini Syria na Iraq , Obama anakabiliwa na mbinyo mkali nyumbani na nje ya nchi hiyo kuongeza juhudi za nchi hiyo kulivunja kundi hilo la wanamgambo.

Dschihad-Kämpfer im Irak

Wapiganaji wa Jihadi nchini Iraq

Baada ya Paris Ufaransa yaongeza mashambulizi

Hadi sasa , Obama anasita kuitikia miito ya ama kubadilisha ama kuimarisha msimamo wake, na badala yake analenga kuyaleta pamoja mataifa mengine zaidi ili kupata taarifa nyingi zaidi za kijasusi za kupambana na kundi hilo, na kupata usaidizi zaidi wa masuala ya kiutu na kijeshi.

Kampeni ya Marekani imelenga zaidi katika kushambulia, pamoja na mafunzo na usaidizi kwa majeshi ya usalama ndani ya Iraq. Juhudi za kutoa mafunzo na kuyapa silaha makundi ya waasi yenye msimamo wa wastani nchini Syria hazijatosha, licha ya kwamba Obama aliidhinisha kuwekwa kwa kikosi maalum cha wanajeshi 50 nchini humo ili kuanzisha mpango huo.

Ufaransa imeongeza mashambulizi yake ya anga nchini Syria , kufuatia mashambulizi dhidi ya Paris, ikitegemea kwa sehemu fulani taarifa za kijasusi za Marekani katika eneo la Raqqa, ngome kuu ya wanamgambo wa Dola la Kiislamu nchini Syria. Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron amesema jana kuwa atahitaji kupata ridhaa ya bunge la nchi hiyo wiki hii ili Uingereza iweze kuanza mashambulizi ya anga pia.

Obama beim Gipfel zu Terrorismus im Rahmen der UN-Vollversammlung

Rais Barack Obama wa marekani

Wakati huo huo Ubelgiji itaendelea kuwa katika kiwango cha juu cha kitisho cha usalama kwa wingi nyingine kuhusiana na hofu ya shambulio la kigaidi, imesema serikali ya Ubelgiji, wakati Marekani imetoa tahadhari kwa Wamarekani wanaotaka kusafiri sehemu mbali mbali duniani.

Usalama katika viwanja vyetu vya ndege haukutengenezwa kumkamata mtu wakati akipanda ndege. Umepangwa kuanza kuwakagua watu mara wanapoanza kutafuta kukata tikiti.

Deutschsprachiges IS-Video Mohamed Mahmoud Screenshot

Mpiganaji wa kundi la IS nchini Iraq

Maafisa nchini Ubelgiji na Ufaransa wanafanya msako kumtafuta Salah Abdeslam mzaliwa wa Ubelgiji , mshukiwa muhimu katika mashambulio ya mjini Paris hapo Novemba 13, ambapo watu wenye silaha na mshambuliaji wa kujitoa muhanga wameuwa watu 130.

Polisi ya Ufaransa leo imekuwa ikichunguza mkanda unaoshukiwa kuwa unatumiwa na watu wanaojiripua sawa na ile iliyotumika katika mashambulizi ya mjini Paris, kwa mujibu wa duru karibu na uchunguzi huo.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre

Mhariri: Yusuf Saumu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com