Fidel Castro ajiuzulu | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 19.02.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Fidel Castro ajiuzulu

Rais Fidel Castro wa Cuba

Rais Fidel Castro wa Cuba

Kiongozi mkongwe wa Cuba Fidel Castro amejiuzulu mapema leo asubuhi kama Rais wa taifa hilo baada ya kushika wadhifa huo kwa karibu nusu karne.Castro alielezea uamuzi wake huo katika barua iliochapishwa na Shirika rasmi la habari la nchi hiyo.


Fidel Castro alisema katika barua hiyo iliochapishwa pia katika gazeti la chama cha kikoministi linalotoka kila siku Granma, kwamba hatokubali muhula mwengine, wakati bunge litakapokutana Jumapili ijayo na akasisitiza " Sitokubali au kushawishi kuuendelea kuwa rais wa baraza la taifa au kamanda mkuu wa majeshi.


Baraza jipya la taifa litakutana Jumapili ijayo ikiwa ni kwa mara ya kwanza tangu Januari, kulichagua baraza tawala la taifa, akiwemo wadhifa wa rais ambao umekua ukishikiliwa na Castro. Tangazo la Castro mwenye umri wa miaka 81 kwa hivyo , linamaliza utawala wake wa karibu nusu karne, na kumuweka nafasi ya usoni nduguye Raul mwenye umri wa miaka 76 kuchukua nafasi yake


Harakati za Castro hadi kufikia kukamata hatamu za uongozi zilianzia Desemba 2, 1956, wakati akiwa pamoja na wana mapinduzi wenzake akiwemo Che Guevara, walipoanza uasi dhidi ya utawala wa Batista kwa kufika kusini mashariki mwa kisiawa hicho kwa meli baada ya kuwa uhamishoni waliokoandaa uasi huo.


Miezi ishirini na tano baadae wakamuangusha batista na Castro akatangazwa Waziri mkuu

Castro anayeitwa na wafuasi kwa jina la "Fidel au El Comandante" na aliyewahi kusomea sheria akajiweka karibu na Urusi ya zamani na kambi ya mashariki, nchi zilizouunga mkono utawala wake wa kikoministi hadi kusambaratika kwa uliokua muungano wa kisovieti 1989.


Muda wote alikua na uhasama na Marekani. pamoja na hayo amewashuhudia Marais 10 wa Marekani wakiingia madarakani na kutoka, licha ya shinikizo la zaidi ya miongo minne kwa sababu ya sera yake ya mapinduzi.

Katika kuungwa mkono na Urusi kwa hali na mali, dola hilo mkubwa liliweka hata makombora ya kinuklea, katika kuisaidia Cuba kukabiliana na kitisho cha Marekani 1962, baada ya kushindwa jaribio la kukivamia kisiwa hicho lililofanywa na wacuba uhamishoni lina kuungwa mkono na shirika la ujasusi la Marekani-CIA Aprili 1961.Cuba ikavunja uhusiano wa kibalozi na Marekani.


Castro alikua pia kwa muda mrefu Kiongozi mwenye usemi miongoni mwa mataifa ya ulimwengu wa tatu katika mvutano baina ya mashariki na magharibi. Alituma wanajeshi 15,000 kuiasaidia serikali ya Angola 1975 ya chama cha MPLA na kutuma pia wanajeshi Ethiopia 1977 wakati wa utawala wa Mengistu Haile Mariam.


Baada ya kuporomoka kwa iliokua Urusi ya zamani uchumi wa Cuba nao ulikaribia kuporomoka na Castro akalazimika kuruhusu watalii wa kigeni kuizuri nchi hiyo pamoja na kuanzisha marekebisho madogo ya kiuchumi. Licha ya vikwazo vya kiuchumi vya Marekani Cuba imeendelea kuhimili hali ngumu, hadi tangazo la kujiuzulu kwa Fidel Castro hii leo.

 • Tarehe 19.02.2008
 • Mwandishi Abdulrahman, Mohamed
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/D9g6
 • Tarehe 19.02.2008
 • Mwandishi Abdulrahman, Mohamed
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/D9g6
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com