1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu milioni 22 wanakabiliwa na ukosefu wa chakula Congo

16 Oktoba 2020

Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo - FAO, limejulisha kwamba watu karibu milioni 22 wanakabiliwa na ukosefu wa chakula katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Leo ni Siku ya Kimataifa ya chakula. 

https://p.dw.com/p/3k0zT
Kongo: Alltagsleben in Brazzaville
Picha: Getty Images/AFP/M. Jourdier

Miongoni mwa sababu za ukosefu wa chakula hapa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni pamoja na usalama mdogo, vita vya kikabila na migogoro mbalimbali inayosababishwa na vikundi vinavyomiliki silaha.

Ndivyo ilivyoripotiwa na shirika la umoja wa mataifa la chakula na kilomo, FAO kufuatana na utafiti wake wa kila mwaka.

Mwakilishi wa shirika hilo nchini hapa, Aristide Ongone Obame, alieleza DW kwamba kilichoifanya idadi ya wanaokosa chakula kuongenzeka mwaka huu, ni janga la Covid-19 linaloikumba mikoa 21 miongoni mwa 26 ya nchi hii, na ndiyo maana hali ya watu karibu milioni 22 imekuwa mbaya. Aristide Ongone Obame. ((Hatua zote zilizochukuliwa na serikali sawa kutoruhusu safari baina ya mikoa hapa nchini, tunajuwa baadhi ya mikoa inakosewa, na kama hazipate kitu toka Kinshasa, watu wanakumbwa na hali jinsi ilivyo leo. Pia mambo ya vita bado inagonga maeneo mengine, na hivyo, hali ya ukosefu wa chakula ni hatari.))

FAO, Food and Agriculture Organisation of the United Nations, Logo
FAO: Janga la Corona limechangia uhaba wa chakulaPicha: AP Graphics

Athari za virusi vya korona ni vingi hapa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambako kuwepo kwa ugonjwa huo kulisababisha shughuli nyingi kusimamishwa zikiwemo na shule. Ni mwanzoni mwa wiki hii ndiyo shule zilifunguliwa tena baada ya miezi sita bila kusoma.

Mkuu wa shirika la umoja wa mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO, Audrey Azoulay, alikuwa ziarani hapa nchini tangu Jumatano na akaizuru shule la wasichana Kabambare ili kujionea hali ilivyo, na kuhimiza zaidi kuhusu wanafunzi kurejea shuleni.

Bi Audrey amesema shirika UNESCO litaunga mkono utekelezaji hapa nchini wa hatua ya elimu bila malipo ambayo imeruhusu watoto wengi kwenda shuleni. Shirika hilo litatowa kipaumbele kuwaelimisha wasichana kwani ndio wengi huacha shule kabla kumaliza. Huyu hapa Bi Adrey Azoulay. ((Tunachokitarajia kwanza wakati huu ni uhimizaji kuhusu umuhimu wa kuwarejesha wasichana shuleni kwani, tuna hofu kwamba katika nchi nyingi pamoja na Kongo, kusimamishwa kwa shule ni fursa ya upungufu wa idadi na hofu kubwa ni kwamba mabinti wanaweza wasirejee shuleni.))

Shirika la umoja wa mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO, linaandaa kuanzisha kampeni hiyo ya uhimizaji kwani linalo hofu wasichana milioni 11 wanaweza wasirejee shuleni baada ya shule kuanzishwa tena.

Mwandishi: Jean Noel Ba-Mweze/DW, Kinshasa