EU yazindua operesheni ya ulinzi katika Bahari ya Shamu
20 Februari 2024Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen amesema Ulaya itahakikisha uhuru wa kusafiri katika Bahari ya Shamu, ikishirikiana na washirika wake wa kimataifa.
Afisa mmoja alisema operesheni hiyo ya Ulaya itapewa jina la Aspides katika kigiriki, kumaanisa ngao, na itajumuisha manowari nne. Marekani tayari inaongoza muungano wake wa jeshi la wanamaji katika eneo hilo na imefanya mashambulizi ya kulipiza kwenye maeneo ya Wahuthi nchini Yemen, ikishirikiana na Uingereza.
Mashambulizi kadhaa ya Wahuthi yamevuruga usafiri wa meli katika Bahari ya Shamu, na kuzilazimu baadhi ya kampuni kutumia njia mbadala ikiwemo kuzunguka upembe wa kusini mwa Afrika safari inayochukua wiki mbili.
Jana jioni, Wahuthi walisema walizilenga meli tatu katika saa 24 zilizopita, ikiwemo meli iliyosajiliwa Uingereza ya Rubymar, meli inayomilikiwa na Marekani Sea Champion na Navis Fortuna walioielezea kuwa ya “Kimarekani.“
Wahuthi ambao wanaungwa mkono na Iran, na kudhibiti sehemu kubwa ya Yemen, wamekuwa wakitatiza safari za meli tangu Novemba katika kampeni wanayosema ni ya mshirikamo na Wapalestina wa Gaza wakati wa vita vya Israel na Hamas.
AFP