EU Ivory Coast
30 Desemba 2010Duru za kibalozi zimearifu kuwa Umoja wa Ulaya utaongeza vikwazo hivyo mwezi ujao kwa lengo la kumbana rais Laurent Gbagbo mpaka aondoke madarakani.
Pamoja na vikwazo hiyvo ni kuongeza orodha ya watu wa Gbagbo watakaopigwa marufuku kuingia katika nchi za Umoja wa Ulaya. Wawakilishi wa serikali 27 za nchi za Umoja wa Ulaya walifikia uamuzi huo kwenye mkutano wao uliofanyika mjini Brussels.
Wawakilishi hao wamesema vikwazo zaidi vitawekwa dhidi ya Gbagbo na wapambe wake ikiwa pamoja na kuzuia mali za Gbagbo anaeng'ang'ania madaraka pamoja na zile za wafuasi wake
Kuanzia mwezi ujao Umoja wa Ulaya utaongeza idadi ya watu watakaokumbwa na vikwazo hivyo na kufikia 61 kutoka 19.
Mwakilishi mmoja wa kibalozi ameliambia shirika la Reuters kwamba palikuwa na makubaliano katika matumaini ya kuchukua hatua nyingine kuanzia mwezi januari dhidi ya Gbagbo na wafuasi wake.
Rais huyo alishindwa na mpinzani wake Alassane Outtara katika uchaguzi wa rais uliofanyika nchini Cote d'Ivoire mwezi uliopita.
Umoja wa Ulaya kwanza uliwekwa vikwazo dhidi ya Gbagbo na wafuasi wake mwanzoni mwa mwezi huu ili kumshinikiza aondoke.
Katika hatua nyingine wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa imefahamisha kwamba Umoja wa Ulaya utawatambua wajumbe wa kiongozi wa upinzani Alassane Outtara kuwa wawakilishi halali wa Cote d'Ivoire.
Uchaguzi uliofanyika tarehe 28 mwezi novemba nchini Cote d'ivoire ulikuwa na shahaba ya kuurejesha umoja nchini humo, baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 2002 hadi 2003. Tume ya uchaguzi ya muda ilionyesha kuwa kiongozi wa upinzani Alassane Outtara alishinda kwa zaidi ya asilimia 8. Lakini hesabu hizo zilibadilishwa haraka sana na mahakama ya katiba ya Cote d'ivoire inayoongozwa na mshirika mkubwa wa Gbagbo.
Na ghasia zilizofuatia baada ya matokeo kutangazwa zimesababisha vifo vya watu zaidi ya 170 na pana hatari ya kuzuka tena vita nchini Cote d'ivoire .
Katika hatua nyingine ya kumshinikiza Laurent Gbagbo,nchi za Umoja wa Ulaya zimekubaliana kuwatambua wale mabalozi tu walioteuliwa na kiongozi wa upinzani Alassane Outtara.
Hatahivyo licha ya hatua hizo za Umoja wa Ulaya Gbagbo bado hajaonyesha dalili yoyote ya kukunjika, badala yake ameilaumu Ufaransa kwa kuongoza kampeni ya kimataifa kwa lengo la kumng'oa madarakani.
Mwandishi/Mtullya Abdu/RTRE/
Mhariri:Mwadzaya,Thelma