DW yavuma kila mahali
17 Januari 2013
Matangazo kusikika, mote mote yaenea
Mpaka na kwetu Afrika, kweli yametufikia
Kiangazi na masika, hatamu kushikilia
Makini na si papara, matangazoye adhimu
Husikika kwa ubora, huachilia utamu
Kwa sauti barabara, zisizo mang’amung’amu
Hutuletea habari, huru zilizo murua
Huongeza umahiri, vipindi kusisimua
Kwa weledi na fahari, maarifa kufunua
Kisima cha maarifa, sifa umejizolea
Sehemu zenye maafa, hujasita elezea
Bila kuogopa kufa, hivyo kutopendelea
Habari zenye mantiki, siasa hata jamii
Zilizo na uhakiki, pasipo na usanii
Ukweli na penye haki, kwa mabaya husifii
Vipindi vyenye kufana, elimu na burudani
Vyawezesha kupambana, na maisha mtaani
Huwaokoa vijana, mbinu tia maanani
Mazingira kukazia, kuelimisha kwa kina
Wanyonge kuwalilia, kwa maisha kutofana
Shamba kutopalilia, kwa mvua kukosekana
Kiswahili kukikuza, sifa iliyotukuka
Kigezo cha kuongoza, ni kweli sio mashaka
Wengi wamesikiliza, na hivyo kuelimika
Hapa mwisho wa kunena, endeleza mapambano
Upate pia heshima, kuhimili mashindano
Usichoke na kukoma, ulete maelewano
Hongera kwa matangazo, yarindimayo hewani
Tanbihi: Shairi hili limeandikwa na msikilizaji Jpseph Mwaka kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 50 ya DW.
Mhariri: Mohammed Khelef