1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Ghasia Kongo Mashariki zachochea chuki kwa nchi za Magharibi

Philipp Sandner | Tatu Karema
14 Februari 2024

Mapigano katika jimbo la Kivu Kaskazini nchini Kongo yamesababisha maelfu ya watu kuyahama makazi yao na kuzusha maandamano mapya. Wakongo wengi wanaulaumu UM na mataifa ya Magharibi. Wataalamu wanasema huu ni upotoshaji

https://p.dw.com/p/4cOas
DR Kongo | Waasi wa M23
Waasi wa M23 wanadhibiti maeneo makubwa ya Kivu KaskaziniPicha: Arlette Bashizi/REUTERS

Mapigano ya hivi karibuni katika mji wa Goma Mashariki mwa jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo yamezua wasiwasi kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC), ambalo siku ya Jumatatu lilisema kwamba lina wasiwasi na kuongezeka kwa ghasia katika eneo hilo. Baraza hilo limelaani mapigano hayo yalioanzishwa mapema mwezi huu na waasi wa M23. 

Huku Baraza hilo la Usalama la Umoja wa Mataifa likielezea mashaka kuhusu hali nchini Kongo, siku ya Jumatatu, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alitangaza kwamba nchi yake inapeleka wanajeshi 2,900 kama sehemu ya juhudi za pamoja za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC, ya kutuliza mapigano nchini Kongo. Tayari vikosi vya SADC vinapambana katika ghasia hizo kwa ushirikiano na jeshi la Kongo.

Makabiliano kati ya waasi wa M23 na vikosi vya serikali yamejikita karibu na mji wa Sake. Mji huo ukiwa na takriban wakazi 50,000, Magharibi mwa Goma, jimboni Kivu Kaskazini, unaonekana kama eneo la kimkakati. Onesphore Sematumba, mchambuzi kutoka taasisi ya utafiti ya Crisis Group ameiambia DW.

Ramani | DR Kongo Kiingereza

Sematumba amesema kuwa kabla ya haya, tayari kulikuwa na kambi tatu kubwa za wakimbizi karibu na Goma. Sasa ni Sake yote pamoja na maeneo ya mbali zaidi ambayo wakazi wake walikuwa wamekimbilia Sake hapo awali kuelekea Goma.

Benoit Safari, mmoja wa wakimbizi wengi waliotoroka Sake, anasema alikimbilia Goma siku ya Jumatano iliyopita, ambapo hajui mtu na pia wapi atakapolala usiku na kupata chakula.

Soma pia: Hofu yaongezeka Kongo baada ya M23 kudhibiti mji unaonganisha Goma na Bukavu

Mashirika ya msaada yanasema kuwa mji huo ambao tayari unatatizika kulisha wakazi wake milioni moja na wakimbizi kutoka kaskazini, unakabiliwa na shinikizo kubwa la kukidhi mahitaji ya mamia ya wakimbizi wa ndani wanaowasili kila siku.

Watu wameiambia DW kuwa Goma imekuwa gereza la wazi, huku njia zote za nchi kavu zinazoelekea maeneo mengine ya nje ya mji huo zikiwa zimefungwa na waasi. Hali hii imesababisha kupanda kwa bei za bidhaa za kimsingi.

Sematumba amesema ujio wa wakimbizi wa ndani unasababisha kuongezeka kwa hali ya wasiwasi katika eneo hilo na kuongeze kuwa wakazi wa Goma wameanza kuhofia usalama wao na kutafuta njia ya kutoka katika eneo hilo.

Lakini wanawezaje kufanya hivyo wakati njia pekee ya kutoka nje ya mji huo inaelekea Rwanda? Rwanda inadaiwa kuwaunga mkono waasi wa M23, ingawa serikali ya Kigali imekanusha shutuma hizo.

Nani wa kulaumiwa?

Chuki inaongezeka miongoni mwa watu wa eneo hilo dhidi ya mashirika ya kimataifa kama vile ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo, MONUSCO, unaoonekana kuhusika kwa sehemu katika kuchangia hali hiyo.

Kombe la AFCON | Ivory Coast - DR Kongo
Timu ya taifa ya DR Kongo ilitumia nusu fainali ya AFCON kutoa ujumbe juu ya vurugu zinazoikumba nchi yao.Picha: Franck Fife/AFP/Getty Images

Katika mji mkuu wa Kongo wa Kinshasa, ulio umbali wa kilomita 2,000 kuelekea magharibi, maandamano makali yameelekezwa sio tu katika makao makuu ya MONUSCO, bali pia katika balozi za Ufaransa na Marekani, miongoni mwa nyingine.

Mapema siku ya Jumanne, naibu waziri mkuu ambaye pia ni waziri wa mambo ya ndani wa Kongo, Peter Kazadi, alizuia  pikipiki na wachuuzi wa mitaani kuingia Gombe. Kazadi alisema kuwa wanakumbusha kila mtu kwamba maeneo ya wanadiplomasia wa kigeni na wafanyakazi wa MONUSCO hayapaswi kuingiliwa.

Maandamano yalipamba moto baada ya timu ya soka ya Kongo kushindwa na Ivory Coast katika nusu fainali ya michuano ya soka ya AFCON wiki jana. Ili kuongeza ufahamu kuhusu ghasia zinazoikumba nchi yao, wachezaji wa Kongo waliiga bastola zinazoelekezwa kwenye mahekalu yao na kufunga midomo yao kwa mikono. Picha hizo zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii, na kuzua hisia mseto.

Sematumba amesema kuwa kulaumu watu nje ya Kongo, iwe wachezaji wa kimataifa au taifa jirani la Rwanda, ni jambo la kawaida, lakini alitahadharisha kuwa tatizo ni kubwa zaidi.

Maelfu wakimbia vita Sake