1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC: Juhudi za kusaka utulivu wa Kivu Kaskazini zaendelea

Benjamin Kasembe/DW Goma3 Agosti 2020

Wawakilishi na wajumbe kutoka makabila yote ya jimbo la Kivu ya kaskazini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo waafikiana kutafuta suluhisho la hali mbovu ya usalama inayoshuhudiwa jimbo hilo la mashariki mwa DRC

https://p.dw.com/p/3gM5z
Ruanda-Rebellen von Sylvestre Mudacumura befehligt
Picha: AFP/L. Healing

Jimbo hilo limekumbwa na misukosuko ya ukosefu wa usalama kwa zaidi ya miongo miwili. Raia wake wamekuwa wakiishi katika hali ya vurugu kutokana na kuongezeka kwa idadi ya makundi ya waasi wanaovichoma vijiji moto.

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa kikao hicho kilichodumu kwa siku tatu mfululizo jijini Goma gavana wa mkoa huo Carly Nzanzu Kasivita alibaini kuwa hiyo itakua njia mbadala ya kudumisha usalama wa wakaazi

Wakati huohuo wawakilishi wa mashirika ya kiraia wamedai kuwa bado mkoa huo utaendelea kukabiliwa na uvamizi mkubwa wa makundi ya wanamgambo kutoka nje na ndani ya Congo kufuatia kile walichokiita uzembe wa serikali kushindwa kugunduwa chanzo kinachowapelekea mamia ya vijana kujiunga na makundi hayo ya waasi na kusababisha wasiwasi mkubwa kwa raia.

Wakaazi wa Kivu Kaskazini wamekuwa wakiishi kwa hofu kufuatia machafuko ya miaka mingi
Wakaazi wa Kivu Kaskazini wamekuwa wakiishi kwa hofu kufuatia machafuko ya miaka mingiPicha: picture-alliance/AP Photo/A. K. Maliro

Akizungumza na vyombo vya habari Thomas D'aquin Muiti ambaye ni msemaji wa mashirika ya kiraia nchini Congo amesema kikao hicho hakitoshi kumaliza tofauti kati ya makabila yanayo zozana mashariki mwa Congo kila uchao.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya wawakilishi wa asasi za kiraia mkoani Kivu ya kaskazini kutangaza kurudi upya kwa kundi la waasi wa M23 ambao wameanzisha harakati zao wilayani Rutshuru. Hata hivyo tangazo hilo limeendelea kukanushwa na viongozi wa kundi hilo lililowahi kuuteka mji wa Goma mnamo Novemba 2012.