1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DR Congo: kesi ya Floribert Chebeya ifunguliwe

11 Februari 2021

Mashirika 117 yasiyo ya kiserikali katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, yamedai kuanzishwa tena kesi kuhusu mauaji ya mtetezi wa haki za binadamu Floribert Chebeya, yaliyotokea zaidi ya miaka kumi iliyopita.

https://p.dw.com/p/3pCxK
DRK Oppositionspolitiker Floribert Chebeya
Picha: Etienne Ansotte/dpa/picture-alliance

Ukweli umeendelea kufunikwa zaidi ya miaka kumi sasa kuhusu mazingira ya kuuawa Floribert Chebeya, aliyekuwa Katibu Mtendaji wa shirika la kutetea haki za binaadamu Voix des Sans Voix (VSV) na Fidèle Bazana, dereva wa shirika hilo hilo.
Wanaharakati hao wawili wa haki za binadamu waliuawa mnamo Juni 1, 2010 kwenye ofisi ya Inspekta Mkuu wa Polisi nchini Kongo (PNC), Jenerali John Numbi kama ilivyothibitishwa na maafisa wawili wa polisi waliokimbia, na ambao waliamua kuvunja ukimya wakieleza kwamba walitekeleza agizo la Jenerali Numbi.

Mashirika 117 za kutetea haki za binadamu yameomba Jenerali Numbi akamatwe, mashahidi hawa wawili walindwe pia kulindwa kwa eneo mahali mwili wa dereva Fidèle Bazana ulipo, kama alivyosisitiza Rostin Manketa, Katibu Mtendaji wa la Voix des Sans Voix.
''Tunaomba Jenerali John Numbi Banza Tambo, mshukiwa mkuu katika mauaji ya Floribert Chebeya na Fidèle Bazana, akamatwe haraka; kuanzishwe tena kesi hiyo ya mauaji ili kupambana na uhalifu dhidi ya wanaharakati wa haki za binadamu na demokrasia; yalindwe kwa lengo la uchunguzi maeneo la Jenerali Numbi na haswa lile la Jenerali Selua Katanga maarufu kama Djajijia ambamo mwili wa Fidèle Bazana ulizikwa.''

Je hukumu iliyotolewa iliridhisha wahusika?

Kesi hii iliendeshwa katika Mahakama ya Kijeshi na hukumu iliyotolewa haikuwaridhisha ndugu pamoja na mashirika ya kutetea haki za binaadamu, ambao wanahisi kwamba haikusababisha kukamatwa kwa wauaji halisi.
Jambo analolikubali pia Jean Marie Kabengela, mmoja wa mawakili wa shirika VSV katika kesi hiyo kwenye Mahakama ya Kijeshi. Hofu yake ni kwamba mwili wa Bazana unaweza kuwa tayari umehamishwa. Jean-Marie Kabengela.
''Inawezekana leo kuwa wameuhamisha mwili. Ila cha muhimu ni kulilinda eneo kwani shimo ambalo limechimbwa na likifunikwa tena kutaonyesha dalili.''

Kwa miaka kumi iliyopita, Jenerali John Numbi ameendelea kuwa na cheo cha juu katika jeshi la polisi. Na sasa mambo yameibuka ​​wakati hana tena kazi.