Diplomasia na mzozo wa Syria | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.11.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Diplomasia na mzozo wa Syria

Muungano wa Upinzani wa Syria umedokeza leo Jumamosi (09.11.2013) kuwa tayari kutumia diplomasia kukomesha vita vya miezi 31 wakati kundi hilo likianza mkutano kuamuwa iwapo ushiriki mkutano wa amani wa Geneva.

Rais wa Muungano wa Taifa wa upinzani wa Syria Ahmad Al-Jarba (katikati).

Rais wa Muungano wa Taifa wa upinzani wa Syria Ahmad Al-Jarba (katikati).

Msemaji wa muungano huo Khaled al-Saleh amesema muungano huo umesema mara kadhaa kwamba iko tayari kujihusisha na mchakato wa kisiasa ambao utakidhi matakwa ya wananchi wa Syria.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Waarabu kwa Syria Lakhdar Brahimi hivi karibuni ameimarisha juhudi za kuishinikiza serikali ya Syria na upinzani kuhudhuria mkutano huo uliopangwa na Marekani na Urusi kufanyika Geneva.Hakuna tarehe maalum iliowekwa kwa mkutano huo.

Al-Saleh amekaririwa akisema mjini Istanbul Uturuki ambako muungano huo unaoungwa mkono na mataifa ya magharibi unashiriki mkutano huo wa siku mbili " Tunaamini katika kufikia suluhisho la kisiasa kukomesha mzozo huo lakini hatua za serikali zinaonyesha haiko tayari kushiriki katika mchakato wowote ule makini wa mazungumzo."Pia ameongeza kusema kwamba Rais Bashar al-Assad hatakuwa na nafasi katika serikali mpya ya Syria.

Wasubiri mwaliko wa Umoja Mataifa

Viongozi wa Muungano wa Taifa wa upinzani wa Syria.

Viongozi wa Muungano wa Taifa wa upinzani wa Syria.

Wakati maafisa wengine wa upinzani wamesema uamuzi wa mwisho wa mkutano huo hautotangazwa kabla ya Jumapili,al-Saleh amesema muungano huo ulikuwa unasubiri mwaliko rasmi kutoka Umoja wa Mataifa ili kuhudhuria mkutano huo wa amani.Umoja wa Mataifa ni mdhamini rasmi wa mkutano huo wa "Geneva 2."

Samir al-Nashar mjumbe wa muungano huo wa upinzani ameliambia shirika la habari la dpa kwamba wajumbe wa upinzani wameujadili mkutano huo wa Geneva na balozi wa Marekani kwa Syria Robert Ford.Ameongeza kusema kwamba wamewaambia Wamarekani kwamba ushiriki wao lazima uzingatie hakikisho madhubuti ikiwa ni pamoja na mpango wa wazi na ramani fulani ya kipindi cha mpito.

Rais wa muungano huo Ahmed al-Jarba amesema wiki iliopita mjini Cairo kwamba upinzani hautohudhuria mkutano huo venginevyo kunakuwepo na ratiba kamili ya kuondoka madarakani kwa Rais Assad.Upinzani pia unapinga Iran kuhudhuria mkutano huo kutokana na kuwa muungaji mkono mkuu wa Assad.

Upinzani una matatizo

Baraza la Taifa la Syria ambalo ni kundi kubwa kabisa ndani ya muungano huo wa upinzani limetishia kujitowa katika muungano huo iwapo upinzani huo utaamuwa kushiriki mkutano huo.Muungano huo wa taifa ambao unategemea uungaji mkono wa kigeni kwa muda mrefu imekuwa ikisibiwa na uhasama wa kimajimbo na unaathirika kutokana na kukosa uaminifu kwa washirika wake halikadhalika na makundi mbali mbali ya waasi yanayopigana nchini Syria.

Mjumbe wa amani wa Umoja Mataifa na Jumuiya ya Waarabu kwa Syria Lakhdar Brahimi.

Mjumbe wa amani wa Umoja Mataifa na Jumuiya ya Waarabu kwa Syria Lakhdar Brahimi.

Mapema wiki hii Brahimi alionya kwamba upinzani kwanza lazima wawe na msimamo mmoja na kwamba kunapaswa kuwepo ujumbe wa pande mbili kutoka Syria katika mkutano wa "Geneva 2" yaani wa serikali na ule wa upinzani.Ameongeza kusema kwamba upinzani umegawika na hauko tayari na una matatizo.Hata serikali ya Syria imeonekana haiko tayari hivyo kuhudhuria mkutano huo wa Geneva.

Waziri wa habari Omran al-Zohbi amesema wiki hii kwamba serikali itagoma kwenda iwapo itamaanisha ni kukabidhi madaraka kama ilivyodaiwa na waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Mwana Mfalme Saud al-Faisal na wapinzani fulani wa serikali walioko nje.

Mwandishi: Mohamed Dahman/dpa/AFP/

Mhariri: Amina Abubakar

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com