Dimba mwishoni mwa wiki hii | Michezo | DW | 16.11.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Michezo

Dimba mwishoni mwa wiki hii

Timu kadhaa za kimataifa zitakuwa uwanjani kuania tiketi za kombe lijalo la dunia kanda ya afrika na Amerika kusini;finali za olimpik 2008 Beijing na kama Ujerumani na Itali tiketi za kombe la Ulaya.

Comoro inaandika jumamosi hii historia yake ya dimba kwa mpambano wao wa kwanza wa kimataifa nyumbani mjini Moroni kuania tiketi ya kombe lijalo la dunia 2010 Afrika Kusini. Comoro ina miadi na Madagascar. Simba wa nyika Kamerun,Black Stars Ghana na Tembo wa Ivory Coast- zote 3 zaweza mwishoni mwa wiki hii, zikatia mfukoni tiketi zao za kuliwakilisha bara la Afrika katika dimba la Olimpik mjini Beijing 2008.

Tukianza na kinyan’ganyiro cha kuania tiketi za finali ya kombe la Ulaya mwakani nchini Uswisi na Austria, mpambano wa jumamosi hii jioni kati ya Ujerumani na Cyprus ni kama ada tu kwa wajerumani.

Kwa mabingwa wa dunia Itali ni mpambano wa kufa kupona kati yake na Scotland.Ujerumani imeshatia kikapuni tiketi yake ya kombe la Ulaya mwezi uliopita tena hata kabla kuaibishwa na jamhuri ya czech walipozabwa mabao 3:0.

Kufuta aibu hiyo waliopakwa na wacheki, kocha wa Ujerumani Joachim Loew ameitaka timu yake kucheza bora zaidi leo hii mjini hannover lakini pia katika mechi yao ya mwisho dhidi ya Wales jumatano ijayo mjini Frankfurt.

Kupigwa kumbo na mapema nje ya kombe lijalo la dunia Afrika kusini 2010 kutazitia timu nyingi uchungu tena kubwa na hata ndogo.

Kinyan’ganyiro cha kanda ya Afrika kinacvhanganya tiketo za finali ya Kombe la dunia na kombe la Afrika la mataifa kwa mwaka huo wa 2010.Hivyo kukosa kushiriki katika mashindano yote 2 kunatia uchungu:

Comoro chini ya mfumo huo inacheza leo mechi yake ya kwanza ya kimataifa katika uwanja wake mjini Moroni na mahasimu wao hawatoki mbali,bali jirani zao Madagaskar.

Katika duru ya kwanza mjini Antananarivo, Comoro ilizabwa mabao 6-2 mwezi uliopita.Leo lakini wanatamba nyumbani na hii ni mara ya kwanza wanacheza mechi ya kimataifa mbele ya mashabiki wao.Kufuta lakini mabao 4 ya duru ya kwanza itakua si rahisi kwa wanagenzi hawa.

Madagascar lakini, ina rekodi mbaya inapocheza n’gambo:Katika mapambano yake 6 ya kombe la dunia,Madagascar iliilaza namibia,ikatoka asuluhu nchini Zimbabwe na kushindw amechi 9 nyengine.

Ilizabwa mabao 23 kwa 8 yake.Chini ya kocha mjerumani Franz Gerber, Madagascar inatumai kurekebisha rekodi hiyo na kutamba leo Moroni.Wangazija watakua na kazi ngumu kuzuwia dharuba kutoka Madagascar.

Mpambano mwengine leo ni kati ya Guinea Bissau na Sierra Leone.Sierra leone ilishinda duru ya kwanza kwa bao 1:0,lakini leo wanacheza Bissau.Jana duru hii ya timu chipukizi za kanda ya afrika kwa kombe lijalo la dunia,ilianza kwa mpambano kati ya jirani 2:Djibouti na Somalia.

Timu 3 za dimba za Afrika zaweza mwishoni mwa wiki hii kukata tiketi zao za kuiwakilisha Afrika katika dimba la Olimpik mjini Beijing,2008:

Simba wa nyika –Cameroun,Black Stars (Ghana) na Tembo wa Corte d’Iviore au Ivory Coast.

Ghana inachuana na mahasimu wao wakubwa Nigeria katika kundi A wakati Ivory Coast inaikaribishja Zambia katika kundi B.Kila moja inahitaji pointi zote kusonga mbele.

Togo iliowakilisha Afrika katika Kombe la dunia hapa Ujerumani mwaka jana, imefungiwa kucheza nyumbani mpambano wake wa kuania tiketi nyengine ya kombe la dunia la 2010.Sababu ni fujo lililozuka ilipocheza nyumbani na Mali.

CAF-shirikisho la dimba la Afrika,limeupiga uwanja wa Togo marufuku kwa mechi 3 na hii ina maana Togo haitakua na nafuu ya kucheza nyumbani katika mapambano yake yote 3.Kura itapigwa Novemba 25 nchini Afrika Kusini.

Stadi wa Senegal El-Hadji Diouf yamkini akarudi kuvaa jazi ya timu ya Taifa Senegal ikichuana na Mali mjini Paris jumamosi.Mchezaji huyo bora wa mwaka wa Afrika mara 2, atahitaji mazowezi makubwa huku Senegal ikijinoa kwa changamoto za Kombe la Afrika la Mataifa litakaloanza Januari mwakani nchini Ghana.

Mapambano mengine jumamosi hii ni kati ya Afrika Kusini na Marekani mjini Johannesberg.Nigeria yaumana na Australia mjini London.Angola yapimana nguvu na Ivory Coast huko Melun,Ufaransa wakati Tunisia inaikaribisha Namibia mjini Tunis.

Chipolopolo –Zambia ina miadi na Taifa Stars mjini Dar-es-salaam hapo Nov.21.

 • Tarehe 16.11.2007
 • Mwandishi Ramadhan Ali
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CImh
 • Tarehe 16.11.2007
 • Mwandishi Ramadhan Ali
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CImh