DFB huenda ikaandaa mkutano maalum | Michezo | DW | 06.11.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

DFB huenda ikaandaa mkutano maalum

Shirikisho la kandanda la Ujerumani – DFB huenda likaandaa mkutano usio wa kawaida wa bodi ya wasimamizi baada ya makao yake mkuu kuvamiwa na polisi.

Hii ilikuja kama sehemu ya uchunguzi unaofanywa kuhusu uwezekano wa kukwepa kulipa kodi na kuhusishwa na Kombe la Dunia la FIFA 2006.

Afisa mmoja wa kandanda amesema anaamini kuwa mkutano maalum huenda ukaandaliwa kabla ya ule uliopangwa kuandaliwa na bodi mwezi ujao. Erwin Bugar, mkuu wa shirikisho la kandanda katika jimbo la mashariki la Saxony-Anhalt, ameiambia radio ya umma ya MDR kuwa yeye na wanachama wengine wa bodi wamesikia ishara kuwa DFB inatafakari kuitisha mkutano. Hata hivyo amesema huenda ikachukua muda kuandaa, kwa vile bodi ya shirikisho hilo inawajumuisha zaidi ya watu 40.

Ofisi ya mwendesha mashtaka mjini Frankfurt imemtambua rais wa sasa wa DFB Wolfsgang Niersbach kama mmoja wa washukiwa watatu inaowalenga katika uchunguzi huo wa kukwepa kulipa kodi. Polisi walivamia makao makuu ya DFB pamoja na makazi ya Niersbach, mtangulizi wake Theo Zwanziger, na aliyekuwa Katibu Mkuu wa DFB Horst R. Schmidt kuhusiana na malipo yaliyotolewa kwa FIFA mnamo mwaka wa 2005 na kamati ya maandalizi ya Kombe la Dunia ya euro milioni 6.7

Ruhy valley derby

Na tukibakia katika kandanda ya hapa Ujerumani ni kuwa mashabiki wanasubiri kwa hamu mchuano mkali wa hapo kesho kati ya nambari mbili kwenye msimamo wa ligi ya Bundesliga Borussia Dortmund dhidi ya nambari nne Schalke katika debi ya Bonde la Ruhr.

Borussia iliwazaba watani wao tatu bila mara ya mwisho timu hizo zilipokutana katika uwanja wa Dortmund wa Westfalenstadion mwezi Februari wakati wenyeji walipofyatua langoni makombora 31 ikilinganishwa na matatu tu ya Schalke.

Hata hivyo Dortmund wanakosa usingizi kuhusiana na hali ya mshambuliaji wao Marco Reus ambaye aliumia katika mchuano wao wa Europa League siku ya Alhamis dhidi ya Qarabag.

Reus alitolewa uwanjani wakati wa kipindi cha mapumziko baada ya kupokea matibabu uwanjani kutokana na maumivu ya paja. Alifunga bao katika ushindi wao wa nne sifuri ambao uliwapa BVB kibai cha kutinga hatua ya mchujo.

London derby

Kocha wa Arsenal Arsene Wenger ana wasiwasi mkubwa kuhusiana na orodha inayoendelea kuwa ndefu ya majeruhi katika timu yake.

Wenger amethibitisha kuwa Hector Bellerin atakosa mchuano wa kesho wa debi ya kaskazini mwa London dhidi ya Tottenham Hotspur, wakati Laurent Koscielny akitiliwa mashaka ikiwa atakuwa amepona kabisa.

Arsenal wana wachezaji kadhaa wa kikosi cha kwanza ambao wako mkekani, wakiwemo beki wa kulia Bellerin na beki wa katikati Koscielny. Alex Oxlade Chamberlain, Theo Walcott na Aaron Ramsy wote wako nje hadi baada ya kipindi cha michuano ya kimataifa wakati Jack Wilshere anatarajiwa kurejea katikati ya Desemba.

Toma Rosciky na Danny Welbeck wanatarajiwa kurejea uwanjani Januari mwakani.

Mapungufu hayo yalionekana wakati Arsenal walizabwa magoli matano kwa moja na Bayern katika Champions League katikati mwa wiki, na Wenger anasema sasa ni wakati wa kujinyanyua tena

Wenger

Naamimi kuwa bila shaka yalikuwa matokeo ya kusikitisha Jumatano usiku lakini kabla ya hapo tulifanya vyema sana katika Premier League na tunataka kuendelea kutoka kinyang'anyiro kimoja hadi kingine. Naami kwa sasa katika Premier League tuna matumaini makubwa na hicho ndio tunataka kuonyesha Jumapili dhidi ya Tottenham. Kawaida, ni derby, na ni mpambano ambao ari na nguvu za kuondoa woga ni muhimu

Kocha wa Spurs Mauricio Pochettino anaamini kuwa timu yake ina upungufu wakati ikijiandaa kwa mchuano huo kwa sababu ilikuwa na siku chache za kupumzika baada ya mchuano wao wa Europa League katikati ya wiki.

Pochettino,

"derby kawaida ni mpambano tofauti. Unahitaji kucheza na moyo wako na hamu. Nafahamu maana yake kwa wafuasi wetu. Yaliyopita sio muhimu kwa namna utacheza mchezo huo. Tuko katika hali nzuri sana. Ni kweli kwamba mpinzani wetu kawaida huwa na faida kwa sababu wana siku moja zaidi ya kujiandaa lakini hatuwezi kulalamika. Tunapaswa kuwa tayari. Tunapaswa kuwa imara kiakili na kujaribu kushinda mchuano huo kwa sababu tunajua ni derby.

Tottenham na Arsenal zitakutana uwanjani Emirates kwa serby yao ya 181 ya upande wa Kaskazini mwa London.

Eto'o azuru Sierra Leone

Mwaka mmoja baada ya FIFA kuzindua kampeni yake ya 11 dhidi ya Ebola, watoto nchini Sierra Leone walikuwa na mgeni maalum. Mshambuliaji wa zamani wa Barcelona na Inter Milan Samuel Eto'o alizuru katika taifa hilo la Afrika Magharibi kuangalia hatua zilizopigwa, tangu kampeni hiyo ilipoanzishwa wakati wa mlipuko wa Ebola. Shirika la Afya Duniani – WHO limetangaza hapo jana kuwa Sierra Leone haina tena virusi vhatari vya Ebola. Nyota huyo wa Cameroon alihimiza umuhimu wa afya nzuri ili kutimiza chohcote kile tunachotaka maishani

Eto'o

Nimezungumza kama kaka mkubwa kwa watoto wanaocheza uwanjani na kuwaamnia: wakati nilikuwa mdogo niliwatazama wachezaji kama vile Roger Milla, George Weah na wengine wengi. Waliniwezesha kuwa na ndoto na kuitimiza ndoto hiyo ambayo ili kuwa ni kucheza kandanda. Naamini nilitimiza ndoto yangu hasa kwa sababu nilitaka kuwa kama hawa watu.

Eto'o, ambaye ana umri wa miaka 34 kwa sasa anachezea klabu ya Uturuki ya Antalyaspor. Amefunga magoli nane katika mechi kumi kufikia sasa msimu huu.

Na wakati Eto'o akiwahimiza vijana kutimiza ndoto zao, ni habari nzuri kwa bara la Afrika, maana timu mbili za bara hilo zimefuzu katika fainali ya dimba la Kombe la Dunia la FIFA kwa wachezaji wa chini ya umri wa miaka 17 linaloendelea nchini Chila.

Fainali hiyo itachezwa Jumapili kati ya Nigeria, ambao ndio mabingwa watetezi, na Mali. Nigeria walifika fainali kwa kuwalaza Mexico 4-2 nao Mali wakawacharaza Ubelgiji 3-1 katika nusu fainali. Nigeria wameshinda dimba hilo mara nne; 1985, 1993, 2007 na 2013.

AJABU!

Wezi waliiba njumu za wachezaji wa klabu ya Sporting Braga kutoka chumba chao cha kubadilishia mavazi wakati wakijiandaa kwa mchuano wao wa Europa League ugenini dhidi ya Olympique Marseille. Klabu ya Marseille ililazimika kununua njumu mpya 46 na hata kujitolea kukodi ndege maalum ya kibinafsi ya kuzileta njumu hizo mpya kutoka Ureno.

Timu hiyo ya Ureno iliacha njumu zao katika chumba chao cha kubadilishia jezi katika uwanja wa Stade Veledrome baada ya kufanya mazoezi Jumatano usiku. Mchuano huo uliendelea ilivyopangwa na wenyeji Marseille wakashinda goli moja kwa sifuri…nadhani Braga hawatadai kwamba kupotea njumu zao ndiko kulisababisha wao kushindwa mchuano huo.

Mwisho wa michezo kwa sasa, kwa mengi zaidi tembelea ukurasa wetu wa michezo utajisomea mengi tu yanayojiri viwanjani, fungua dw.com/Kiswahili. Pia unaweza kuwasiliana nami nitafute kwenye twitter @amanibruce na pia ukurasa wangi wa facebook. Mimi ni Bruce Amani kwaheri.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AP
Mhariri:

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com