Dau la Arsene Wenger litahimili mawimbi? | Michezo | DW | 18.05.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Dau la Arsene Wenger litahimili mawimbi?

Mbivu na mbichi zitajulikana Jumapili nchini England katika ligi kuu na kinyang'anyiro kitakuwa cha kuangalia ni kocha yupi mahiri atakayeshindwa kuipatia timu yake nafasi ya kushiriki ligi ya vilabu bingwa.

Arsene Wenger wa Arsenal ndiye meneja aliye kwenye shinikizo kubwa kwa kuwa timu yake iko nje ya nafasi nne bora na inaingia katika raundi ya mwisho ya mechi kwa kupambana na Everton huku baadhi ya mashabik wakitaka aondoke katika klabu hiyo baada ya miaka 21.

Manchester City na Liverpool wana mustakabali wao wa kusalia miongoni mwa timu nne bora mikononi mwao, kwa kuwa Liverpool watakuwa wanaingia katika mechi yao ya mwisho uwanjani kwao Anfield, dhidi ya Middlesbrough ambao washashushwa daraja, wakiwa alama moja juu ya Arsenal. Manchester City wao watakuwa wanateremka dimbani kucheza na Watford, na City wako alama 3 juu ya Arsenal wakiwa wanaishikilia nafasi ya tatu katika msimamo. Kutokana na hali hiyo, vijana hao wa Pep Guardiola huenda wakatupwa nje ya nne bora iwapo tu, Arsenal watashinda na wao walazwe na Watford, kisha Arsenal wafunge mabao mengi yatakayozidi ile tofauti ya mabao matano iliyoko baina yao na hao The Citizens.

Itakapotokea kwamba timu zote tatu hizo hazitotofautishwa na tofauti ya mabao ama mabao yaliyofungwa, huenda kukaandaliwa mechi moja ya ziada kuamua atakayepata nafasi ya tatu ya moja kwa moja kushiriki ligi ya vilabu bingwa barani Ulaya msimu ujao.

Chelsea wao watakabidhiwa taji la ubingwa baada ya mechi yao na Tottenham Hotspur wao washajihakikishia kumaliza msimu katika nafasi ya pili, hii ikiwa ni mara yao ya kwanza kumaliza katika nafasi hiyo katika kipindi cha miaka 54. Spurs watakuwa wanachuana na Hull City ambao washateremka daraja pamoja na Middlesbrough na Sunderland.

Fussball Englisch Premier League Spiel Chelsea vs Tottenham (picture-alliance/dpa/W. Oliver)

Chelsea tayari washaunyakua ubingwa wa England

Manchester United watamaliza katika nafasi ya 6 ingawa bado wanaweza kupata nafasi ya kushiriki ligi ya vilabu bingwa msimu ujao iwapo wataebuka mabingwa wa ligi ya Ulaya, ambapo watacheza fainali Jumatano tarehe 24 dhidi ya Ajax Amsterdam.

Everton wao wamefuzu kushiriki ligi hiyo ya Ulaya tayari kwa kuwa watamaliza msimu katika nafasi ya 7.

Mwandishi: Jacob Safari/APE

Mhariri: Bruce Amani

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com