Cuba yaadhimisha miaka 60 ya mapinduzi | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.01.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Cuba yaadhimisha miaka 60 ya mapinduzi

Cuba imeadhimisha miaka 60 ya mapinduzi dhidi ya aliyekuwa mtawala wa kiimla Fulgencio Batista huku kiongozi wa chama tawala cha kikomunisti Raul Castro akiwaasa Wacuba kuendelea kuilinda misingi ya mfumo wa kijamaa.

Cuba imeadhimisha miaka 60 ya mapinduzi ya taifa hilo dhidi ya aliyekuwa mtawala wa kiimla, Fulgencio Batista, huku kiongozi wa chama tawala cha kikomunisti, Raul Castro, akiwaasa Wacuba kuendelea kuilinda misingi ya mfumo wa kijamaa licha ya changamoto za kilimwengu na kikanda.

Kwenye hotuba yake ya maadhimisho hayo, Raul Castro - ambaye kwa sasa ni rais mstaafu na pia mwenyekiti wa chama tawala - ameituhumu vikali serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani, kwa kurejea kwenye mipango yake ya kizamani ya kukabiliana na taifa hilo pamoja na uingiliaji wake kwenye eneo la Amerika ya Kusini.

"Kwa kuwa malengo ya kibeberu yamerejeshwa katika ukanda wetu, Wamarekani wanapaswa kuelewa kuwa Amerika ya Kusini na Caribbean zimebadilika, lakini pia ulimwengu. Sisi tutaendelea kushinikiza kikamilifu mchakato wa makubaliano na ushirikiano wa kanda, kulingana na dhana ya umoja katika utangamano." alisema Castro kwenye sehemu ya hotuba yake.

Katika Siku ya Mwaka Mpya ya mwaka 1959, jeshi la kimapinduzi chini ya uongozi wa Fidel Castro pamoja na ndugu yake Raul walifanikiwa kuyaangusha majeshi ya serikali baada ya miaka miwili ya vita vya msituni, na hatimaye mtawala wa kiimla wakati huo, Fulgencio Batista, aliyekuwa akiungwa mkono na Marekani kukimbilia ughaibuni.

Kuba Parlament in Havanna (Imago/Agencia EFE/A. Padrón Padilla)

Mrithi wa Raul Castro, Miguel Diaz-Canel aliliambia bunge kuwepo kwa sera za kikatili na upungufu wa fedha nchini Cuba.

  

Mapinduzi ya Cuba yalisababisha kuibuka kwa vuguvugu la wafuasi wa mrengo wa kushoto kote Amerika ya Kusini, lakini maadhimisho haya yaliyofanyika jana Jumanne, yamekuja katika wakati ambapo ukanda huo unabadilika na kuangazia siasa ya mrengo wa kulia, hasa kwa kuzingatia kuapishwa hapo jana kwa Rais mpya wa Brazil, Jair Bolsonaro, anayeegemea siasa kali za mrengo wa kulia.

Mizozo ya kisiasa na sera kali za mrengo wa kulia vyazidi kushika kasi Amerika ya Kusini.

Washirika wa karibu wa Cuba, Venezuela na Nicaragua, kwa wakati huu wanakabiliwa na mizozo ya kisiasa, na Rais Trump wa Marekani amezidisha vikwazo vya muda mrefu vya Marekani dhidi ya taifa hilo, baada ya mtangulizi wake Barack Obama kutaka suluhu ya kurejesha mahusiano katika hali ya kawaida.

Mshauri wa masuala ya ulinzi wa Rais Trump, John Bolton, alinukuliwa mnamo mwezi Novemba mwaka jana kwamba, Marekani huenda ikachukua mkondo mkali zaidi dhidi ya Cuba, Venezuela na Nicaragua.

Hotuba ya Castro aliyeachia madaraka ya urais mwezi Aprili mwaka jana, lakini akiendelea kusalia kama kiongozi wa chama cha Kikomunisti hadi mwaka 2021, ilikuwa sehemu ya maadhimisho hayo yaliyofanyika kwenye eneo la makaburi ambako kaka yake Fidel Castro na shujaa wa uhuru, Jose Marti, walizikwa.

Kwenye hotuba hiyo, Castro alisema vita vya Cuba kwa mwaka wa 2018 vilikuwa ni vya kiuchumi, na kutofautiana na matamshi yaliyotolewa na mrithi wake, Rais Miguel Diaz-Canel, mbele ya bunge la kitaifa mwishoni mwa mwezi Disemba aliyetangaza kuongezeka kwa sera za kikatili, huku kukiwa na upungufu wa fedha. Castro alisisitizia haja ya kupunguza matumizi yote yasiyo ya msingi na kuwekeza zaidi.

Mwandishi: Lilian Mtono/DPAE/RTRE.

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com