1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

City na Spurs wagawana alama England

19 Agosti 2019

Meneja wa Manchester City Pep Guardiola amelaani muamuzi wa video au VAR katika mechi yao dhidi ya Tottenham Hotspur Jumamosi baada ya maamuzi yake kupelekea mechi yao kuishia sare ya magoli mawili.

https://p.dw.com/p/3O8WR
Manchester City Trainer Pep Guardiola
Picha: picture-alliance/empics/PA Wire/J. Walton

Hii ni baada ya goli la dakika ya mwisho la Gabriel Jesus kukataliwa kwa msingi kwamba Nicolas Otamendi alikuwa ameunawa mpira.

Mechi hiyo ilishia sare ya mabao mawili. Rahee Sterling na Sergio Aguero ndio waliofunga upande wa City na Spurs wakafungiwa na Erik Lamela na Lucas Moura. Huyu hapa Pep Guardiola.

"Tumecheza dhidi ya Tottenham mojawapo ya timu bora Ulaya na tumecheza vizuri sana. Kwa bahati mbaya hatukuweza kushinda. Tumeshindwa kuchukua alama zote dhidi ya Tottenham mara mbili kwasababu ya VAR, msimu uliopita ilikuwa kwasababu mchezaji alidaiwa kaotea, msimu huu ameushika mpira, lakini ndivyo ilivyo. Kuna wakati kulikuwa na kona na Lamela akamparamia Rodri ambaye alianguka lakini wakati huo VAR ilikuwa imekwenda kunywa kahawa," alisema Guardiola.

Nitakubali sheria, sheria ni sheria

Kocha wa Tottenham Mauricio Pochettino lakini hakukubaliana na Guardiola.

UEFA Champions League Finale | Tottenham Hotspur v FC Liverpool
Kocha wa Spurs Mauricio PochettinoPicha: Getty Images/M. Hangst

"Mimi nakubali sheria, nazikubali na nitazikubali hata katika siku za usoni kwasababu ukweli ni kwamba ipo siku ambapo maamuzi yatakwenda dhidi yetu. Na siku hiyo nitayakubali jinsi tu nilivyoyakubali leo. Sheria ni sheria, VAR iko na ni sehemu ya mchezo wa leo," alisema Pochettino.

Katika matokeo mengine ya ligi hiyo ya England Arsenal walipata ushindi wa mbili moja katika mechi ambayo kiungo wao mpya Dani Ceballos aliye kwa mkopo kutoka Real Madrid aling'ara sana. Liverpool walikuwa washindi wa mabao mawili kwa moja pia walipowatembelea Southampton huko Saint Mary's.

Hapo Jumapili Chelsea waliokuwa nyumbani kwao Stamford Bridge waliponea chupuchupu mikononi mwa Leicester walipotoka sare ya bao moja kwa moja.

Usiku wa Jumatatu Manchester United watakuwa wanaelekea uwanjani Molineux kupambana na Wolverhampton Wanderers waliowapa shida mno msimu uliopita.