Chuki dhidi ya waandishi wa habari yageuka kuwa vurugu | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.04.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Chuki dhidi ya waandishi wa habari yageuka kuwa vurugu

Ripoti ya kila mwaka ya shirika la waandishi wa habari wasio na mipaka RSF, imeonya kuwa chuki dhidi ya waandishi wa habari inayochochewa na viongozi wa mirengo mikali na wa kiimla imegeuka kuwa vurugu kote ulimwenguni. 

Ripoti ya mwaka huu ya shirika la waandishi wa habari wasio na mipaka kuhusu faharasi ya uhuru wa vyombo vya habari inasema chuki dhidi ya waandishi inayosambazwa na wanasiasa "imesababisha ongezeko la vitendo vya vurugu, kiwango cha hofu na hatari dhidi ya waandishi wa habari".

Ripoti hiyo inasema "hali ya uadui katika kauli za rais Donald Trump" dhidi ya waandishi imechangia Marekani kuporomoka hadi nafasi ya 48. Ripoti hiyo inasema kuliko wakati wowote waandishi wa habari nchini humo "wamekuwa na vitisho vingi" na kukimbilia makampuni binafsi ya usalama kwa ajili ya ulinzi. Mshambuliaji mmoja aliingia chumba cha habari katika gazeti la Capital katika jimbo la Maryland Marekani na kuwaua waandishi wa habari wanne mwaka uliopita.

Kupungua kwa uhuru wa vyombo vya habari pia kumeshuhudiwa Afrika. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, "waandishi wa habari wameshambuliwa" nchini Tanzania tangu rais John Magufuli alipoingia madarakani. Taifa hilo limeshuka kwa nafasi 25 katika viwango hivyo.

Azory Gwanda - Journalist (Mwananchi Communications Limited (MCL) in Tanzania (Privat)

Mwandishi wa habari wa Tanzania Azory Gwanda aliyetoweka mazingira ya kutatanisha

Kuuawa kwa mwandishi wa habari Jamal Khashoggi katika ubalozi wa Saudi Arabia mjini Istanbul pia "kulituma ujumbe mkali kwa waandishi wa habari nje ya mipaka ya Saudia". Katika nchi nyingine vitisho, matusi na mashambulizi vimekuwa ni hatari ya kazi, imesema ripoti hiyo.

India ambayo imeshika nafasi ya 140 ilishuhudia waandishi wa habari sita wakiuawa mwaka jana na Brazil iliyoko nambari 105 maripota wamekuwa wakilengwa na wafuasi wa rais wa nchi hiyo, Jair Bolsonaro. Norway imekuwa kinara wa uhuru wa vyombo vya habari kwa mwaka wa tatu mfululizo wakati Finland ikishika nafasi ya pili na Sweden iko nafasi ya tatu. Uturuki ni miongoni mwa nchi zilizo katika hali mbaya ya uhuru wa waandishi.

Shirika hilo la waandishi wa habari wasio na mipaka pia limeorodhesha idadi ya matukio ya kukamatwa na visa vya vurugu vilivyofanywa na mamlaka ya Venezuela ambapo waandishi kadhaa waliikimbia nchi kuepuka kuadhibiwa. Nchi ya Turkmenistan iliyoko Asia ya kati imekamata nafasi ya mwisho na kuiondoa Korea Kaskazini.  Hata hivyo kulishuhudiwa maendeleo kwa baadhi ya nchi, Ethiopia kwa mfano imepanda kwa nafasi 40 chini ya utawala wa waziri mkuu Abiy Ahmed, huku Gambia ikiendelea kuimarika sambamba na Angola.

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com