China yaondowa maelfu ya raia wake Vietnam | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.05.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

China yaondowa maelfu ya raia wake Vietnam

Vikosi vya usalama vimewekwa katika miji mikubwa Vietnam kuzima maandamano mapya yaliochochewa na utafiti wa kuchimba mafuta wa China katika eneo la bahari lenye mzozo wakati China ikiwaondoa maelfu ya raia wake Vietnam.

Waandamanaji mjini Hanoi.

Waandamanaji mjini Hanoi.

Shirika la habari la serikali nchini China limesema zaidi ya raia wake 3,000 tayari wamerudi nyumbani katika siku za hivi karibuni baada ya mvutano wa kuwania eneo la Bahari ya China Kusini kati ya nchi hizo mbili kuzusha maandamano yaliosababisha vifo wiki iliopita na kuuweka uhusiano wa nchi hizo katika hali mbaya kabisa kuwahi kushuhudiwa kwa miongo mingi.

Makundi ya watu yenye hasira wiki iliopita yalitia moto au kuharibu mamia ya shughuli za kibiashara zenye kumilikiwa na wageni na kuwauwa Wachina wawili na kuwajeruhi wengine 140.

Wakati uwekaji wa jukwaa kubwa la utafiti wa kuchimba mafuta uliofanywa na China katika eneo hilo la mzozo umeonekana kama ni kitendo cha uchokozi mkubwa,kuchemka kwa ghadhabu hiyo ya wananchi kumeishtukiza serikali ya nchi hiyo.

Ikihofia taathira kwa uwekezaji ambao ni muhimu nchini Vietnam,serikali imechukuwa tahadhari kubwa wakati makundi ya wanaharakati yalipojaribu kufanya maandamano zaidi juu ya kwamba walisisitiza kuwa yatakuwa ya amani.

Jengo la viwanda likiteketea katika jimbo la Binh Duong nchini Vietnam.

Jengo la viwanda likiteketea katika jimbo la Binh Duong nchini Vietnam.

Mamia ya askari wa usalama Jumapili (18.05.2014) wamemwagwa katika mitaa yenye kuelekea katika eneo kubwa uliko ubalozi wa China mjini Hanoi na kuzuwiya watu kufikia kiunga hicho na maeneo mengine yanayoshukiwa kufanyika maandamano.

Mablogu ya makundi ya kijamii yaliohusika katika maandamano hayo yamesema wanaharakati wamekamatwa katika meneo mbali mbali nchini humo au wamezuiliwa kuondoka majumbani mwao.

Shughuli za ushikiano zasitishwa

Shirika la habari la China Xinhua limesema raia wa China waliorudishwa nyumbani ni pamoja na watu 135 waliojeruhiwa katika vurugu za Jumanne na Jumatano iliopita wakiwemo 16 ambao ni mahtuti.

China pia imesema kwamba inatuma meli tano kuwarudisha nyumbani raia wake zaidi na itasitisha baadhi ya shughuli za ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.

Taarifa ya wizara ya mambo ya nje imesema ghasia za hivi karibuni zinaharibu mazingira na hali ya mabadilishano na ushirikiano baina ya nchi hizo.

Waandamanaji wakiingia kiwandani katika jimbo la Binh Duong nchini Vietnam.

Waandamanaji wakiingia kiwandani katika jimbo la Binh Duong nchini Vietnam.

"Upande wa China kuanzia leo unasitisha sehemu ya mipango yake ya mabadilishano" imesema taarifa hiyo bila ya kufafanuwa mipango hiyo na kuongeza kusema "China itaangalia jinsi hali hiyo inavyoendelea na kuona hatua itakazochukuwa zaidi."

Hapo awali China iliwaonya raia wake dhidi ya kwenda Vietnam kufuatia kile ilichokiita "mripuko wa ghasia" na kuwahimiza wale ambao bado wangalipo nchini Vietnam kuchukuwa hatua za tahadhari zaidi.

Mzozo wa kuwekwa kwa jukwaa hilo la utafiti wa kuchimba mafuta kumezidi kuutia sumu uhusiano kati ya nchi hizo mbili ambapo huko nyuma ziliwahi kucharuana na kuzidi kutofautiana kutokana na madai yao ya eneo la Bahari ya China Kusini.

Kwa mujibu wa serikali wiki iliopita wafanyakazi waliandamana katika majimbo 22 kati ya 63 nchini Vietnam , wakati makundi ya watu yenye ghadhabu yakivitia moto viwanda na kampuni zinazomilikiwa na wageni zinazoaminika kuwa na mafungamano na China au zenye kuwaajiri wafanyakazi wa Kichina.

China imekuwa ikishutumiwa sana nchini Vietnam kwa tabia yake ya maonevu iliokuwa nayo kwa zaidi ya miaka 1,000 na serikali ya kikomunisti ya Vietnam mara moja moja huwaachilia waandamanaji kudhihirisha ghadhabu zao.

Udhibiti wa athari

Waandamanji mjini Hanoi.

Waandamanji mjini Hanoi.

Kuchemka kwa ghadhabu kwa hivi karibuni kumepelekea serikali ya Vietnam kuchukuwa hatua ya kupunguza taathira kwa uchumi wake unaokuwa wenye kutegemea uwekezaji wa kigeni.

"Hatutoruhusu vitendo vyo vyote vyenye kulenga wawekezaji wa kigeni,makampuni au watu binafsi ili kuhakikisha kwamba matukio hayo ya kusikitisha hayarudiwi tena",Dang Minh msaidizi waziri wa mambo ya nje wa Vietnam amewaambia waandishi wa habari hapo jana.

Amezitaka nchi ziendelee kuwashajiisha wawekezaji na raia wao kutokuwa na wasi wasi kufanya biashara nchini Vietnam.

Serikali ya Vietnam imesema zaidi ya watu 300 wanaoshukiwa kuhusika katika ghasia hizo wametiwa mbaroni.

Kwa mujibu wa takwimu za serikali soko kubwa sana la ajira la wafanya kazi wanaolipwa ujira mdogo nchini Vietnam mwaka 2013 lilivutia uwekezaji wa kigeni wa moja kwa moja wenye thamani ya dola bilioni 21.6 wakati mwaka uliotangulia huo uwekezaji huo ulikuwa na thamani ya dola bilioni 16.3.

Wachambuzi wanasema matukio hayo ya karibuni yanaweza kuwa na athari ya muda mrefu kwa taswira yake kama nchi yenye usalama kwa uwekezaji.

Miongoni mwa makampuni yaliolengwa wakati wa ghasia hizo ni ya China,Taiwan,Korea Kusini na Singapore.

China ambayo imegoma kuliondowa jukwaa lake hilo la utafiti wa kuchimba mafuta la Haiyang Shiyou imekuwa ikishutumiwa wazi wazi kwa hatua yake hiyo hasa kwa kuzingatia kuongezeka kwa mvutano katika eneo hilo la Bahari ya China Kusini ambapo Marekani imeita kuwa uchokozi.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/Reuters

Mhariri : Caro Robi

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com