Chelsea yataka kufanya kweli Europa League
14 Februari 2013Timu tatu za Ujerumani, Borussia Moenchengladbach, VFB Stuttgart na Bayer Leverkusen zitaingia uwanjani pia leo jioni kuwania kufuzu kuingia katika kundi la timu 18 zitakazosalia.
Chelsea imekuwa timu ya kwanza bingwa kutolewa katika awamu ya makundi ya Champions League na inakabiliwa na mpambano katika kundi la timu 32 zilizosalia katika kinyang'anyiro cha ligi ya Ulaya na ina miadi jioni ya leo na Sparta Prague.
Hawataki wachezaji mashoga
Liverpool wako nchini Urusi huku mashabiki wa timu ya Zenit mwezi Desemba walitoa wito kwa klabu yao kutowasajili wachezaji ambao si wazungu na ama ambao ni mashoga, na mkurugenzi mtendaji wa klabu hiyo Ian Ayre amesema katika tovuti ya klabu hiyo kuwa timu yake imeeleza wasi wasi wake katika barua iliyotumwa kwa shirikisho la kandanda barani Ulaya , UEFA na pia klabu ya Zenit St. Petersburg.
"Limekuwa suala kuu la kutia wasi wasi kwetu. Tunasubiri jibu kuhusiana na hilo," amesema.
Kocha wa Liverpool Brendan Rodgers atateremsha uwanjani kikosi madhubuti kabisa mjini St Petersburg, akimwacha kando mchezaji aliyejiunga na kikosi hicho hivi karibuni Daniel Sturridge na Philippe Coutinho, ambao wanafungwa na sheria kutokuwamo katika orodha ya wachezaji wa kikosi hicho.
Nahodha wa Chelsea John Terry amesema kuwa kikosi chake kinaichukulia ligi ya Ulaya kwa dhati hata kama ni kama tukio la ligi ya pili.
"Hivi sasa tumo katika Ligi ya Ulaya na kuna ujumbe mmoja tu hapa- tunataka kwenda katika ligi hiyo na kushinda . Hilo ndio lengo letu," amesema Terry.
Cech anacheza kwao
Mlinda mlango Petr Cech anacheza nchini mwake na dhidi ya klabu ambayo aliichezea mwaka 2001-02 , na anafahamu kuwa wenyeji watakuwa moto wa kuotea kwa mbali.
"Kwao wao utakuwa mchezo mkubwa mno katika wakati wao, kwa hiyo hiyo ndio hatari kwasababu watataka kuonyesha kuwa wanaweza kufanya vizuri dhidi yetu", amesema Cech, na kuongeza kuwa Sparta ina mchanganyiko mzuri wa vijana , wachezaji wenye uchu na wale wenye uzoefu.
Mabingwa watetezi Atletico Madrid pia wanakabiliwa na upinzani kutoka Urusi, Rubin Kazan, na mlinda mlango wao Sergio Asenjo, ana wasi wasi mkubwa na mshambuliaji mrefu wa Kazan , Jose Rondon.
Mabingwa wa zamani Inter Milan wana miadi na timu kutoka mashariki ya Ulaya , Cluj kutoka Romania.
Timu za Bundesliga
Borussia Moenchengladbach inapambana jioni ya leo na Lazio Rome ambayo itamkosa mshambuliaji wake kutoka Ujerumani Mil´roslav Klose, pamoja na nahodha Stefano Mauri.
Hannover 96 inakutana na kikosi kinachoongozwa na mshambuliaji kutoka Cameroon , Eto'o , VFB Stuttgart ina kabiliana na Genk ya Ubeljigi wakati Bayer Leverkusen inaikaribisha Benfica Lisbon ya Ureno.
Mwandishi : Sekione Kitojo / dpae
Mhariri: Josephat Charo