CAR, makundi 14 ya waasi wafikia makubaliano ya amani | Matukio ya Afrika | DW | 03.02.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

CAR, makundi 14 ya waasi wafikia makubaliano ya amani

Makubaliano ya amani yamefikiwa kati ya serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na makundi 14 ya waasi kufuatia mazungumzo ya ana kwa ana ya siku tano. UN na AU zimetangaza kufikiwa kwa makubaliano hayo siku ya Jumamosi.

Makubaliano hayo ya amani yanawakilisha matumaini ya nadra kwa taifa hilo maskini na lisilo na njia ya bahari, ambako mapigano ya kidini na kikabila yameendelea tangu 2013.

Maelfu ya watu wameuawa na mamia kwa maelfu wamepoteza makazi yako katika mgogoro uliowapeleka watu wawili kwenye mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC.

"Nimedhamiria kufanya kazi na rais na serikali yake kushughulikia wasiwasi wa ndugu zetu walioamuka kuchukuwa silaha na kuanza kupigana," alisema mkurugenzi wa baraza la mawaziri la Jamhuri ya Afrika ya Kati Firmin Ngrebada, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Pande hizo zitasaini rasimu ya makubaliano Jumapili hii, ambayo yanajikita kwenye ugawanaji wa madaraka na kipindi cha mpito cha utoaji haki, viliripoti vyombo vya habari vya serikali ya Sudan, vikimnukuu mpatanishi mkuu Atta al Manan.

Makubaliano ya mwisho yanatarajiwa kusainiwa siku ya Jumatano. Mazungumzo yalianza Januari 24 mjini Khartoum. " Hii ni siku kubwa kwa Jamhuri ya Afrika ya Kati na watu wake wote," alisema Kamishna wa Umoja wa Afrika kwa ajili ya amani na usalama, Smail Chergui.

Zentralafrikanische Republik Kaga Bandoro Flüchtlingscamp (picture-alliance/AP Photo/D. Belluz)

Mamia kwa maelfu ya raia wamegeuka wakimbizi kufuatia vurugu za makundi ya silaha katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Hatari ya mauaji ya kimbari

Mapigano yalibeba hatari kubwa ya mauaji ya kimbari, Umoja wa Mataifa umeonya. Mgogoro huo ulianza 2013 wakati waasi wa kundi la Seleka, ambao wengi wao walikuwa Waislamu, walipotwaa madaraka katika mji mkuu Bangui.

Wapiganaji wa kundi la Anti-Balaka, ambao wengi wao walikuwa Wakristo wakampabana nao. Misikiti kadhaa ilichomwa moto. Waislamu wengi wameikimbia nchi hiyo baada ya makundu kuwachinja na kuwakata viungo wenzao katika mitaa ya nchi hiyo.

Mapigano ya mzunguko katika taifa linalojulikana kwa mapinduzi kuliko vurugu za kidini yalikuwa yanastua kiasi kwamba Papa Francis alifanya ziara ya kijasiri mwaka 2015, akivua viatu vyake na kuinamisha kichwa chake katika msikiti mkuu katika eneo lililosalia la Waislamu katika mji mkuu Bangui.

"Kwa pamoja tusema 'hapana' kwa chuki," alisema Papa. Vurugu hizo hazijawahi kutoweka, na ziliongezeka na kusambaa mwaka uliopita baada ya kipindi cha utulivu kiasi wakati ambapo makundi ya waasi yakipambana kudhibiti ardhi yenye utajiri wamadini ya dhahabu, almasi na urani.

UN, serikali wakiri udhaifu

Baada ya zaidi ya watu 40 kuuawa katika shambulio la waasi dhidi ya kambi ya watu waliopoteza makaazi yao mwezi Novemba, wote, kiongozi wa ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wenye jumla ya wanajeshi 13,000 na waziri mkuu wa taifa hilo walikiri kuwepo na udhaidu katika uitikiaji wa shambulio hilo.

Straßenszene in Bangui (picture alliance/AP Images)

Vurugu za miaka mitano zimesababisha uharibifu mkubwa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

"Nilijua kwamba hatukuwa na njia stahiki kuwalinda watu wetu," alisema waziri mkuu. Katika ya kutisha mwaka uliopita kukumbuka miaka mitano ya mgogoro huo, shirika la watoto la Umoja wa Mataifa lilisema wapiganaji huwalenga raia mara kwa mara kuliko wenyewe kwa wenyewe, wakishambulia vituo vya afya na shule, misikiti na makanisa na kambi za watu waliokosa makaazi.

Idadi isiyopungua nusu ya watu 640,000 waliokosa makaazi yao ni watoto, ilisema UNICEF, na kuongeza kuwa malefu wanaaminika kujiunga na makundi ya silaha, mara nyingi chini ya shinikizo.

Sehemu kubwa ya raia milioni 2.9 wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu, lilisema shirika hilo. Siku ya Alhamisi, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipiga kura kurefusha vikwazo vya silaha dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa mwaka mmoja lakini liliweka uwezekano wa kuondoa vikwazo hivyo mapema kama serikali imwekuwa ikiomba.

mwandishi: Iddi Ssessanga/ape

Mhariri: Caro Robi