1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cameroon yafungua mjadala wa kumaliza mgogoro

Angela Mdungu
30 Septemba 2019

Cameroon inaanza mdahalo wa kitaifa hii leo, ikiwa ni juhudi za kumaliza mgogoro wa wanaotaka kujitenga katika mikoa yenye wakazi wanaozungumza lugha ya Kiingereza.

https://p.dw.com/p/3QTfA
Kamerun Präsident Paul Biya
Picha: picture-alliance/AP Photo/Lintao Zhang

Mjadala huo unaofanyika mjini Yaounde, unaanza huku viongozi muhimu wa upande wa waasi wakiwa tayari wamekataa kushiriki.

Majadiliano hayo ya kutaka kumaliza mgogoro nchini Cameroon, yanayoongozwa na Waziri mkuu Joseph Dion Ngute, yamepangwa kuanza leo Septemba 30 hadi tarehe 4 mwezi Oktoba. Rais wa nchi hiyo Paul Biya ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 37, anatumaini mazungumzo hayo yatamaliza mgogoro  ambao  umekuwa ukiuathiri uchumi wa nchi hiyo, unaotegemea zaidi uzalishaji wa Kahawa na cocoa.

Kiongozi wa wanaotaka kujitenga Mark Bareta, ni mmoja wa watu waliotaka mjadala lakini alitangaza kujitoa siku ya Ijumaa. Wakati anajitoa Bareta alisema njia pekee ya kuwa na mazungumzo ya kweli ni kuyafanya katika eneo lisiloegemea upande wowote.

Viongozi wa makundi ya uasi wazidi kujitoa

Kiongozi mwingine wa kundi la wapiganaji Ebenezer Akwanga ambaye pia amejitoa amesema tukio hilo ni sawa na kujionesha kwa jumuiya ya kimataifa na si juhudi za kutaka kupata suluhisho la kudumu kwa raia wa Kusini mwa nchi hiyo na  Cameroon kwa ujumla.

Zaidi ya watu 3,000 wamekufa na wengine nusu milioni wameyakimbia makazi yao, tangu kuanza kwa mapigano mnamo mwaka 2017. Mapigano hayo ni kati ya jeshi na wapiganaji wanaotaka uhuru wa mikoa miwili inakozungumzwa  lugha ya kiingereza.

Kamerun | Unterstützer anglophoner Aktivisten aus Gefängnis entlassen
Wanausalama wakiwa wamesimama wakati wa kuachiliwa wanaharakati wa wazungumzaji wa lugha ya Kiingereza, mjini Yaounde, Agosti 2018 Picha: Reuters/Stringer

Hata hivyo hata kabla ya kuanza, mjadala huo wa kitaifa nchini Cameroon umekumbwa na matatizo kwani wanaharakati wengi wamekamatwa na polisi huku wataalamu wakisema utaleta matokeo yanayoonekana. 

Mwezi Januari mwaka  2017 Wanaharakati wa ngazi ya juu walikamatwa wakituhumiwa kwa  ugaidi na uasi. Rais Paul Biya alisimamisha kusikilizwa kwa kesi zao mwezi Agosti kwa madai ya kutuliza hali.

Kati ya kila raia 5 wa Cameroon  mmoja anazungumza kiingereza kati ya jumla ya  raia 24 milioni wa nchi hiyo. Watumiaji hao wa Kiingereza, wanapatikana zaidi katika Mkoa wa Kaskazini Magharibi na Kusini Magharibi ambayo ilijumuishwa katika nchi hiyo inayotumia lugha ya Kifaransa baada ya kipindi cha Ukoloni barani Afrika zaidi ya miaka 60 iliyopita. Wengi wa wenyeji wa maeneo hayo, wamekuwa wakilalamika kubaguliwa na kukandamizwa.