1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Côte d'Ivoire kunatokota

Oumilkher Hamidou15 Februari 2010

Upande wa upinzani wawataka wananchi wateremke majiani kupinga utawala wa rais Laurent Gbagbo aliyeivunja serikali na tume ya uchaguzi

https://p.dw.com/p/M1NF
Rais Laurent GbagboPicha: AP

Waziri mkuu wa Côte d'Ivoire Guillaume Soro,hatounda serikali mpya hadi leo usiku kama alivyotakiwa na rais Laurent Gbagbo alipotangaza kuivunja serikali na tume ya uchaguzi nchini humo.Viongozi wa upande wa upinzani nchini Côte d'Ivoire wamelaani uamuzi huo na kusema hawamtambui tena Laurent Gbagbo kama rais.

Laurent Gbagbo ametangaza kuzivunja taasisi hizo mbili ijumaa iliyopita kufuatia mvutano pamoja na tume ya uchaguzi kuhusu kuandikishwa wapigaji kura.

Laurent Gbagbo anamtuhumu mkuu wa tume ya uchaguzi,Robert Mambé,ambae ni wa kutoka upande wa upinzani,kuongeza majina ya watu laki nne na 29 elfu katika orodha za wapiga kura na ambao hawajathibitishwa bado kama ni raia wa Côte d'Ivoire.

Waziri mkuu Guillaume Sorro anakabiliwa na kazi ngumu ya kuunda serikali mpya.Viongozi wa upande wa upinzani wameshasema hawamtambui tena Laurent Gbagbo kama rais wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

"Sijui waziri mkuu atakua tayari lini,lakini sio kabla ya jumanne-ni mapema mno na hali ni tete pia kwa sasa kuweza kupitisha uamuzi haraka haraka."amesema hayo mshauri mmoja wa waziri mkuu Guillaume Soro ambae hakutaka jina lake litajwe.

Uamuzi wa rais Laurent Gbagbo utasababisha kucheleweshwa kwa mara nyengine tena uchaguzi wa rais ambao kimsingi ulikua uitishwe mwishoni mwa mwezi huu au mapema mwezi ujao wa March.

Uchaguzi huo wa rais ni muhimu ili kumaliza vurugu la kisiasa linaloigubika nchi hiyo iliyokumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2002-2003-na kuigawa sehemu mbili nchi hiyo inayoongoza katika biashara ya kakao ulimwenguni.

Wagombea wa upande wa upinzani,Henri Konan Bédié na Alassane Ouattara wanamtuhumu rais Gbagbo kubuni vizingiti ili kuchelewesha makusudi uchaguzi wa rais.

Wananchi wameingiwa na hofu baada ya upande wa upinzani kutoa mwito wa maandamano kote nchini humo.

Präsidentenwahl an der Elfenbeinküste Flash-Galerie
Mgombea pekee wa kike wa uchaguzi wa rais Jacqueline Loés Oble nchini Côte d'IvoirePicha: DW/ Adayé

Msemaji wa vugu vugu la vijana wanaompinga rais Gbagbo ,Kouadio Konan Bertin anasema:

""Nnawaambia wananchi na vijana wa Cote d'Ivoire:tangu miaka kumi sasa,hatufanyi chochote.Tutakodowa macho mpaka lini?Nchi yetu inaangamia.Nani aliyefikiria kua itafika siku hatutakua na umeme?Nani aliyefikiria itafika siku tutakua na uhaba wa maji nchini Cote d'Ivoire?Wakati umewadia sasa wa kuchukua hatua za kumng'owa madarakani Laurent Gbagbo.Ni mwito huu na tunawataka vijana wote wateremke majiani kuelezea machungu yao na kuchonga njia itakayoikomboa Cote d'Ivoire."

Wakati huo huo waziri mkuu Guillaume Sorro anaendelea kushauriana na upande wa upinzani.Baada ya kuzungumza na Henri Konan Bedie jana,hii leo anapanga kuzungumza na muakilishi maalum wa katibu mkuu wa umoja wa mataifa nchini Cote d'Ivoire Young-jin Choi, wakuu wa chama cha umma FPI-cha rais Gbagbo na wale wa muungano kwaajili ya demokrasia na amani RHDP-chama cha rais wa zamani wa Cote dIVoire,Houphouet Boigny.

Mwandishi:Hamidou,Oummilkheir /AFP/Reuters

Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed