BVB yazidi kuchanja mbuga Bundesliga | Michezo | DW | 14.09.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

BVB yazidi kuchanja mbuga Bundesliga

Katika Bundesliga , Borussia Dortmund yaendelea kuogelea katika bahari ya ushindi, wakati Bayern Munich yashinda dhidi ya Augsburg kwa goli linalolalamikiwa mno.

Fußball Bundesliga 4. Spieltag Hannover 96 - Borussia Dortmund

Wachezaji wa Borussia Dortmund wakishangiria bao

Kwa ushindi wa kwanza nyumbani chini ya ukufunzi wa kocha Andre Breitenreiter FC Schalke 04 imeweza kuleta maelewano kiasi na mashabiki wake na kujupa katika msimamo wa ligi hadi nafasi ya tano ikiwa na pointi saba kutokana na michezo minne.

Schalke 04 Jumapili(13.09.2015) ilifanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-1 nyumbani dhidi ya Mainz 05 baada ya kutofanya vizuri katika michezo yake mitatu ya nyuma.Kocha wa Schalke 04 Andre Breitenreiter amesema timu yake jana ilionesha uhai.

Fußball Bundesliga 4. Spieltag FC Schalke 04 FSV Mainz 05

Schalke 04 wakishangiria bao dhidi ya Mainz 05

"Katika dakika 30 za mwanzo tulionesha uwezo mkubwa, katika kujituma , kwenda mbio, ari , na umakini , kila kitu kilikuwapo. Kwa hiyo mchezo wetu kuanzia mwanzo ulikuwa mzuri sana, na ndio sababu tuliweza kupata nafasi nyingi golini, ambazo kwa bahati mbaya hatukuweza kuzitumia. Nafikiri tunakubaliana kwa pamoja , kwamba kwa mchezo huu tulipaswa kumaliza kazi katika kipindi cha kwanza."

Katika mchezo wa kwanza hata hivyo jana werder Bremen iliipiga mwereka Hoffenheim kwa mabao 3-1 ambapo katika mchezo wake wa kwanza tangu kurejea katika kikosi hicho Claudio Pizarro alisaidia katika ushindi huo.

"Jana nilifanya mazowezi zaidi kuliko wenzangu , kwasababu ninahitaji zaidi kufanyia kazi hali ya mwili wangu. Nilifikiri naweza kucheza kwa muda mrefu kidogo. Lakini nahisi , dakika hizi kumi zilikuwa sawa. Na wote tumefurahi, kwamba tumeshinda."

Fußball Bundesliga 4. Spieltag TSG 1899 Hoffenheim SV Werder Bremen

Claudio Pizarro akimpongeza Anthony Ujah baada ya kufunga bao kwa basi kutoka kwake

Mabingwa watetezi Bayern Munich waliponea chupu chupu kuangukia pua baada ya kupata ushindi wa kibahati wa mabao 2-1 dhidi ya Augsburg , ambapo mabingwa hao walipata bao la ushindi kwa njia ya penalti ambayo haikuwa halali kwa mujibu wa kocha wa Augsburg Markus Weinziel.

"Nijisikia fahari kwa kikosi changu, kwa vile tulivyocheza leo ilikuwa vizuri sana. Kwa muda wa dakika 90 tuliweza kulinda lango letu vizuri. Nafikiri tulijipanga vizuri. Si rahisi kuizuwia Bayern kwa muda wa dakika 90. Tulipata bao la kuongoza na katika kipindi cha pili mbinyo ulikuwa mkubwa zaidi. Bao la kusawazisha la Bayern lilikuwa sawa, lakini katika dakika 90 kupigiwa penalti , nahisi kila mmoja ameona."

Borussia Dortmund imeanza msimu huu kwa kishindo baada ya kupata ushindi katika michezo yake yote minne, ambapo siku ya Jumamosi iliiporomosha Hannover 96 kwa mabao 4-2 na kuongoza msimamo wa ligi hiyo kwa wiki ya pili mfululizo. Nahodha wa Dortmund Mats Hummels anasema kila timu msimu huu ni ngumu.

Fußball Bundesliga 4. Spieltag Hannover 96 - Borussia Dortmund

Pierre-Emerick Aubameyang wa Borussia Dortmund

"Kila timu katika Bundesliga ni ngumu, kuweza kuishinda. Tulifahamu kwamba nyumbani kwa Hannover haingekuwa rahisi , na hii hutokea kwa nadra sana. Na kutokana na hilo tulijipanga na kuweza kupambana. Tumefungwa mabao mawili, lakini tulijipanga kucheza mchezo wa kushambulia zaidi na kwa hivi sasa tunacheza kandanda safi na tuna bahati ya kufunga mabao mengi."

Bayer Leverkusen hata hivyo ilipokea kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa SV Damstadt timu iliyopanda daraja msimu huu, wakati makamu bingwa Wolfsburg ilitoshana sare na timu nyingine iliyopanda daraja msimu huu Ingolstadt bila kufungana.

Masaibu ya Borussia Moenchengladbach na VFB Stuttgart hayajapatiwa ufumbuzi hadi katika mchezo wa nne wa Bundesliga, baada ya timu hizo kupokea tena kipigo, ambapo Hertha BSC Berlin iliilaza VFB Stuttgart kwa mabao 2-1 na Hamburg SV iliichapa Borussia Moenchengladbach kwa mabao 3-0. FC Kolon iligaragazwa na Frankfurt kwa mabao 6-2.

La Liga

Kwingineko katika bara la Ulaya lionel Messi aliingia uwanjani akitokea katika benchi la Barcelona na kuwasaidia mabingwa hao watetezi kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Atletico Madrid siku ya Jumamosi wakati Cristiano Ronaldo , CR7 alipachika wavuni mabao matano katika ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Espanyol.

Viongozi wa ligi ya Uingereza Manchester City ilihitaji bao la mchezaji wa akiba Kelechi Iheanacho kuweza kuishinda Crystal Palace kwa bao 1-0 , lakini mabingwa watetezi Chelsea iliangukia pua kwa mara nyingine tena pale ilipopata kipigo cha mabao 3-1 dhidi ya Everton.

Manchester United iliishinda Liverpool kwa mabao 3-1 pia kijana chipukizi kutoka Ufaransa Anthony Martial akipachika bao katika mchezo wake wa kwanza na mashetani hao wekundu.

All Africa Games

Mashindano ya All Africa games yanaendelea mjini Brazzaville, ambapo katika kandanda mwishoni mwa juma Zimbabwe iliishinda Congo Brazzaville kwa bao 1-0 na Burkina Faso ilitoka sare bila kufungana na Sudan.

Burkna Faso imepata fursa ya kuingia katika nusu fainali ya michezo hiyo ya All Africa Games kwa kurusha shilingi na kuishinda Sudan na itapambana na washindi wa kundi B Nigeria. Burkina Faso na Sudan zilikuwa zimefungana kwa pointi, na mabao ya kufunga na kufungwa nyuma ya washindi wa kundi A wenyeji Congo Brazzaville.

Congo itapambana na washindi wa pili wa kundi B Senegal katika nusu fainali nyingine zote zitafanyika kesho mjini Brazzaville.

Champions League barani Afrika

Na katika michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika , Zamalek iliichambua Orlando Pirates ya Afrika kusini kwa mabao 4-1 jana Jumapili na kuweka matumaini hai ya kukutana na mahasimu wao wa jadi mabingwa wa kombe hilo Al-Ahly katika fainali.

Al-Ahly iliipiku Etoile Sahel ya Tunisia kwa wingi wa magoli baada ya kila timu kupata pointi 13 katika kundi A ikifuatiwa na Stade Malien ya mali na Esperance pia ya Tunisia ikishika nafasi ya nne.

Zamalek itacheza na Etoile Sahel ya Tunisia katika nusu fainali wakati Pirates itakumbana na Al_ahly katika marudio ya fainali ya mwaka 2013 ya Champions League ambapo Wamisri walishinda. Timu hizo za Misri zikishinda katika nujsu fainali zitakutana katika fainali kwa mara ya kwanza.

Champions League barani Ulaya

Champions League katika bara la Ulaya inaanza rasmi kesho Junamme katika awamu ya makundi, ambapo Sevilla ya Uhispania itaoneshana kazi na Borussia Moenchengladbach kesho Jumanne wakati timu zote hizo bado zinasaka ushindi wa kwanza katika ligi zao msimu huu.

Georgien Super-Cup Finale FC Barcelona gegen FC Sevilla

Lionel Messi wa Barcelona

Sevilla imepata pointi mbili tu msimu huu hadi sasa katika La Liga na katika Bundesliga Moenchengladbach haijaambulia kitu baada ya kushindwa katika michezo yake yote minne.

Lakini historia itaandikwa upya kesho wakati VFL Wolfsburg itakaporekea katika medani ya Champions League, dhidi ya CSKA Moscow, kufuatia kukaa nje ya kinyang'anyiro hicho kwa muda wa miaka sita.

England Chelsea Meister Jubel

Kocha wa FC Chelsea Jose Mourinho

Paris St. Germain inapambana na Malmo ya Sweden ,ambapo macho yote yatakodolewa kwa mshambuliaji mahiri Zlatan Ibrahimovic akipambana na timu yake ya utotoni mjini Paris kesho Jumanne.

Manchester United ikirejea tena katika kinyang'anyiro hicho itakuwa mjini Eindhoven kupambana na PSV Eindhoven katika mchezo wa kundi B kesho.

Cristiano Ronaldo atakodolea macho kupata rekodi nyingine zaidi za kufunga mabao wakati Real Madrid itakapozindua kampeni yake nyumbani dhidi ya Shakhtar Donetsk hapo kesho.

Spanien Fußball Real Madrid Cristiano Ronaldo

Cristiano Ronaldo mshambuliaji wa Real Madrid

Manchester City ikiingia katika msimu wa sita wa Champions League mara hii itawania kupata dawa ya kupambana na vilabu vikubwa barani humo wakati kikosi cha kocha Manuel Pellegrini kina kibarua kigumu dhidi ya makamu bingwa wa kombe hilo Juventus Turin kesho Jumanne.

Waendesha mashitaka kutoa taarifa ya FIFA

Mwendesha mshitaka kutoka Marekani Loretta Lynch ataitisha mkutano na waandishi habari hii leo mjini Zurich , Uswisi kutoa maelezo kuhusiana na uchunguzi katika kashfa ya rushwa inayowakabili watendaji kadhaa wa shirikisho la kandanda duniani FIFA.

Lynch atajiunga na mwenzake kutoka Uswisi Michael Lauber , ambaye ameanzisha uchunguzi tofauti kuhusiana na chombo cha utawala wa shirikisho hilo ambalo lina makao yake makuu nchini Uswisi.

Lynch na Lauber wanahudhuria mkutano wa chama cha kimataifa cha waendesha mashitaka katika mji huo wa Uswisi.

FIFA ilitumbukia katika mtafaruku Mei 27 mwaka huu wakati watendaji 14 wa masoko katika michezo na maafisa wa kandanda , ikiwa ni pamoja na wengine kadhaa kutoka FIFA waliposhitakiwa nchini Marekani kwa kupokea hongo, kusafisha fedha na udanganyifu madai yanayohusiana na malipo ya dola milioni 150.

Kwa taarifa hiyo ndio sina budi kusema tumefikia mwisho wa kuwaletea ukurasa huu wa michezo mwishoni mwa juma. Jina langu ni Sekione Kitojo. Kwaherini.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre / dpae

Mhariri: Iddi Ssessanga